
Dar es Salaam. Kuongezeka kwa uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele kutoka kwenye matamasha na maeneo ya burudani katika baadhi ya maeneo ya wilaya za mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Morogoro, kunachochea hofu kuhusu usalama wa afya ya umma, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.
Kutokana na hali hiyo, maelfu ya wakazi wanakabiliwa na ukosefu wa usingizi, msongo wa mawazo wa muda mrefu, ongezeko la shinikizo la damu na hatari ya kupoteza uwezo wa kusikia wa kudumu.
Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na Mwananchi katika wilaya za Kinondoni, Ilala, Temeke na Ubungo mkoani Dar es Salaam, Manispaa ya Morogoro na jijini Arusha, changamoto hizo zimekuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, hali ikiwa mbaya zaidi mwishoni mwa juma na nyakati za usiku.
Wanasema kelele zinazoendelea zimevuruga maisha ya familia, zimeathiri ujifunzaji wa watoto, zimepunguza ufanisi kazini na kusababisha migogoro majumbani, hali inayoonesha jamii zikiwa katikati ya hitaji la burudani na haki ya kuishi katika mazingira tulivu na yenye afya.
Sheria, kanuni zakiukwa
Hali ikiwa hivyo, Mwongozo wa Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira Utokanao na Kelele na Mitetemo wa mwaka 2021 unaeleza wazi kuwa, uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na kelele na mitetemo ni miongoni mwa changamoto zinazotishia afya ya umma.
Licha ya kuwapo masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Viwango vya Kudhibiti Uchafuzi wa Kelele na Mitewtemo) za mwaka 2015, kelele zilizopitiliza kutoka kwenye matamasha, maonyesho ya wazi na maeneo ya burudani za usiku bado zinaendelea, huku ufuatiliaji wa mara kwa mara ukiwa mdogo.
Kuongezeka kwa kero ya kelele pia kunaashiria ukiukwaji wa Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kinachomhakikishia kila mwananchi haki ya kisheria ya kuwa na mazingira safi, salama na ya kiafya.
Licha ya marekebisho yaliyofanywa katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira mwaka 2025, hususani Kifungu cha 36A kinachowapa maofisa mazingira wa halmashauri mamlaka ya kukagua na kupima kelele, kutoza faini kwa wanaokiuka sheria, kusimamisha shughuli zinazosababisha uchafuzi na ukiukwaji wa sheria bado unaendelea.
Miongoni mwa maeneo yanayohusika na kadhia hiyo ni Sinza, Ukonga na Kawe mkoani Dar es Salaam, Msamvu (Morogoro) na katikati ya Jiji la Arusha, hali inayoonesha kuwapo kwa upungufu katika utekelezaji wa sheria.
Vilevile, Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) ya mwaka 1982 inazipa halmashauri mamlaka ya kutunga sheria ndogo za kudhibiti muda wa kufunga baa na viwango vya kelele katika maeneo ya makazi.
Malalamiko ya wananchi
Kwa Mariam Juma, mkazi wa Msamvu mkoani Morogoro, usingizi umekuwa anasa.
Anasema kila mwisho wa wiki hulazimika kuvumilia muziki mkali kutoka kwenye baa zilizo jirani na makazi yake.
“Unalala kwa vipande vipande. Asubuhi unaamka umechoka, kichwa kinauma na huwezi kufanya kazi vizuri,” anasema huku Rehema Ally akieleza kuwa, “wakati mwingine watoto wanaamka usiku wakilia kwa kelele. Hii imekuwa kawaida sasa.”
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Kened Msuya anasema: “Kuanzia jioni hadi alfajiri muziki unapigwa, hatupati kabisa usingizi.”
“Hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya malalamiko,” anasema Swed Said, huku Joyce Haule mkazi wa jijini Arusha akiunga mkono hoja hiyo akieleza kuwa: “Tumeripoti mara kadhaa lakini hakuna mabadiliko.”
Salma Mushi, mkazi wa Kijenge, jijini Arusha anasema: “Hata watoto hawapati muda wa kupumzika. Ni kelele kila wiki.”
Hoja hiyo inaungwa mkono na Abdalla Mahenya akisema muziki unapigwa usiku kucha, hivyo hawapati usingizi.
Yanayojiri Morogoro na Arusha pia yamelalamikiwa na mkazi wa eneo la Sinza Palestina, Jumanne Ramadhani (38), mfanyabiashara anayeishi karibu na eneo linaloandaa mara kwa mara matamasha ya muziki.
