
Kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozize, imeanza kusikilizwa katika Mahakama Maalumu inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui.
Rais huyo wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati anatuhumiwa kuhusika na makosa yauhalifu dhidi ya ubinadamu yanayodaiwa kufanywa kati ya mwaka 2009 na 2013.
Bozize, ambaye aliongoza taifa hilo kuanzia mwaka 2003 hadi alipoondolewa madarakani mwaka 2013, anashtakiwa akiwa nje ya nchi huku akiishi uhamishoni nchini Guinea-Bissau. Miongoni mwa tuhuma zinazomkabili ni mauaji, mateso, utekaji wa watu kwa nguvu na ubakaji unaodaiwa kufanywa na wanajeshi wa kikosi chake cha ulinzi wa Rais.
Maafisa watatu wa zamani wa jeshi wanaohusishwa na kesi hiyo wanashikiliwa na mamlaka husika nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati humo na wanatarajiwa kushtakiwa pamoja na mchakato wa kesi kuendelea.
Mahakama hiyo maalumu ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa Bozize mwaka 2024 baada ya uchunguzi kubaini ushahidi unaomhusisha na makosa hayo akiwa kiongozi wa juu wa jeshi na serikali.
Jamhuri ya Afrika ya Kati ilitumbukia katika machafuko baada ya waasi wa Muungano wa Seleka kumuondoa madarakani Francois Bozize mwaka 2013. Tukio hilo lilifuatiwa na mauaji yaliyofanywa na wanamgambo wa Kikristo wa kundi la Anti Balaka.
Bozize mwenyewe alikimbilia Cameroon kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, lakini alirejea nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2019 kutangaza kugombea kwake katika uchaguzi uliopangwa kufanyika nchini humo. Mahakama ya Kikatiba iliamua kwamba hakukidhi matakwa ya “maadili mema” kwa sababu ya madai yake ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.