
Hat trick zimeanza kuitika Ligi Kuu baada ya straika wa Pamba Jiji, Mathew Tegisi kufanya hivyo akiiongoza timu yake kuichakaza Mtibwa Sugar mabao 4-0.
Mkenya Tegisi ameungana na staa wa Singida Black Stars, Mossi Nduwumwe aliyefanya hivyo jana wakati timu yake ikishinda mabao 5-0 dhidi ya Dodoma Jiji.
Tangu kuanza msimu wa Ligi Kuu 2025/26, ilishuhudiwa ukame wa mabao matatu katika mchezo mmoja ‘Hat trick’ katika michezo 26 iliyokuwa imechezwa.
Mrundi Nduwumwe alikuwa wa kwanza msimu huu kufungua akaunti hiyo na leo, nyota wa zamani wa Shabana FC, Tegisi amefuata nyayo hizo.
Tegisi ameonekana kuwa na kiwango bora tangu atue Pamba Jiji na idadi hiyo ya mabao ya leo, amefikisha mabao 11 akizidiwa na Nduwumwe mabao na Feisal Salum wa Azam mwenye mabao 14.
Matokeo hayo yanaiweka pabaya Mtibwa Sugar iliyopoteza mchezo wa pili mfululizo ikianza dhidi ya Mbeya City ilipolala bao 1-0 na kubaki nafasi ya 12 kwa pointi 27.
Ushindi wa Pamba Jiji unaifanya kupanda nafasi ya saba kwa pointi 38 baada ya timu zote kucheza mechi 27 zikibaki tatu pekee kumaliza msimu huu.
Katika mchezo huo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, mabao ya Tegisi amefunga dakika ya 17,46 na 49 huku lingine likifungwa na Shaban Siwa dakika ya 44.