“Tunatoa taarifa kuhusu kelele, lakini zinaendelea hadi usiku wa manane. Baadhi ya matamasha huanza jioni na kuendelea hadi alfajiri. Kiwango cha sauti ni kikubwa kiasi kwamba haiwezekani kufanya mazungumzo ukiwa nyumbani. Unalazimika kutoka nje ndipo uweze kuzungumza kawaida,” anasema.
Kutoka Mbagala Zakhem, Dar es Salaam, Mariam Juma (40), mwalimu wa shule ya msingi na mama wa watoto watatu, anasema kukosa usingizi mara kwa mara kunaathiri afya yake na ufanisi wake kazini.
“Mapigo ya moyo wangu huongezeka na kichwa huuma. Kuna baadhi ya usiku silali kabisa. Unaamka umechoka na mwenye hasira. Kufundisha huwa vigumu unapokuwa hukupata usingizi,” anasema akiongeza kuwa uchovu humfanya ashindwe kuzingatia kazi.
Kwa Kassim Shukuru (33), fundi magari anayeishi Sinza Mori, anasema mwishoni mwa wiki ndiyo kipindi kigumu zaidi kwa familia yake.
“Kunapokuwa na tamasha karibu au msanii mpya anatumbuiza kwenye klabu, hakuna anayelala. Watoto huamka wakilia na ifikapo asubuhi kila mtu huwa amechoka,” anasema akieleza uchovu huo mara nyingi huathiri ufanisi wake kazini siku inayofuata.
Hatari za kiafya
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu anapokaa kwa muda mrefu kwenye mazingira yenye kiwango cha sauti kinachozidi desibeli 85 huongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya kupoteza uwezo wa kusikia.
Mashirika ya kimataifa ya wataalamu wa magonjwa ya moyo pia yameonya kuhusu athari za kiafya zinazotokana na kelele za mazingira. Chama cha Madaktari wa Moyo cha Ulaya, Chuo cha Madaktari wa Moyo cha Marekani, Chama cha Moyo cha Marekani na Shirikisho la Moyo Duniani hivi karibuni vilitoa tamko la pamoja likitaka kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya vichochezi vya msongo wa mazingira, ikiwamo uchafuzi wa kelele, kama sehemu ya juhudi pana za kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo duniani.
Hali hiyo inaonesha hatari zinazotokana na kelele nyingi zinazidi usumbufu wa kawaida na zinaweza kusababisha madhara ya kiafya ya muda mrefu. Wataalamu wa afya waliohojiwa wanasema kiwango cha sauti katika matukio ya burudani za moja kwa moja mara nyingi huzidi kiwango hicho na kufikia desibeli 100 hadi 110, kiwango kinachoweza kusababisha upotevu wa kudumu wa uwezo wa kusikia hata baada ya muda mfupi wa kuathirika.
“Sheria za kudhibiti kelele zisipotekelezwa, madhara yake ni ya kibiolojia na hujikusanya kadiri muda unavyopita,” anasema Dk Khuzema Rangwala, daktari bingwa wa masikio, pua na koo (ENT) katika Hospitali ya Saifee, Dar es Salaam.
Dk Rangwala anasema kuathiriwa mara kwa mara na kiwango hicho cha sauti kunaweza kusababisha uharibifu usiotibika wa sikio la ndani.
“Seli za nywele zilizopo ndani ya koklea zinazopitisha mawimbi ya sauti huharibika na zikishaharibika haziwezi kurejea katika hali yake ya awali,” anasema.
Anaeleza kuwa dalili za awali ni pamoja na kushindwa kuelewa vizuri mazungumzo katika mazingira yenye kelele, kuongeza kiwango cha sauti unapokuwa unasikiliza na mlio wa kudumu masikioni unaojulikana kama tinnitus.
“Tinnitus inaweza kuanza kama athari ya muda baada ya mtu kuathiriwa na kelele kubwa. Lakini mtu anapoendelea kuathirika mara kwa mara, hali hiyo huwa ya kudumu na huathiri usingizi, umakini na afya ya akili,” anasema.
Anaonya kuhusu upotevu wa uwezo wa kusikia usioonekana kirahisi, hali ambayo miunganiko ya neva kati ya sikio na ubongo huanza kuharibika kabla vipimo vya kawaida vya usikivu havijaonesha tatizo.
Anasema kuathiriwa na kelele kwa muda mrefu huongeza homoni za msongo wa mawazo kama cortisol na adrenaline, hivyo kuongeza hatari ya shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, wasiwasi na sonona.
“Kukosa usingizi kwa muda mrefu hudhoofisha kinga ya mwili na huathiri uwezo wa kujifunza pamoja na udhibiti wa hisia, hasa kwa watoto,” anasema.
Daktari bingwa wa masikio, pua na koo wa Medinova Specialised Polyclinic, Dk Rizwan Rafeeque anasema kuathiriwa kwa muda mrefu na kelele nyingi, iwe kutoka kwenye matamasha, barabarani au mazingira ya mijini, hakuathiri usikivu pekee bali pia huuweka mwili katika hali ya msongo unaozidi athari za sikio.
“Watu wengi hudhani kelele ni usumbufu wa kawaida tu, lakini kitabibu ni kichocheo cha msongo wa mwili. Kuendelea kuathiriwa na sauti kubwa kunaweza kusababisha mwitikio wa msongo wa mwili, kuongeza shinikizo la damu na baada ya muda, kuchangia magonjwa makubwa zaidi yanayoathiri afya kwa jumla,” anasema.
Dk Rafeeque anasema dalili za awali kama kutoka usaha masikioni mara kwa mara, mlio wa masikioni, kupungua kwa uwezo wa kusikia au kuhisi usumbufu katika mazingira yenye kelele hazipaswi kupuuzwa, kwani zinaweza kuashiria tatizo la kiafya.
Anasema kuendelea kuishi kwenye mazingira yenye kelele kunaweza kusababisha msongo wa mawazo, wasiwasi na sonona.
“Athari hutegemea jinsi mtu anavyopokea na kutafsiri kelele. Baadhi ya watu huathirika zaidi kuliko wengine. Kelele zisizozoeleka zinaweza kuvuruga utulivu wa akili na kuingilia shughuli za kawaida za kila siku,” anasema.
Hoja hizo za kitabibu zimetolewa pia na daktari bingwa wa masikio, pua na koo kutoka Arusha, Alex Macha akisema kelele za muda mrefu husababisha uharibifu wa seli za ndani ya sikio ambazo hazirejei tena, hali inayoweza kusababisha upotevu wa kudumu wa kusikia.
Dk Mwabaya Bakari kutoka Morogoro anasema: “Tunaona wagonjwa wengi wenye matatizo ya usingizi, presha na msongo wa mawazo yanayohusishwa na kelele.”
Waandaaji wa matukio
Baadhi ya waandaaji wa matukio wanakiri viwango vya sauti hupimwa mara chache wakati wa shughuli za burudani.
Mmoja wa waandaaji wa matukio mkoani Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema upungufu katika usimamizi, ushindani na gharama kubwa za vifaa hufanya uzingatiaji wa sheria kuwa mgumu.
“Hatuna vifaa vya kupima desibeli na mamlaka mara chache huja kufuatilia kiwango cha sauti wakati wa matukio. Sheria zipo, lakini hali halisi ilivyo ni tofauti,” anasema.
Anasema uwekezaji katika mifumo bora ya kuzuia sauti kutoka nje na mifumo ya kitaalamu ya kudhibiti sauti ni wa gharama kubwa.
“Maeneo mengi hayawezi kumudu vifaa vya kisasa vya kudhibiti sauti, hivyo waandaaji hutegemea mifumo ya kawaida,” anasema akieleza ushindani kati ya matukio mbalimbali pia huchangia ongezeko la kelele.
“Iwapo kuna matamasha mawili mwishoni mwa wiki moja, kila mmoja hujaribu kuzidi mwenzake kwa kuongeza sauti ili kuvutia watu,” anasema.
Mmiliki wa baa jijini Arusha (aliyeomba kutotajwa jina) anasema: “Wateja wanakuja kwa ajili ya muziki. Ukipunguza sana sauti, biashara inashuka.”
Anasema changamoto kubwa ni ukosefu wa vifaa vya kisasa vya kudhibiti sauti na gharama za uendeshaji.
Wapenzi wa muziki ‘live’
Neema Joseph (29), ofisa masoko anayehudhuria mara kwa mara matukio ya muziki wa moja kwa moja jijini Dar es Salaam, anasema uzoefu wa ndani ya tamasha ni tofauti na kusikia sauti ukiwa nje ya eneo la tukio.
