Mkuu wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen, Mahdi al Mashat, amesifu Majeshi ya Iran, hasa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), akisema utendaji wao wakati wa vita vya Marekani na Israel umeonyesha ustahimilivu, azma thabiti, na nguvu ya kijeshi.

Al‑Mashat siku ya Jumanne aliipongeza uongozi na wananchi wa Iran kwa ushindi katika vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Marekani na Israel.

Amesema mafanikio ya Iran yanahudumia maslahi ya mataifa ya kanda pamoja na ulimwengu mpana wa Kiislamu, huku yakichangia kuimarisha usalama na uthabiti wa kikanda.

Aidha, amesifu namna Iran ilivyosimamia vita hivyo, akisisitiza majibu madhubuti ya Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya mashambulizi pamoja na kulengwa kwa maslahi na kambi za wale aliowataja kuwa wachokozi.

Amesema majibu ya kijeshi ya Iran, pamoja na ustahimilivu wa wananchi na mshikamano wa kitaifa, yamechangia kwa kiasi kikubwa kusitisha mashambulizi na kuwazuia wachokozi kufikia malengo yao.

Afisa huyo wa Yemen pia amesema msimamo wa Iran juu ya kanuni ya “umoja wa mhimili wa muqawama” ulichangia kuilazimisha Israel kusitisha mashambulizi dhidi ya Lebanon.

Ameongeza kuwa “adui huelewa lugha ya nguvu pekee,” akibainisha kwamba sera za maridhiano au kujisalimisha huzaa shinikizo na madai zaidi.

Al‑Mashat pia ametoa wito wa kuongeza umakini, kulinda mafanikio yaliyopatikana, na kuendelea kushikamana na kanuni ya umoja wa mhimili wa muqawama.

Wakati huo huo, mamia ya maelfu ya Wayemen walifanya maandamano makubwa katika mji mkuu Sanaa na miji mingine siku ya Jumanne wakisherehekea “ushindi wa kihistoria” wa Iran dhidi ya Marekani na Israel, huku wakilaani matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mji mtakatifu wa Makka.

Kwa mujibu wa ripoti, maandamano hayo yalivutia washiriki wanaokadiriwa kufikia mamilioni katika zaidi ya viwanja 220 vya umma katika majimbo 14, huku waandamanaji wakipeperusha bendera za Yemen, Iran, Palestina, Lebanon na Iraq na kupaza sauti kuunga mkono kile walichokiita “mhili wa muqawama.”

Katika taarifa iliyotolewa na waandamanaji, walitoa pongezi kwa Iran, Hizbullah, na mhimili wa Jihad na Muqawama kwa ushindi wa kihistoria dhidi ya “majeshi ya kihalifu ya dunia,” wakisema pia kuwa “tusi la Trump dhidi ya Makka linaonyesha hali yake ya kisasi iliyokuja sambamba na kushindwa kwake kihistoria.”

Katika taarifa tofauti, kiongozi wa Ansarullah, Abdul‑Malik al‑Houthi, ameipongeza Iran, uongozi wake na wananchi wake, kwa ushindi katika kukabiliana na “madhalimu wenye kiburi wa zama hizi, Marekani na Israel,” huku akiwataka Wayemen kuunganisha juhudi za kumaliza mzingiro wa Saudi‑Marekani dhidi ya Yemen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *