
Dar es Salaam. Muharram ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu iitwayo Hijra, na wa nne miongoni mwa miezi mitukufu katika Uislamu.
Mwezi huu unatukumbusha tukio kubwa katika historia ya Uislamu, nalo ni tukio la Hijra, (kuhama kwa Mtume wa Allah kutoka Makka kwenda Madina), tukio lililotenganisha baina ya haki na batili
Kabla hatujaendelea kueleza umuhimu wa Hijra kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu, tunapenda kukumbusha baadhi ya hekima kubwa za Allah katika kufuatana kwa miezi na miaka, na kupishana kwa usiku na mchana. Hakika Allah Mtukufu, ameufanya usiku na mchana kuwa hazina za matendo mema au mabaya na hatua za kupita kwa umri mpaka muda wao wa kuishi unapomalizika.
Allah amejaalia alama ya mchana ni jua lenye mwangaza ili watu watafute kipato cha kujikimu kimaisha, na alama ya usiku ni mwezi ili wapumzike ndani yake. Kwa sababu hiyo, Allah ameuita usingizi wa usiku kuwa ni kufa, na kuamka mchana kuwa ni kufufuliwa:
“Naye ndiye anaye kufisheni usiku, na anakijua mlichofanya mchana. Kisha Yeye hukufufueni humo mchana ili muda uliowekwa utimizwe. Kisha kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, na tena akwambieni mliyokuwa mkiyafanya.” [6: 60].
Allah Mtukufu ameufanya mwaka wa Kiislamu kuwa na miezi 12: “Hakika idadi ya miezi mbele ya Allah ni miezi kumi na miwili katika Kitabu cha Allah tangu siku alipoumba mbingu na ardhi; miongoni mwake iko miezi minne mitukufu…”[9: 36].
Allah Mtukufu amejaalia Mfumo wa Kisharia katika Uislamu wa kuhesabu nyakati utegemee miezi ya mwandamo. Hii ni kwa sababu mwezi una alama inayoonekana na kueleweka na watu wote, wasomi na wasio wasomi.
Alama hiyo ni kuonekana kwa mwezi mwandamo upande wa magharibi baada ya jua kuzama. Hivyo basi, mwanzo wa siku katika sharia ya Kiislamu ni baada ya jua kuzama, si baada ya jua kupinduka katikati ya mbingu.
Maswahaba wa Mtume (Allah awaridhie wote), waliutambua umuhimu wa Hijra ya Mtume wa Allah, hivyo tukio hili adhimu wakalifanya kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Hawakuzingatia mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwa matukio mingine makubwa kama vile kuzaliwa kwake Mtume, kupewa Utume, vita vya Badr na ufunguzi wa mji wa Makka Matukio haya yote yalifaa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu.
Hata hivyo, kila tukio lilikuwa na maana ambayo ilikuwa ndogo ukilinganishwa na matokeo makubwa na mazuri yaliyoletwa na Hijra (kuhama) katika kuenea kwa wito wa Kiislamu
Kwa hiyo, tukio la Hijra (kuhama kwa Mtume kutoka Makka kwenda Medina) ndiyo tukio la uamuzi mkubwa katika historia ya Uislamu. Kila mafanikio yaliyopatikana baada yake yanahusishwa nayo na yanarejea katika tukio hilo.
Kwa sababu hiyo, Amiri (kiongozi) wa Waumini Umar ibn al-Khaṭṭab, (Allah amridhie), aliufanya mwezi wa Muharram (mfungo nne) kuwa mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu.
Khalifa Umar ibn al-Khaṭṭāb aliletewa hati iliyoandikwa kuhusu deni la mtu mmoja kwa mtu mwingine, ambalo muda wake wa kulipwa ulikuwa katika mwezi wa Shaban. Akauliza: “Ni mwezi upi wa Shaban? Ni wa mwaka huu, mwaka ujao au mwaka uliopita?” Kuanzia hapo, akawakusanya watu.
Hilo lilitokea katika mwaka wa 16 au wa 17 baada ya tukio la Hijra. Akashauriana nao kuhusu ni tukio gani litumike kuwa mwanzo wa kalenda. ‘Ali ibn Abu Ṭalib, (Allah amridhie), pamoja na wengine, wakashauri kwamba kalenda ianze tangu Hijra ya Mtume kutoka Makka kwenda Madina.
Hii ni kwa sababu tukio la Hijra lilikuwa linajulikana kwa watu wote, na lilikuwa wazi zaidi kuliko mingine.
Hivyo wakaufanya mwaka wa Hijra kuwa mwanzo wa kuhesabu miaka katika Uislamu. Hii ni kwa sababu katika mwaka huo ndipo ilipoanzishwa dola huru ya Waislamu, na ndipo ilipoundwa nchi ya kwanza ya Kiislamu iliyokuwa chini ya utawala wa Waislamu.
Kisha Maswahaba waliokusanywa na ‘Umar walishauriana kuhusu ni mwezi gani uwe mwanzo wa mwaka. Baadhi yao wakasema: “Tuanze na mwezi wa Rabi‘ al-Awwal (mfungosita), kwa sababu ni mwezi ambao Mtume wa Allah aliwasili Madina akiwa amehama.”
Wengine wakasema: “Tuanze na mwezi wa Ramaḍhn, kwa sababu ni mwezi ambao Qur’ani iliteremshwa.”Lakini maoni ya Umar, ‘Uthman na Ali (Allah awaridhie), yaliungana katika kuupa uzito mwezi wa Muharram (Mfungonne) kuwa mwanzo wa mwaka.
Hii ni kwa sababu Muharram ni mwezi mtukufu na unafuata mwezi wa Dhul-Hijjah (mfungotatu), ambao ndani yake watu hutekeleza Hijja, ibada inayokamilisha nguzo za Uislamu, kwa sababu
Hija ndiyo nguzo ya mwisho kufaradhishwa miongoni mwa nguzo tano. Pia, Muharram unafuata mwezi ambao Mtume wa Allah alipokea kiapo cha utii kutoka kwa Anṣar (wakazi wa mji wa Madina) kuhusu Hijra. Kiapo hicho kilikuwa miongoni mwa maandalizi ya Hijra.
Itaendelea katika tolelo lijalo In shaa Allah. 0712 69081