“Ukiwa ndani, muziki mkubwa unaonekana wa kawaida kwa sababu hiyo ndiyo mazingira ambayo watu wamekuja kuyafurahia. Unahisi mdundo, ngoma na besi mwilini kote na hicho ndicho kinachoufanya muziki wa moja kwa moja uvutie,” anasema Neema.
Anasema matamasha mara nyingi huwa sehemu muhimu za kijamii zinazowawezesha watu kukutana na kupumzika baada ya wiki yenye shughuli nyingi.
“Kwa vijana wengi wa jijini, matamasha ni njia ya kupumzika, kukutana na marafiki na kusherehekea muziki pamoja. Yanajenga hisia ya umoja kwa sababu kila mtu anashiriki tukio lilelile,” anasema.
Hata hivyo, Neema anakiri waandaaji wanapaswa kuzingatia ustawi wa watu wanaoishi karibu na maeneo hayo. “Waliomo ndani ya tamasha wanafurahia muziki mkubwa, lakini waandaaji wanapaswa pia kuwazingatia majirani na kuhakikisha sauti haisambai kwa umbali mkubwa,” anasema.
Kelvin Msuya (32), yeye anasema: “Matamasha ya moja kwa moja yanapaswa kuwa na nguvu. Mfumo wa sauti unapokuwa imara na umati ukaitikia, hutengeneza uzoefu ambao ni vigumu kuuelezea,” anasema Neema.
“Mashabiki wengi hutegemea muziki uwe mkubwa kwa sababu ndiyo unaotengeneza msisimko. Msanii anapoimba wimbo maarufu na maelfu ya watu wakaimba pamoja naye, nguvu iliyopo ukumbini huwa ya kipekee.”
Kauli za wataalamu NEMC
Hamadi Taimuru, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria katika Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), anasema waandaaji wengi hukosea kudhani vibali vya burudani vinavyotolewa na mamlaka nyingine vinawaruhusu kuvuka viwango vya kelele vinavyoruhusiwa.
Anasema NEMC inaweka mkazo mkubwa kwenye elimu kwa umma na kampeni za uhamasishaji ili kuongeza uelewa kuhusu kanuni za kelele na athari zake kwa afya.
“Tunafanya kampeni za uhamasishaji katika jamii mbalimbali ili waandaaji na wananchi waelewe hatari za kelele zilizopitiliza na viwango vilivyowekwa na sheria,” anasema.
Anaeleza kuwa lengo ni kuwafikia watu wengi iwezekanavyo na kuhamasisha uzingatiaji wa sheria kwa hiari kabla ya hatua za utekelezaji kuchukuliwa.
Kwa mujibu wa Taimuru, Mwongozo wa Kudhibiti Kelele wa mwaka 2021 unasisitiza ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali zikiwamo NEMC, halmashauri za manispaa, Jeshi la Polisi Tanzania, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) katika kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele.
Kwa upande mwingine, Basata inasema vibali vya maonyesho hutolewa baada ya kufanya majadiliano na waandaaji kuhusu eneo la tukio, aina ya tukio na muda unaotarajiwa wa kufanyika.
“Msanii au mwandaaji anapoomba kibali, kwanza tunathibitisha tukio litafanyika wapi, ni la aina gani na muziki utapigwa kwa muda gani,” anasema mmoja wa maofisa kutoka Basata.
Anasema wataalamu wa kiufundi wa baraza kuna wakati hukagua maeneo ya matukio ili kutathmini namna mifumo ya sauti ilivyofungwa na kupunguza uwezekano wa kusababisha usumbufu wa kelele.
“Ndiyo maana katika tamasha na maonyesho mengi, spika huwekwa juu. Uwekaji sahihi husaidia kudhibiti umbali ambao sauti husafiri na kupunguza usumbufu kwa jamii zinazozunguka eneo hilo,” anasema.
Kwa mujibu wa Basata, hufanya ufuatiliaji kwa kushirikiana na NEMC pamoja na mamlaka za Serikali za mitaa ili kuhakikisha waandaaji wanazingatia masharti ya vibali.
Usikose kufuatilia kesho tukiangazia mamlaka zenye jukumu la kudhibiti uchafuzi wa mazingira zinavyoshindwa kutekeleza wajibu wake wa kudhibiti kikamilifu.