Katika ujumbe wake kwa Siku ya Kukabiliana na Kuenea kwa Jangwa na Ukame Duniani inayoadhimishwa Juni 17 kila mwaka, Guterres amesema hali hiyo inatishia uhakika wa chakula, maisha ya mamilioni ya watu na afya ya mazingira duniani.

“Maeneo ya malisho ni nafasi kubwa za wazi zinazopatikana katika kila hali ya hewa na katika kila bara,” amesema Katibu Mkuu. 

Ameeleza kuwa maeneo hayo yanafunika karibu nusu ya uso wa ardhi duniani, yakitoa chakula na ulinzi muhimu huku yakitegemewa na zaidi ya watu bilioni mbili kwa maisha yao ya kila siku.

Habari za UN/Daniel Dickinson Faru mweusi amepumzika katika Hifadhi ya Wanyama ya Selous nchini Tanzania. (faili)

Nguzo muhimu kwa bayoanuwai na vita dhidi ya tabianchi

Mbali na kusaidia uzalishaji wa chakula, Guterres amesema maeneo ya malisho yana mchango mkubwa katika kuhifadhi bayoanuwai na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Maeneo hayo ni makazi muhimu ya wanyamapori na pia hufanya kazi kama visima vya asili vya kufyonza hewa ukaa kutoka angani.

Hata hivyo, ameonya kuwa uharibifu unaoendelea wa maeneo hayo unasababisha kupungua kwa bayoanuwai, kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi chafuzi na kudhoofisha mifumo ya chakula duniani. 

“Hali hizi zinatishia mfumo wa chakula duniani, zinadhuru maisha ya watu wa maeneo hayo na kuongeza uzalishaji wa gesi chafuzi,” amesema.

Wito wa uwekezaji na ushirikiano wa kimataifa

Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu ametoa wito wa kuwekeza zaidi katika urejeshaji wa maeneo ya malisho, hususan kupitia kuimarisha usalama wa maji na kusaidia jamii za vijijini kupata ajira endelevu. 

© World Bank Musa Idris, mkulima mnufaika wa kilimo cha umwagiliaji kutoka Jimbo la Jigawa, kaskazini mwa Nigeria.

Pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa ili kupata suluhu zinazovuka mipaka ya nchi.

“Mwaka huu pia unaadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Maeneo ya Malisho na Wafugaji, fursa ya kusaidia wafugaji na watu wa jamii za asili ambao maarifa yao ya jadi yanaweza kusaidia kulinda mifumo hii ya ikolojia,” aamesema. Ameongeza kuwa maarifa hayo yanaweza kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuhifadhi ardhi na kukabiliana na kuenea kwa jangwa.

Akihitimisha ujumbe wake, Guterres amesisitiza kuwa mustakabali wa binadamu unategemea afya ya ardhi. “Ili kulinda mustakabali wetu, lazima tuilinde ardhi. Pamoja, hebu tuhakikishe kwamba maeneo ya malisho kila mahali yanastawi kwa ajili ya vizazi vijavyo.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *