Fursa mpya ya uwekezaji na maandalizi ya maisha ya baada ya kustaafu imefunguliwa kwa Watanzania wanaofanya kazi katika sekta rasmi na isiyo rasmi baada ya uzinduzi wa Foresight Private Retirement Fund (FPRF), mfuko wa uwekezaji wa kustaafu uliopata idhini kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mtaalamu wa Masoko ya Mitaji na Dhamana, Dkt. Ibrahimu Mwangalaba, amesema mfuko huo unaziba pengo lililokuwepo kwa wananchi wengi, hususan wa sekta isiyo rasmi, ambao kwa muda mrefu wamekosa fursa rahisi za kujiwekea akiba na kuwekeza kwa ajili ya maisha ya baadaye.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa CORE Securities Limited, CPA George Fumbuka, amesema FPRF imeundwa kwa unyumbufu zaidi ikilinganishwa na mifumo ya kawaida ya pensheni, huku ikiruhusu wananchi kuanza uwekezaji kwa kiwango cha chini cha Sh10,000. Ameongeza kuwa mfuko huo una mipango maalumu kulingana na umri wa mwekezaji ili kukidhi mahitaji tofauti ya kifedha.
CPA Fumbuka amesema wawekezaji wataweza kupata mafao yao baada ya miaka mitano kwa njia ya mkupuo, pensheni ya kawaida au mchanganyiko wa njia hizo.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Nelson Mabula, alisema chama hicho kitaendelea kuwahamasisha wanachama wake kushiriki katika mfuko huo kutokana na manufaa yake katika kujenga ustawi wa kifedha wa muda mrefu.
#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

(Feed generated with FetchRSS)