Dar es Salaam. Raia wanne wa China wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kuteka nyara kwa nia ya kuleta madhara pamoja na kutakatisha fedha kiasi cha Sh313 milioni.

Washtakiwa hao ni mchimba madini, Deng Anqing (50), watafiti wawili wa kilimo Fan Hua (53) na Zhang Jianjun (51) pamoja na mchimbaji madini Deng Qiang(40).

Wamefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi Juni 18, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 13513 ya mwaka 2026 na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Dhamili Masinde akisaidiana na Judith Kyamba, mbele ya Hakimu Mfawidhi, Herieth Mwailolo.

Kabla ya kusomewa mashtaka yao, hakimu Mwailolo amewaeleza washtakiwa hao kuwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Pia shitaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote, halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo wataendelea kusalia rumande hadi upelelezi utakapokamilika.

Hakimu Mwailolo baada ya kutoa maelekezo hayo, wakili Kyamba amewasomea mashitaka yao.

Wakili Kyamba amedai washtakiwa wanatuhumiwa kwa makosa matatu  yakiwamo kuongoza genge la uhalifu, kuteka nyara kwa nia ya kudhuru na utakatishaji fedha kinyume cha sheria.

Amedai katika shitaka la kwanza, ambalo ni kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili na Mei, 2026 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika kipindi hicho, kwa makusudi waliendesha mtandao wa uhalifu uliokuwa ukijihusisha na utekaji nyara kwa nia ya kusababisha madhara na kujipatia Sh130 milioni pamoja na dola za Marekani 70,000 (Sh183. 54 milioni) mali ya  Weiyi Chen.

“Washtakiwa katika kosa hili wameshtakiwa kinyume na aya ya 4(1) ya Jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1) na 19(2) vya Sheria ya kudhibiti makosa ya kiuchumi na uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, toleo la mwaka 2023,”amedai wakili Kyamba.

Shitaka la pili ni kuteka nyara kwa nia ya kudhuru linalowakabili washtakiwa wote, ambapo wanatuhumiwa wameshtakiwa kinyume na kifungu cha 250 cha kanuni ya adhabu, sura ya 16, toleo la mwaka 2023.

Amedai kuwa Mei 14, 2026 washtakiwa wakiwa katika Jengo la PSSSF Twin Towers, Wilaya ya Ilala, wanadaiwa kuteka nyara  kwa nia ya kusababisha madhara.

Wakili Kyamba ameendelea kuieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la tatu ni kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa wote.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa la kutakatisha  fedha kinyume na kifungu cha 12(1)(d) na 13(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia Utakatishaji wa Fedha, Sura ya 423, toleo la mwaka 2023, kikisomwa pamoja na aya ya 22 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 19(2) vya aheria ya kudhibiti makosa ya kiuchumi na uhalifu wa kupangwa, Sura ya 200, toleo la mwaka 2023.

Ilidaiwa kuwa Mei 15, 2026 katika mgahawa wa Zhe Jiang, uliopo Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja walijipatia Sh130 milioni pamoja na dola za Marekani 70,000 (sawa na Sh183.4 milioni), mali ya Chen huku wakijua au wakiwa na sababu za kuamini kwamba fedha hizo zilikuwa mapato yaliyotokana na kosa la msingi la utekaji nyara kwa nia ya kusababisha madhara.

Hata hivyo, washtakiwa hao wakiwa wanatafsiriwa na mkalimani aitwaye Olivia kwa lugha ya Kichina hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Upande wa mashtaka walidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mwailolo ameahirisha kesi hadi Julai 2, 2026 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *