
Dodoma. Wakulima na wafugaji nchini wametakiwa kutumia bima za kilimo ili kujikinga dhidi ya hasara zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali, huku wakihimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya viuatilifu ili kuongeza ubora wa mazao na kunufaika na masoko ya ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa leo Jumatano, Juni 17, 2026, jijini Dodoma na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) pamoja na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Ofisa Bima wa Tira, Gladys Steven amesema bima za kilimo ni nyenzo muhimu kwa wakulima na wafugaji katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ukame, mafuriko na magonjwa ya mifugo.
“Bima za kilimo ni kinga muhimu dhidi ya majanga yasiyotabirika yanayoweza kuathiri uzalishaji na kusababisha hasara kubwa za kiuchumi,” amesema.
Amesema huduma hizo zinapatikana kwa wakulima na wafugaji wa aina zote, wakiwamo wanaoshiriki kupitia vyama vya ushirika na Amcos.
Ameongeza kuwa Tira inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia maonyesho, vyombo vya habari na ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima za kilimo.
Kwa mujibu wa Gladys, mwamko wa wakulima kujiunga na bima umeongezeka na hatua hiyo inawasaidia kupata mikopo kwa urahisi kutoka taasisi za kifedha.
Kwa upande wake, Meneja wa TPHPA, Musa Chilinda amesema mamlaka hiyo inaendelea kusimamia matumizi ya viuatilifu na afya ya mimea, ili kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanakuwa salama na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Amesema TPHPA husimamia mnyororo mzima wa viuatilifu kuanzia uingizaji, usafirishaji, uuzaji hadi matumizi yake ili kuhakikisha wakulima wanapata bidhaa zenye viwango vinavyokubalika.
“Tunatoa ushauri na maelekezo sahihi kwa wakulima ili wapate mazao bora yanayokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi,” amesema.
Chilinda amesema mamlaka hiyo pia hufanya ukaguzi wa afya ya mimea mashambani na mipakani ili kudhibiti wadudu na magonjwa yanayoweza kuhatarisha uzalishaji wa mazao na biashara ya kimataifa.
Ametaja baadhi ya vihatarishi vinavyofuatiliwa kuwa ni pamoja na nondo wa parachichi aina ya false codling moth na inzi wa matunda.
Naye Meneja wa Maridhia Afya ya Mimea na Uwezeshaji Masoko kutoka Wizara ya Kilimo, Mahamudu Sasamalo amesema wakulima wanapaswa kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kunufaika na masoko ya kimataifa, ikiwemo soko jipya la ndizi nchini Afrika Kusini.
Amesema mafanikio ya kufunguliwa kwa soko hilo yametokana na majadiliano ya muda mrefu ya kitaalamu yaliyowezesha kuruhusiwa kwa usafirishaji wa ndizi aina ya plantain.
Sasamalo amesema masoko mapya yataongeza kipato cha wakulima, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuendelea kufungua fursa za ajira kwa wanawake na vijana.