Chanzo cha picha, Reuters
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4
Uongozi wa Iran umekuwa ukipendekeza makubaliano na Marekani kama ushindi kutokana na ustahimilivu wao ila hoja hiyo si rahisi kukubalika haswa na raia wa Iran.
Taifa hilo limepitia wakati mgumu, uchumi wao umeathirika pakubwa huku wanaounga mkono Iran wakikanusha kila siku kuwa hawatalegeza Kamba ikija katika matakwa yao na Washington.
Ila kuna raia wa Iran ambao wapo ndani na nje ya nchi hiyo ambao hawaoni kama diplomasia ndiyo itatatua mgogoro uliopo, ila kwao ni nafasi nzuri ya kubadilisha utawala wa Iran.
Maafisa wakuu wa Israel wametangaza makubaliano na Marekani kama ushindi. Mohammed Bagher Qalibaf, spika wa bunge la Iran alisema “Iran imechukua hatua ndefu kufikia ushindi huu”
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amesema makubaliano hayo yataleta mageuzi, na iwapo yatatekelezwa kikamilifu, yatatatua matatizo mengi ya Iran yaliyoletwa na ‘watu tofauti’ nchini humo na Mashariki ya kati.
Semi za Qalibaf zina uzito, kwani inaonyesha kuwa makubaliano na Marekani yanaungwa mkono na viongozi wengine wakuu wa Iran ikiwemo jeshi la IRGC.
Chanzo cha picha, Getty Images
Uongozi wa Iran pia unatangaza makubaliano hayo kuwa ushindi kwani Marekani na Israel wameshindwa kuafikia malengo yao katika vita walivyoanzisha nchini Iran.
Walishindwa kuishinikiza Iran kujisalimisha, walishindwa kubadilisha mfumo wa uongozi wa kiislamu, na hawakuweza kumaliza mpango wa nyuklia wa Iran kupitia nguvu za kijeshi, na pia hawakuvunja uhusiano wa Iran na Hezbollah.
Licha ya yote, Iran bado ina uwezo wa kufanya majadiliano, huku Lebanon ikijumuishwa katika makubaliano yao ya kupatikana kwa amani.
Ila simulizi ya Iran kuwa imeshinda vita, inapokea changamoto ndani ya Iran.
Mbunge mmoja mwenye msimamo mkali nchini Iran, amesema makubaliano hayo yataigeuza Iran kuwa chini ya utawala wa Marekani. Pia aliwashtumu wapatanishi wa Iran kwa kuenda kinyume na agizo la kiongozi mkuu wa kutofungua Mlango Bahari wa Hormuz.
Ukosoaji huo una uzito kwani unatoka ndani ya utawala wa Iran.
Kwa miezi kadhaa, viongozi tofauti, vyombo vya habari wamekuwa wakisisitiza kuwa Marekani si taifa ya kuaminiwa.
Kulingana na Iran, vita vilianza wakati mazungumzo yanaendelea, na kuishtumu Marekani kwa kutumia kipindi cha mazungumzo kujiandaa kwa vita Pamoja na Israel.
Makubaliano na Marekani awali yalipokea pingamizi nyingi, ila kwa sasa, sauti za ukosoaji zimepungua, kumaamisha makubaliano hayo yameidhinishwa na ngazi ya juu ya uongozi wa taifa hilo.
Kwa sasa huenda uongozi wa taifa hilo umetathmini kuwa kukataa makubaliano hayo utakuwa na athari kubwa zaidi.
Chanzo cha picha, EPA
Shinikizo la kiuchumi ni sehemu kubwa ya Iran kukubali kuafikia makubaliano na Marekani.
Vita, vikwazo vya kiuchumi, vizuizi vya usafirishaji wa meli, kupungua kwa upatikanaji wa masoko ya mafuta na fedha za kigeni, pamoja na mfumuko mkubwa wa bei, vyote vimeendelea kuibana nchi hiyo na raia wa kawaida wa Iran.
Kwa familia nyingi za Kiirani, swali kuu si kama makubaliano hayo yanaonekana kuwa ushindi, bali ni kama yatashusha gharama za maisha na kupunguza hofu ya kuzuka kwa duru nyingine ya vita.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema kuwa Iran haitapokea fedha za walipa kodi wa Marekani, lakini inaweza kupata mabilioni ya dola ikiwa itatekeleza ahadi zake na vikwazo vya kiuchumi vitaondolewa.
Hilo linaipa Tehran nafasi ya kuwasilisha makubaliano hayo kama njia ya kuvutia uwekezaji na kujenga upya uchumi wake, badala ya kuonekana kuwa inategemea Marekani.
Hata hivyo, hatari bado zipo wazi. Maelezo kamili ya makubaliano hayo hayajachapishwa rasmi, na mazungumzo zaidi yanatarajiwa kuanza nchini Uswisi siku ya Ijumaa.
Masuala magumu zaidi bado hayajatatuliwa kikamilifu yakiwemo hatma ya urani iliyorutubishwa ya Iran, kiwango cha urutubishaji kitakachoruhusiwa, kuondolewa kwa vikwazo, suala la Mlango-Bahari wa Hormuz na hali ya Lebanon.
Pia kuna hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu Israel. Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, amekanusha taarifa kwamba Israel itaondoa wanajeshi wake kusini mwa Lebanon, akisisitiza kuwa majeshi ya Israel yataendelea kubaki huko.
Wakati huo huo, Donald Trump ameikosoa hadharani Israel kuhusu operesheni zake nchini Lebanon, akisema watu wengi sana wameuawa. Pia alisema hakuridhishwa na shambulio la Israel mjini Beirut lililofanyika muda mfupi kabla ya makubaliano kati ya Iran na Marekani kuafikiwa, ingawa alisisitiza kuwa uhusiano wake na Netanyahu unaendelea vizuri.
Ila makubaliano hayo yanaonekana kuwa dhaifu, Ikiwa Israel itaendelea na operesheni zake nchini Lebanon, Iran itakabiliwa na shinikizo la kujibu. Na ikiwa Washington haitafanikiwa kuizuia Israel, madai ya Tehran kwamba Lebanon imejumuishwa katika makubaliano hayo yanaweza kujaribiwa haraka sana.