
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5
Mara ya kwanza Bedia Trifonovic alipokwenda nyumbani kwa mwanamke ambaye baadaye alikuwa mke wake, alishangaa sana. Walipoingia kupitia mlango wa mbele, Sofia alimwambia kwamba anaweza kuacha viatu vyake hapo.
Akikumbuka tukio hilo, anasema:
“Mnavaa viatu sehemu mnayolala… hapo ndipo nilihisi kama ni jambo la kuchukiza.”
Kwa upande wake, Sofia Trifonovic, ambaye anaishi nchini Marekani, naye alishangazwa alipogundua kwamba Bedia, ambaye asili yake ni nchini Serbia, alikuwa anavua viatu vyake anapoingia ndani ya nyumba.
“Unataka ninuse miguu yangu ndani ya nyumba yako? Acha nibaki na viatu vyangu vya michezo.”
Hivyo ndivyo alivyohisi katika hali hiyo.
Lakini tofauti hii ya maoni, ingawa inaonekana kuwa ndogo na ya kawaida, haikuwa tu mabishano kati ya wanandoa. Ilionesha mjadala mpana zaidi unaoendelea duniani kuhusu iwapo watu wanapaswa kuvua viatu wanapoingia nyumbani au la, jambo waliloligundua baada ya kueleza kisa chao kwenye mitandao ya kijamii.
Video moja iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii ilipata mamia ya maoni. Video hiyo ilimuonesha Bedia Trifonovic akiwa amevaa viatu vya ndani ya nyumba, huku Sofia Trifonovic akiwa amevaa viatu vya michezo ndani ya nyumba yao.
Video hiyo ilizua mjadala mkubwa kuhusu ni nani kati ya wanandoa hao anayezingatia zaidi usafi.
Kwa hiyo, ni nani aliye sahihi? Na je, kuvaa viatu ndani ya nyumba kunaweza kuwa hatari kwa afya?
Ili kupata majibu ya maswali hayo, BBC ilitembelea maabara ya mikrobiolojia (sayansi ya viumbe vidogo) kuchunguza kama viatu vinavyovaliwa nje vinaweza kuingiza bakteria, vijidudu na uchafu mwingine ndani ya nyumba, na ikiwa hali hiyo inaweza kuathiri afya ya watu wanaoishi humo.
Chanzo cha picha, Sophia Trifunovic
Iwapo utavua viatu vyako au utaendelea kuvivaa ukiwa ndani ya nyumba, huenda ikategemea sana mahali ulipokulia na utamaduni uliokuzunguka.
Katika sehemu kubwa za Mashariki ya Kati, Asia na eneo la Balkani, kuvaa viatu ndani ya nyumba huchukuliwa kuwa ni ukosefu wa adabu. Kinyume chake, katika baadhi ya maeneo ya Ulaya na Marekani, kumwomba mgeni avue viatu vyake kunaweza kuonekana kama kitendo kisicho cha heshima.
Japan ni moja ya nchi zenye msimamo mkali zaidi kuhusu suala hili, kwani nyumba nyingi zina eneo maalum la kuingilia linaloitwa genkan, ambapo watu hutakiwa kuvua viatu vyao kabla ya kuingia sehemu za ndani za nyumba.
Fabio Gygi, mhadhiri mwandamizi wa anthropolojia katika Chuo Kikuu cha SOAS London, anaeleza kwamba ikiwa mtalii atasahau kuvua viatu vyake nchini Japan:
“Kutakuwa na mwitikio wa haraka na mkali sana… watu watakimbilia kukuzuia wakisema: Hapana, simama, vua viatu vyako.”
Anaongeza kuwa mwitikio huo unatokana na sababu za kiafya pamoja na mitazamo ya kifalsafa.
Aliendelea kusema:
“Una maana ya kiishara, kwa kuwa mazingira ya nje huonekana kuhusishwa na uchafuzi, hatari na kila kitu kichafu.”
Pia alisema:
“Ndani ya nyumba ni mahali ambapo unataka kudumisha usafi na utakatifu… na usafi ni hali ambayo mwanadamu hutafuta kufikia, na ibada nyingi za kidini zimejengwa juu ya wazo hilo.”
Kwa hiyo, katika tamaduni nyingi, kuvua viatu si suala la usafi pekee, bali pia ni ishara ya heshima, utaratibu na kutenganisha mazingira ya nje yanayoweza kuwa machafu na mazingira ya ndani yanayotakiwa kubaki safi.

Bakteria gani hupatikana kwenye viatu?
Tulichukua jozi ya viatu vya michezo ambavyo vilikuwa vimetumika kutembea mjini Brighton, Uingereza, wikendi iliyopita na kuvipeleka kwenye maabara ya microbiolojia ili kuona vilikuwa na nini.
