Chanzo cha picha, shutterstock.com
Katika kijiji cha Likuyu, Tanzania, mapema asubuhi ya kawaida, kijana mmoja hutazama magari ya wageni yakipita kuelekea msituni. Hayasemi sana.
Lakini kwa Hassan Salehe Mabukisela, kila gurudumu linalozunguka kuelekea eneo la Mkuju River hubeba swali moja kubwa: je, maisha yake yatabadilika kweli?
Kwenye kijiji hicho, kilichoko Nyanda za Juu za Kusini, Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Hassan anaiona urani kwa namna tofauti na wataalamu wa nishati au wawekezaji wa kimataifa.
Kwa kijana huyo mwenye miaka 28 na mhitimu wa chuo kikuu, urani si mjadala wa siasa za dunia, nishati ya nyuklia au mabadiliko ya tabianchi.
Ni suala la maisha.
“Fursa hii itabadilisha maisha yangu na familia yangu. Kwa ujuzi ninaoupata sasa, ninaweza kupata kipato na kusaidia familia yangu,” anasema.
Baada ya muda wa kufanya kazi ndogo ndogo kijijini, Hassan ni miongoni mwa vijana 10 waliopata mafunzo ya kuendesha mitambo na teknolojia za kisasa zitakazotumika katika mradi wa Urani wa Mkuju River.
Sio Hassan pekee anayesubiri mabadiliko.
Katika kijiji jirani, mwanamke mmoja tayari ameanza kupanga namna ya kunufaika na mabadiliko ya kiuchumi yanayotarajiwa kuletwa na mradi huo.
“Nimeanza kuandaa mazingira ya kupika kama mama lishe. Nikikosa nafasi ya kuingia mgodini, nitauza chakula,” anasema.
Kauli hizi mbili zinaweka wazi namna wananchi wa Namtumbo wanavyouangalia mradi huo. Kwao, urani si madini tu. Ni matarajio ya ajira, biashara na maisha bora. Lakini matarajio hayo yana msingi gani?
Kutoka msituni Namtumbo hadi soko la dunia
Chanzo cha picha, Daily News
Takribani kilomita 180 kaskazini mashariki mwa mji wa Songea, katikati ya misitu ya Mkoa wa Ruvuma, ndipo ulipo mradi wa Urani wa Mkuju River. Eneo hilo liko takribani kilomita 54 kutoka makazi ya karibu ya watu katika Kijiji cha Likuyu Sekamaganga, Wilaya ya Namtumbo.
Kwa miaka mingi, lilijulikana kwa ukimya wa misitu inayopakana na Hifadhi ya Selous. Leo, ukimya huo unakatizwa na sauti za magari ya wataalamu, mafundi na wakandarasi, huku jamii ikianza kujiandaa kwa kile kinachoonekana kuwa miongoni mwa miradi mikubwa zaidi ya kubadili uchumi wa kusini mwa Tanzania.
Julai 30, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kiwanda cha majaribio cha uchenjuaji wa urani katika eneo la Mkuju River, Namtumbo na akasema: “Ndani ya nchi yetu Mungu ametubariki uraniamu (urani). Ni vyema kusimamia ule mradi wetu kule Namtumbo, wale wawekezaji waanze kazi sasa tufaidike na rasilimali ile.”
Mradi huo, unaotekelezwa na Mantra Tanzania Limited kwa ushirikiano na Rosatom ya Urusi, unakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi trilioni tatu na kuvutia uwekezaji wa takribani dola bilioni 1.2 za Marekani.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, makampuni 13 ya Urusi yanafanya kazi nchini Tanzania kwa uwekezaji unaokadiriwa kufikia dola milioni 400, huku Mkuju ukiwa mradi mkubwa zaidi.
Serikali inaona mradi huo kama miongoni mwa miradi ya kimkakati yenye uwezo wa kubadili mwelekeo wa uchumi wa madini nchini.
Utekelezaji wake unatarajiwa kudumu kwa takribani miaka 20, huku awamu ya kwanza ya uzalishaji ikitarajiwa kuchukua miaka 12.
Mpaka sasa, vijana 10 tayari wamepata mafunzo ya kuendesha mitambo na teknolojia za kisasa zitakazotumika katika hatua za awali za mradi.
