
Akiwa amezaliwa katika familia iliyokimbia mzozo nchini Sierra Leone na kujenga maisha mapya nchini Ujerumani, Rüdiger anasema mafanikio yake yametokana na fursa ambazo wazazi wake walipata baada ya kupata usalama.
Sasa akiwa anaiwakilisha Ujerumani katika Kombe la Dunia la FIFA 2026 na pia mwanachama wa Timu ya Gamechanging ya UNHCR, Rüdiger amesema safari ya familia yake imeunda mtazamo wake wa maisha. “Safari ya wazazi wangu iliwapeleka kutoka Sierra Leone hadi Ujerumani ambako walipata usalama dhidi ya mzozo na nafasi ya kujenga maisha bora kwa familia yetu. Kwa kweli, bila hilo, nisingekuwa hapa leo,” anaeleza.
Rüdiger anasema mchezo huo ulimpa hisia ya kuwa sehemu ya jamii na kumpa matumaini alipokuwa mtoto. “Soka siku zote limekuwa zaidi ya mchezo kwangu. Nilipokuwa mtoto, lilikuwa mahali nilipopata nafasi yangu, mahali pa matumaini na ndoto,” ameeleza, akiongeza kuwa michezo inaweza kuwasaidia vijana kurejesha matumaini na kuota maisha bora ya baadaye.
Anarudisha kwa jamii ‘nyumbani’
Leo, Rüdiger anawasaidia vijana nchini Sierra Leone kupitia taasisi yake, kwa kusaidia upatikanaji wa elimu, michezo na huduma za afya. Amesema athari za vita bado zinaonekana nchini humo na kwamba anataka kusaidia kuunda fursa kwa kizazi kipya.
“Kila ninachofanya kinarejea kwa wazazi wangu, safari yao na nguvu ya mchezo kubadilisha maisha,” amesema Rüdiger, akisisitiza kuwa wakimbizi wanaweza kustawi na kutoa mchango mkubwa kwa jamii wanapopewa usalama, msaada na nafasi ya kufanikiwa.