Katika Chuo Kikuu cha Brighton, mtaalamu wa mikrobiolojia Sarah Pitt alichukua sampuli kutoka juu na chini ya kiatu, kisha akaacha sampuli hizo zikue kwenye sahani ya maabara kwa usiku mmoja.
Siku iliyofuata, uchunguzi wa hadubini wa sampuli ulionesha uwepo wa bakteria wengi.
Miongoni mwao kulikuwa na Staphylococcus aureus, bakteria wanaosababisha maambukizi kwenye mw baktera ambao kwa mujibu wa Pitt wanaweza kuwa “hatari” hata kwa watu wenye afya nzuri.
Pitt alieleza: “Ukichana au kujikwaruza na bakteria hawa wakaingia mwilini, wanaweza kusababisha jipu kubwa lenye usaha.”
Alisema pia kwamba bakteria hawa wanaweza kusababisha homa ya mapafuna sumu ya damu kwa watu wenye kinga dhaifu ya mwili.
Viatu hivyo pia vilikuwa na bakteria wanaoitwa Staphylococcus epidermidis, ambao kwa kawaida huishi kwenye ngozi ya binadamu. Bakteria hawa wanaweza kusababisha magonjwa makubwa kwa watu wenye kinga dhaifu, na mara nyingi maambukizi yao hupatikana hospitalini.
Tafiti nyingine na mapitio ya kisayansi zimeonesha kuwa viatu vinaweza pia kuchafuliwa na aina nyingine za vimelea, ikiwa ni pamoja na bakteria wa kinyesi kama Escherichia coli.
“Duniani kote, kunaweza kuwa na aina tofauti za bakteria, pamoja na fangasi na vimelea vingine,” alisema Pitt.

Bakteria kutoka nje wanaweza kuishi ndani ya nyumba zetu?
Tafiti zimeonesha kwamba viatu vinaweza kuhamisha bakteria kwa haraka kutoka mazingira ya nje na kuziingiza ndani ya nyumba.
Pitt anasema: “Kuna ushahidi mzuri kwamba vijidudu vinaweza kuendelea kuishi ndani ya nyumba na vinaweza kusambaa na kusababisha maambukizi kwa wanafamilia wengine.”
Anaongeza kuwa vijidudu hivi vinaweza kubaki hai kwa siku kadhaa, au hata muda mrefu zaidi kwenye mazulia yenye joto na unyevunyevu.
Alieleza: “Ukipiga magoti au mtoto akitambaa juu ya zulia… unapobonyeza zulia, unaweza kuwa unawaamsha tena bakteria hao.”
Hali hii inaleta hatari kubwa zaidi kwa watu wenye kinga dhaifu ya mwili kama vile watoto wachanga au wazee kuliko kwa watu wazima wenye afya nzuri.
Ingawa Pitt anakiri kwamba kukutana na vijidudu kunaweza kusaidia kujenga kinga ya mwili, anaamini kuwa maisha yetu ya kila siku tayari yanatupa mawasiliano ya kutosha na aina nyingi za bakteria.
Viatu viwe nje au ndani ya nyumba?
Beth anaamini jibu la swali letu linaonekana wazi kupitia maabara
Anasema: “Kuvaa viatu ndani ya nyumba ni kitu kinachochukiza, lakini pia kunaweka afya katika hatari ya kweli.”
Anaongeza: “Popote ulipo duniani, unapaswa kuvua viatu mara tu unapoingia ndani ya nyumba.”
Ikiwa kweli mtu anataka kuendelea kuvaa viatu ndani, kutumia mikeka ya mlangoni (doormats) na kutokuwa na mazulia kunaweza kusaidia kupunguza kiasi cha bakteria, alisema.
Alibainisha kwamba: “Kwa hali bora, nyumba inapaswa kusafishwa kwa kina angalau mara moja kwa wiki, na hii huenda inatosha kudhibiti bakteria, vumbi na uchafu.”
Sasa baada ya kuoa, Sophia na Bidya wamefikia maelewano.
Sophia anasema: “Ndani kabisa, ningependelea kila wakati kuvaa viatu… lakini najua kwamba ninapokwenda Serbia, lazima nivae ndala.”
Wakiwa nyumbani kwao Marekani, yeye huvaa “viatu vya ndani” ambavyo havitumiki nje ya nyumba. Anaongeza: “Napenda hisia ya uzito wa viatu miguuni mwangu, hivyo ndivyo nilivyolelewa.”
Kuhusu Bidya, naye amechukua baadhi ya tabia za Sophia.
Anasema: “Kuna nyakati naingia ndani nikiwa nimevaa viatu kwa haraka.”
Sophia anahitimisha: “Sijaribu kuwa Mserbia kabisa au kumfanya Bidya awe Mmarekani kabisa… Tunahifadhi utambulisho wetu, na tunajaribu kuchanganya tamaduni zote mbili.”