Tangu mlipuko huo utangazwe rasmi tarehe 15 Mei mwaka huu, maendeleo makubwa yamepatikana katika uwezo wa upimaji wa virusi, amesema Tarik Jašarević, msemaji wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO), akiwaambia waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswisi.

Vipimo vya virusi vya Bundibugyo vinavyosababisha mlipuko huo sasa vinapatikana katika maeneo sita nchini DRC ambayo ni Bunia na Mongbwalu katika Jimbo la Ituri, Bukavu na Lwiro katika jimbo la Kivu Kusini, Goma katika jimbo la Kivu Kaskazini, pamoja na mji mkuu wa nchi hiyo Kinshasa.

Maabara nyingine nne pia zimeanzishwa nchini Uganda, ambako ugonjwa huo uliingizwa kutoka DRC. Hadi sasa, Uganda imethibitisha wagonjwa 19 na mgonjwa mmoja anayeshukiwa.

Hata hivyo, WHO imesema bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

© WHO/Joël Lumbala WHO inawahamasisha watu huko Nyankunde, Ituri mashariki mwa Congo kuhusu jinsi ya kuzuia kuenea kwa Ebola.

Kuvunja mnyororo wa maambukizi

“Tuna maeneo ambayo taarifa za tahadhari ni chache sana,” amesema Jašarević. “Inawezekana kuna minyororo ya maambukizi ambayo bado haijagunduliwa. Bado kuna watu wanaoweza kuwaambukiza wengine, na tunahitaji kuwafikia.”

Kwa upande wake, Bruno Michon, Meneja wa Operesheni za Mlipuko wa Ebola katika Shirikisho la Kimataifa la Chama cha Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), amesisitiza kuwa ili kudhibiti ugonjwa huo, uwekezaji hauhitajiki tu katika huduma za matibabu bali pia katika kujenga imani ya jamii.

“Jambo hilo linahitaji muda na si rahisi. Lakini katika mlipuko huu si chaguo la ziada. Linaokoa maisha,” amesema.

Akizungumza kutoka Bunia, kitovu cha mlipuko huo, Michon amesema baadhi ya watu bado wana mashaka kuhusu ugonjwa huo.

“Baadhi ya watu bado wanahoji kama ugonjwa huu ni wa kweli,” amesema. “Wengine wanaamini kuwa mlipuko huu umebuniwa ili kuvutia misaada kutoka nje.”

Ameongeza kuwa baadhi ya wananchi wanaona taratibu za mazishi salama na yenye heshima kama shambulio dhidi ya tamaduni na mila zao badala ya hatua za kulinda familia na jamii.

Hofu na taarifa potofu zakwamisha mapambano

Mashaka, hofu na kutokuamini vimeendelea kuathiri juhudi za kukabiliana na Ebola mashariki mwa DRC, eneo ambalo kwa muda mrefu limekumbwa na migogoro ya silaha.

Kutokuamini mamlaka za nje kunachangia kuongezeka kwa hatari ya maambukizi kuenea zaidi.

Kwa mujibu wa WHO katika siku za mwanzo za mlipuko huo, vituo viwili vya matibabu ya Ebola vilichomwa moto katika eneo hilo ambalo pia limekumbwa na mapigano makali yaliyowalazimu zaidi ya watu 100,000 kuyahama makazi yao.

Wakati huo, WHO ilieleza kuwa mashambulizi hayo yalihusishwa na kampeni za taarifa potofu zilizokuwa zikisambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

“Watu wanapokuwa na hofu, wanaweza wasiripoti dalili za ugonjwa,” amesema Michon. “Wanaweza kuepuka vituo vya matibabu kwa kuogopa kuambukizwa na badala yake kubaki nyumbani wanapopata homa.”

Ameongeza kuwa baadhi ya wagonjwa hujisitiri kwa sababu ya unyanyapaa unaohusishwa na Ebola.

“Wanaona aibu kuwaambia wanafamilia wao kwamba ni wagonjwa.”

Pia amesema familia nyingi huendelea kuwazika wapendwa wao kwa kufuata mila za jadi bila kufahamu kiwango cha hatari kinachohusika.

© UNICEF/John James Timu ya wataalamu wa usafi ikiua vijidudu kwenye hema huko Bunia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kusikiliza jamii ndiyo njia ya kujenga imani

Michon amesema imani hujengwa kwa kusikiliza hofu za wananchi na kujibu kwa vitendo vinavyoonyesha heshima kwa jamii.

“Baada ya kusikia maoni ya wananchi, tulianza kutumia mifuko ya kuhifadhia miili yenye sehemu ya uwazi ili familia ziweze kuuona uso wa marehemu na kuanza mchakato wa maombolezo,” amesema.

Ameongeza kuwa wakati baadhi ya wananchi walipohofia kuwa dawa ya klorini ilikuwa ikitumika kuwapa sumu, wahudumu wa afya hawakubishana nao.

“Badala yake tuliwaonyesha jinsi dawa hizo za usafishaji zinavyoandaliwa.”

Kwa mujibu wa Michon, imani ndiyo msingi wa mafanikio yote katika mapambano dhidi ya Ebola.

“Bila imani, hatuwezi kugundua wagonjwa mapema. Hatuwezi kuhakikisha mazishi salama na yenye heshima. Hatuwezi kuwalinda familia, wala hatuwezi kusitisha maambukizi.”

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa, “Imani si shughuli ya kando katika hatua za kudhibiti Ebola. Imani ndiyo kiini cha kila kitu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *