
NI leo fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa wasichana chini ya umri wa miaka 17, itakayowakutanisha Tanzania dhidi ya Uganda saa 10:30 jioni Uwanja wa KMC Complex Mwenge Dar es Salaam.
Fainali hiyo itanguliwa na mechi ya mshindi wa tatu kati ya Sudan Kusini dhidi ya Kenya itakayopigwa Uwanjani hapo saa 7 mchana.
Serengeti Girls ilifuzu fainali baada ya kuichapa Sudan Kusini 4-0 katika nusu fainali, huku Uganda ikii-tandika Kenya mabao 3-0.
Tanzania imeingia hatua hiyo ikiwa na rekodi nzuri baada ya kumaliza Kundi A kileleni na pointi saba, ikifunga mabao 15 na kuruhusu moja. Kikosi hicho kimeonyesha ushindani mkubwa hasa kwenye safu ya ushambuliaji na uimara wa safu ya ulinzi, hali inayokifanya kuwa miongoni mwa timu zinazotajwa kuwania taji hilo.
Kwa upande wa Uganda safari yao kwenye michuano hiyo imekuwa ya kuvutia baada ya kufanya vizuri makundi hadi kufika hatua hiyo.
Kwenye hatua ya makundi pekee timu hiyo imefunga mabao 20 ikiwa na wastani wa kufunga mabao matano kwa kila mechi na haijaruhusu bao hadi kufika fainali.
Kocha wa Uganda, Sheryl Botes alisema “Tunafurahi kufika fainali, lakini lengo letu ni kutwaa ubingwa wa mashindano haya. Tunapaswa kuwa makini na kubaki kwenye lengo letu ingawa tunafahamu ugumu wa mechi tutakayokutana nao.”
Kocha wa Tanzania, Ester Chabruma alisema “Tumekuwa na maandalizi mazuri kilichobaki ni dakika 90 ambazo hazitakuwa rahisi kutokana na ubora wa mpinzani wetu.