Nchini Zimbabwe, uamuzi wa mahakama uliotupilia mbali pingamizi la kisheria lililotolewa na maveterani wa vita dhidi ya marekebisho ya katiba umesababisha hisia tofauti.

Siku ya Jumatano, Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo ilifungua njia ya mageuzi ya Katiba ambayo yanaweza kuongeza muda wa urais kutoka miaka mitano hadi saba, na hivyo kumruhusu Rais Emmerson Mnangagwa kubaki madarakani hadi mwaka wa 2030.

Mjini Harare, wauangaji mkono wa serikali walikusanyika nje ya mahakama wakifurahia hukumu hiyo. Silvesta Hashiti, wakili anayemwakilisha rais Emmerson Mnangagwa, alisema waliowasilisha mashtaka “wameshindwa kuthibitisha utovu wa nidhamu kwa upande wa rais” na hawana msingi wa kisheria wa kesi yao.

Hata hivyo mawakili wa upinzani na maveterani wa vita waliohusika katika kesi hiyo wanasema hawajakata tamaa. Lovemore Madhuku, wakili anayewawakilisha maveterani wa vita wa Zimbabwe anmesema wateja wake “wanaheshimu uamuzi wa mahakama” lakini “hawakatishwi tamaa” na uamuzi huo.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba ya Zimbabwe ambao umefungua njia ya mageuzi ya Katiba pia umeibua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya wachambuzi wa kisiasa, kama Precious Shumba, ambaye amedai kuwa unatishia demokrasia ya Zimbabwe.

“Uamuzi huo wa mahakama unaonyesha mmomonyoko wa mahakama yetu na watendaji na hii ina maana ya kifo cha demokrasia yetu ya kikatiba,” amesema Shumba.

Marekebisho ya Katiba ya Zimbabwe yataongeza muhula wa Rais Emmerson Mnangagwa kwa miaka miwili hadi 2030.

Pia marekebisho hayo yatafuta Uchaguzi Mkuu wa Rais, na kulipa Bunge mamlaka ya kumteua mkuu wa nchi.

Zaidi ya hayo, mabadiliko yaliyopendekezwa, yaliyowasilishwa na Waziri wa Sheria Ziyambi Ziyambi katika Bunge, yataruhusu wabunge kuongezwa muda wao kutoka miaka mitano hadi saba.

Wakosoaji wanasema marekebisho hayo yataimarisha udhibiti wa chama cha Zanu-PF, ambacho kimetawala nchi hiyo yenye utajiri wa rasilimali tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1980.

Mnangagwa aliingia madarakani mwaka wa 2017 katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na jeshi yaliyomng’oa madarakani Robert Mugabe ambaye alikuwa rais wa Zimbabwe kwa kipindi cha miaka 30.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *