
Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Kawe, Halima Mdee, amesema umadhubuti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa kesho utategemea busara na hekima za viongozi wa sasa.
Amesema katika taasisi mbalimbali: “Watu wanahitajiana na kwenye taasisi hizi hakuna malaika, lakini kuna watu wanaosimamia principle (misingi) kadhaa ili taasisi iweze kusonga mbele.”
“Umadhubuti wa Chadema wa kesho utategemea busara na hekima za viongozi wa sasa. Mafanikio yao yatapigiwa makofi, kufeli kwao watapigwa mawe. Kunahitajika busara na hekima kutibu madonda ya uchaguzi wa ndani.”
Mdee, ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), amesema hayo jana, Jumapili, Juni 21, 2026, katika mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa.
Msingi wa mahojiano hayo ni ujumbe wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, aliouweka kwenye akaunti yake ya Instagram akimkaribisha tena Mdee ndani ya chama hicho.
Juni 7, 2026, Lema, ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, aliweka ujumbe huo ukiambatana na picha ya Mdee.
Katika ujumbe huo, Lema alitumia methali ya Kijapani inayoeleza: “Umeanguka mara saba, simama mara nane. Rudi nyumbani, mpenzi, ni wakati wa kuinuka tena.”
Ujumbe huo uliibua mijadala mitandaoni na kwa wachangiaji kadhaa. Damian Wise alisema: “Halima is the best politician, mwanamke ana msimamo wa kiume.” Roma Michael aliandika: “Aje ase, jeshi sana huyu mama.”
Pia, kuna maoni ya wengine wakitaka wote waliokisaliti chama kwa namna moja au nyingine wasipokelewe tena.
Mdee alikuwa miongoni mwa wanachama 19, wakiwemo waliokuwa viongozi wa Bawacha, ambao Novemba 27, 2020, kikao cha Kamati Kuu kiliwatuhumu kwa usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni kuapishwa Novemba 24, 2020 na aliyekuwa Spika wa wakati huo, Job Ndugai (marehemu).
Mdee na wenzake 18 walikata rufaa Baraza Kuu, ambapo Mei 11, 2022, lilibariki kufukuzwa kwao. Hata hivyo, suala hilo lilifika mahakamani na baada ya kesi kusikilizwa, Mahakama ilitengua uamuzi huo wa Baraza Kuu wa kuwafukuza.
Alichokisema Mdee
Katika mahojiano hayo, Mwananchi lilitaka kujua aliupokeaje ujumbe huo wa Lema wa kumkaribisha tena Chadema, ambapo alianza kwa kumpongeza akisema busara anayoitumia Lema isiwe kwa Halima pekee, bali kwa chama chote.
“Inahitaji picha ambayo Lema anayo kichwani, basi iwe kwa uongozi wa chama kuanzia viongozi wa juu.
“Lema anaweza kuwa na matamanio yake, lakini iwe zaidi yangu, Halima. Hasa ukizingatia mpasuko wa chama ulivyokuwa baada ya uchaguzi wa ndani, ni lazima waungane,” amesema Mdee na kuongeza;
“Walikuwa kwenye kampeni, kuna ambavyo walisemeana vya kweli na vya uongo ili watu wapate dhamana. Ni wakati ego zipungue.”
Mdee amesema nafasi ya kuunganisha chama si ya wengine bali ya viongozi wenye dhamana.
“Mwenyekiti (Tundu Lissu) wa chama yuko ndani, hana uhuru wa kufanya mambo, lakini wasaidizi wake wanaweza kumsaidia.”
Lissu yupo gerezani kwa mwaka sasa, akikabiliwa na kesi ya uhaini ambayo ipo mahakamani. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, kwa sasa Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche, ndiye anayekaimu nafasi ya mwenyekiti. Makamu Mwenyekiti Zanzibar ni Said Issa Mohamed.
Katibu Mkuu ni John Mnyika, huku Manaibu Katibu Mkuu wakiwa Aman Golugwa (Bara) na Ali Ibrahim Juma (Zanzibar).
“Unapokuwa kiongozi unatakiwa kuwa na kifua, ngozi ngumu na busara,” amesema Mdee alipokuwa akijenga hoja za viongozi kuongozwa na mambo hayo wanapofanya uamuzi wa jambo lolote ili kuifanya taasisi kuwa imara.
Mpasuko ambao Mdee anauzungumzia ni ule wa uchaguzi wa ndani uliofanyika Januari 21, 2025, ulioshuhudia mchuano mkali kati ya aliyekuwa mwenyekiti kwa miaka zaidi ya 20, Freeman Mbowe, na Makamu wake, Tundu Lissu, katika nafasi ya uenyekiti.
Lissu aliibuka mshindi kwa kura 513, sawa na asilimia 51.5, huku Mbowe akipata kura 482, sawa na asilimia 48.4. Charles Odero alipata kura moja. Tofauti ya kura za Lissu na Mbowe ilikuwa 31.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, kumekuwa na mpasuko wa makundi ya timu za Mbowe na Lissu, huku wito wa kuvunjwa kwa makundi hayo ukiendelea kutolewa ndani na nje ya chama, hususan kwa viongozi waliopo madarakani kutafuta mwafaka wa pamoja.
Katika mahojiano yake, Mdee amesema watu wanaokuwa nje ya taasisi wanaona mambo mengi zaidi kuliko walioko ndani, hivyo ni jambo muhimu kuhakikisha viongozi wanatumia mbinu mbalimbali kutafakari na kuyafanyia kazi mambo hayo.
“Siasa za upinzani si kazi rahisi. Ni muhimu sana, sana, sana kuliko kitu chochote kuungana kuliko kutumia maneno ya kebehi, dharau na kiburi, hasa ukiwa umepewa jukumu la kusimamia taasisi,” amesema.
Mdee amesema taasisi ikifeli watu watakunyooshea kidole, na taasisi ikifanikiwa utapigiwa makofi hata kama wasaidizi wako wanafanya yote.
“Ujenzi wa taasisi ni pamoja na kuangalia wapi tulikosea. Unaweza kuwa unazungumza mambo kwenye umma, lakini ndani ya moyo wako unajua ukweli ni upi, na unapokuwa umejifungia mwenyewe unaweza kusema, ‘Pale nilikosea, nilivuka mipaka,’” amesema.
Katika kusisitiza hilo, Mdee amesema: “Katika taasisi watu wanahitajiana, na kwenye taasisi hizi hakuna malaika, lakini kuna watu wanaosimamia principle (misingi) kadhaa ili taasisi isonge mbele.”
“Kwangu namwona Lema amefungua ukurasa ambao viongozi wenzake wanapaswa kuuangalia kwa picha kubwa na pana kwa sababu ya kuchunga kauli wanazozizungumza. Unaweza kuwa unazungumza kwa lengo na nia fulani kwa sababu una nguvu kubwa, kumbe unazidi kutengeneza mpasuko,” amesema.
Anarudi lini Chadema?
Alipoulizwa ameondoka kwenye siasa na lini atarejea, Mdee amesema hajawahi kuondoka kwenye siasa kwa sababu mwanasiasa anahitaji jukwaa la kufanya siasa.
“Na mimi nimesema hakuna chama kingine ninachokifahamu zaidi ya Chadema, na kwa sababu milango ya kufanya siasa imefungwa na haijafunguka vizuri, kuna mambo mengine ya kufanya. Si kwamba ningeshindwa kwenda chama chochote cha siasa na kupata jukwaa.
“Nimeshirikiana na vyama vingine, na kwangu amani ya moyo ni kitu cha pekee. Milango ya kufunguliwa haijatosha. Nafanya jambo jingine la kilimo ambalo nalo nalipenda,” amesema.
Amesema anafanya kilimo kwa ubora na siku za usoni watu watakwenda kujifunza mafanikio ya kilimo hicho, ambacho anakipenda kama ilivyo kwenye siasa.