Serikali inatarajia pia kunufaika kupitia hisa zake za asilimia 20, kwa mapato yanayokadiriwa kufikia dola milioni 40 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu wa uchumi, mradi huu unaweza kuchangia zaidi ya asilimia moja ya Pato la Taifa (GDP) utakapofikia uzalishaji kamili.
Lakini mchango wake hauishii ndani ya Tanzania.
Meneja wa Mradi wa Mkuju River, Beria Vorster, anasema uzalishaji unaweza kuiweka Tanzania miongoni mwa nchi 10 wakubwa wa urani duniani, ukichangia takribani asilimia nne ya uzalishaji wa kimataifa.
Anasisitiza kuwa urani ya Tanzania haitalenga matumizi ya kijeshi, bali nishati safi duniani.
Somo la Namibia – mafanikio, maji na miundombinu
Chanzo cha picha, chamberofmines
Zaidi ya kilomita 3,000 kutoka Namtumbo, nchini Namibia, historia ya urani inatoa picha ya maendeleo na tahadhari kwa pamoja.
Urani iligunduliwa katika Jangwa la Namib mwaka 1928, lakini uzalishaji wa kibiashara ulianza mwaka 1976.
Leo, Namibia ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa urani duniani, ikichangia takribani asilimia 10 ya uzalishaji wa kimataifa.
Lakini mafanikio hayo hayakutokana na uchimbaji pekee.
Yaliambatana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, ikiwemo miradi ya maji kama Erongo Desalination Project, iliyojengwa kusaidia shughuli za migodi na jamii katika maeneo ya ukame.
Kwa Raphael Kugesha, mtaalamu wa maendeleo ya uchumi wa jamii, huu ni mfano wa kujifunza.
“Wananchi wanaanza kuelewa kwamba urani si suala la mabomu kama walivyofikiria awali. Wanaona ni chanzo cha nishati, wanajifunza teknolojia mpya na wanaanza kufikiria fursa za biashara zinazozunguka mradi,” anasema.
Hata hivyo anaonya:
“Matumaini ni makubwa, lakini yasipodhibitiwa yanaweza kuleta hali kama iliyowahi kujitokeza kwenye mjadala wa gesi Mtwara. Wananchi wanahitaji kuona matokeo yanayoonekana; ajira, maji, barabara na biashara.”
Kipimo halisi cha Mkuju
Chanzo cha picha, Mantra
Urani (au Uranium) ni kemikali au madini yenye metali nzito yenye mionzi, inayotumika kama chanzo cha nishati ya nyuklia duniani.
Kwa sasa, Mkuju bado iko kwenye hatua za mwanzo. Hakuna mabadiliko makubwa ya moja kwa moja ya kiuchumi yaliyotokea. Lakini mabadiliko ya awali yanaonekana.
Mafunzo yanaendelea. Biashara ndogo zinaanza kujiandaa. Na matarajio yanakua kwa kasi. Kwa upande wa Mantra Tanzania Limited, mafanikio ya mradi hayawezi kupimwa kwa uzalishaji pekee.
“Uchimbaji endelevu si kufuata sheria za mazingira pekee, bali ni kuhakikisha tunajenga thamani ya kudumu kwa jamii zinazotuzunguka,” anasema Meneja wa Uendelevu, Majani Moremi Wambura.
Kwa wananchi wa Likuyu na Namtumbo, kipimo ni cha moja kwa moja zaidi: maji, barabara, elimu, afya na fursa za biashara. Kwa Raphael Kugesha, hicho ndicho kitakachoamua hatima ya mradi.
“Madini haya hayapaswi kupimwa kwa kiasi kitakachochimbwa au mapato yatakayopatikana. Kipimo halisi ni kama mwananchi wa Likuyu ataona maisha yake yanabadilika kupitia huduma na fursa halisi,” anasema.
Na pengine, kipimo kikubwa zaidi cha Mkuju hakitakuwa kwenye ripoti za uzalishaji, kitakuwa kwenye sauti ya kijana kama Hassan na wengine, miaka michache ijayo, atakaposimama tena Likuyu na kusema kama ndoto yake iligeuka kuwa maisha halisi au ilibaki kuwa ahadi iliyopotea msituni.
Ndipo historia ya urani ya Tanzania itatimia. Itaandikwa kwa kile si kwa kile kilichochimbwa chini ya ardhi, bali kwa kile kilichobadilika juu ya ardhi. Na safari hiyo inajionyesha kuanza kwa mguu wa kulia.