Ripoti hiyo “Hali ya uvuvi na ufugaji Samaki duniani 2026” (SOFIA) iliyotolewa mjini Roma Italia inaonesha kuwa wakati uzalishaji wa samaki wa kuvuliwa baharini na kwenye maji ya asili umeendelea kubaki katika kiwango kilekile kwa zaidi ya miongo minne, ufugaji wa samaki, kaa, kamba na viumbe wengine wa majini umeibuka kuwa injini kuu ya ukuaji wa uzalishaji wa chakula duniani.

Ufugaji samaki ndiyo sekta inayokua kwa kasi zaidi duniani

Akizungumzia kuhusu matokeo ya ripoti hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uvuvi na Ufugaji wa Samaki wa FAO, Manuel Barange, amesema ukuaji wa sekta hiyo umeendelea kuwa thabiti kwa zaidi ya miaka 20.

“Ufugaji wa viumbe maji unaendelea kuwa mfumo wa uzalishaji wa chakula unaokua kwa kasi zaidi duniani. Tangu mwanzoni mwa karne hii umekuwa ukikua kwa wastani wa karibu asilimia tano kila mwaka, na mwenendo huu bado unaendelea,” amesema Barange.

Ameongeza kuwa wakati uvuvi wa asili umeendelea kuwa imara kwa takribani miaka 40, ukuaji wa ufugaji samaki unaongeza uzalishaji unaohitajika ili kuimarisha uhakika wa chakula na lishe kwa mamilioni ya watu duniani.

Afrika bado iko nyuma, lakini fursa ni kubwa

Pamoja na mafanikio hayo, FAO imeonya kuwa uzalishaji wa sekta ya ufugaji viumbe maji bado umejikita zaidi barani Asia, jambo linaloonesha pengo kubwa la maendeleo baina ya mabara.

“Takriban asilimia 90 ya uzalishaji wote wa ufugaji samaki duniani unafanyika Asia. Afrika inachangia chini ya asilimia 2.5 pekee ya uzalishaji wa dunia,” amesema Barange.

Kwa mujibu wake, hali hiyo inaonesha fursa kubwa kwa Afrika kuongeza uzalishaji wake wa samaki na viumbe wengine wa majini ili kuboresha upatikanaji wa protini, lishe bora na uhakika wa chakula kwa watu wake wanaoongezeka kwa kasi.

Uzalishaji eatarajiwa kuongezeka zaidi kufikia 2034

Ripoti hiyo inatabiri kuwa uzalishaji wa samaki, kaa, kamba, chaza na viumbe wengine wa majini utaendelea kuongezeka katika miaka ijayo, ukifikia tani milioni 214 ifikapo mwaka 2034.

FAO inakadiria kuwa karibu tani milioni 20 za ziada zitaongezwa katika sekta ya uvuvi na ufugaji wa viumbe maji ndani ya muongo mmoja ujao, huku asilimia 85 ya ongezeko hilo likitokana na ufugaji samaki.

“Kufikia mwaka 2034, matumizi ya vyakula vya majini yatafikia karibu kilo 22 kwa kila mtu duniani, kutoka kilo 21.3 za sasa,” amesema Barange. “Hii itachangia zaidi kuboresha uhakika wa chakula na lishe ya watu duniani.”

Tahadhari juu ya uvuvi usio endelevu

Licha ya ukuaji huo wa kuvutia, FAO imeonya kuwa rasilimali za baharini zinaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa zaidi ya theluthi moja ya hifadhi za samaki duniani bado zinavuliwa kwa kiwango kisicho endelevu.

“Uendelevu wa rasilimali za baharini bado ni changamoto kubwa. Asilimia 62 ya maeneo ya uvuvi duniani ndio yanayovuliwa kwa njia endelevu, maana yake zaidi ya theluthi moja bado hayatumiki kwa njia salama,” amesema Barange.

Hata hivyo, ripoti inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 72 ya samaki wanaovuliwa duniani hutoka katika hifadhi zinazodhibitiwa vizuri, jambo linaloonesha umuhimu wa usimamizi bora wa sekta hiyo.

Mabadiliko ya tabianchi yatabadilisha ramani ya uvuvi duniani

FAO pia imeonya kuwa mabadiliko ya tabianchi yataathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya uvuvi katika miongo ijayo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, ongezeko la joto duniani linaweza kupunguza zaidi ya asilimia 10 ya hifadhi ya samaki wanaoweza kuvuliwa katika maeneo kadhaa duniani ifikapo mwaka 2050.

“Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri uzalishaji wa baadhi ya aina za viumbe maji na pia kubadilisha maeneo zinakoishi,” amesema Barange. “Hii inabadilisha kila kitu katika sekta ya uvuvi mahali pa kuvua, aina ya samaki wanaovuliwa, namna ya kusimamia rasilimali hizo na hata kile kinachofika sokoni kwa walaji.”

Amesisitiza kuwa kukabiliana na mabadiliko hayo kutahitaji maboresho katika sera, mifumo ya usimamizi, shughuli za uvuvi na hata kuandaa njia mbadala za kujikimu kwa jamii zitakazoathirika zaidi.

Kwa sasa, ujumbe wa FAO ni bayana, wakati ufugaji viumbemaji unaendelea kuwa tegemeo jipya la dunia katika kuzalisha chakula, uwekezaji katika uendelevu na usawa wa maendeleo ndio utakaoamua kama sekta hiyo itaweza kulisha dunia ya kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *