Michel Aebischer wa Uswizi wakati wa mapumziko ya maji katika Kombe la Dunia la 2026

Chanzo cha picha, Reuters

Imekuwa taswira ya kawaida katika mechi za Kombe la Dunia.

Mwamuzi hupuliza filimbi dakika ya 22 katika kila kipindi ili kusimamisha mchezo na kuwapa wachezaji nafasi ya kunywa maji na kurejesha nguvu.

Mapumziko hayo ya lazima ya dakika tatu yameanzishwa katika mechi zote 104 za mashindano haya ili kuwasaidia wachezaji kukabiliana na joto kali na unyevunyevu mkubwa nchini Mexico, Canada na Marekani.

Hata hivyo, si kila mtu ameridhishwa na hatua hiyo.

Baadhi ya wadau wameeleza kuwa mapumziko hayo ni fursa ya kibiashara iliyowekwa kwa manufaa ya watangazaji wa televisheni wa Marekani.

Hata viwanja vyenye paa linalofunguka na mifumo ya kudhibiti halijoto vinaendelea kutumia mapumziko hayo.

Kocha wa Marekani, Mauricio Pochettino, amesema hafurahishwi na utaratibu huo isipokuwa katika mazingira yenye hali mbaya ya hewa.

“Sipendi. Ninaona yanafaa tu pale hali ya hewa inapokuwa kali sana. Lakini mazingira yanapokuwa mazuri, si lazima,” alisema.

Kwa hivyo, ni nani wanaonufaika na nani wasionufaika katika mapumziko ya maji ya Kombe la Dunia? Na mtindo huo umeathiri vipi michezo ya ufunguzi?

“Mapumziko ya maji? Mimi nayaita mapumziko ya kugeuza mwelekeo wa mchezo”

Carlo Ancelotti akitoa maelekezo kwa wachezaji wake wa Brazil wakati wa mapumziko ya maji

Chanzo cha picha, Reuters

Katika mechi kati ya Brazil na Morocco, Brazil ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 wakati wa mapumziko ya maji katika kipindi cha kwanza.

Dakika chache baada ya mchezo kuanza tena, Brazil ilisawazisha kupitia Vinicius Jr.

Kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti, alikiri kuwa mapumziko hayo yalimpa nafasi ya kutoa maelekezo mapya na kufanya marekebisho ya kiufundi yaliyoibadilisha timu yake.

“Unaweza kuwaeleza wachezaji tatizo lililopo na kufanya marekebisho ya kimkakati ambayo yanaweza kuleta tofauti kubwa,” alisema.

Kauli hiyo imezua mjadala kuhusu iwapo makocha wanapaswa kuruhusiwa kutumia mapumziko hayo kutoa maelekezo ya kiufundi ikiwa lengo kuu ni kulinda afya za wachezaji.

Kocha mkuu wa Morocco, Mohamed Ouahbi akizungumza na Neil El Aynaoui wakati wa mapumziko ya maji dhidi ya Brazil

Chanzo cha picha, Getty Images

Kocha wa timu ya wanawake ya Marekani, Emma Hayes, anaamini mapumziko hayo huathiri timu inayokuwa inatawala mchezo.

“Yanawanufaisha wale wanaopoteza mwelekeo wa mchezo. Ndiyo maana mimi nayaita mapumziko ya kubadili kasi ya mchezo,” alisema.

“Unapokuwa juu ya mpinzani hutaki mchezo usimame, lakini unapokuwa chini unafurahia mapumziko hayo.”

“Wakati mwingine hata si suala la kufundisha au kutoa maelekezo wakati wa mapumziko hayo. Ni kuhusu kuwapa wachezaji maji, kuwatuliza na kuwasaidia kurejesha utulivu. Wakati mwingine huenda usifanye chochote, lakini hata hilo linaweza kuhesabiwa kama sehemu ya ukocha,” alisema.

“Inasikitisha. Ninaweza kuelewa umuhimu wake katika maeneo yenye joto kali sana, lakini inaonekana huenda utaratibu huu ukawa sehemu ya kudumu ya mchezo.”

Kama ilivyokuwa kwa Brazil, Canada pia ilisawazisha muda mfupi baada ya mapumziko ya maji katika kipindi cha pili, wakati mchezaji wa akiba Cyle Larin alipofuta uongozi wa Bosnia Herzegovina Ijumaa.

Scotland nayo ilifunga bao pekee la ushindi dhidi ya Haiti muda mfupi baada ya mapumziko hayo, huku Australia ikipata bao lake la kwanza katika mazingira kama hayo kwenye ushindi wa mabao mawili kwa nunge dhidi ya Uturuki.

Mshambuliaji wa zamani wa Hispania, Juan Mata, aliyeshinda Kombe la Dunia mwaka 2010, amesema asingependezwa na mapumziko ya dakika tatu katika kila kipindi kama angekuwa bado anacheza.

“Kama mchezaji, sidhani kama ni jambo zuri,” aliiambia ITV Sport.

“Ukiwa nyuma kwa mabao unataka kufunga haraka, na ukiwa mbele unataka kuendelea kumiliki mpira. Nadhani mapumziko hayo yanakatiza kasi na mwelekeo wa mchezo.”

‘Njia nyingine ya kupeperusha matangazo ndani yake’

Mbali na mashabiki waliolipa gharama kubwa za tiketi wakitarajia kushuhudia soka la kuvutia na lisilokatizwa, baadhi ya timu pia zinaonekana kuathiriwa na mapumziko hayo.

Mataifa madogo yanaonekana kuwa miongoni mwa yaliyoathirika zaidi.

Curacao walikuwa wamesawazisha dhidi ya Ujerumani kabla ya mapumziko ya maji katika kipindi cha kwanza, lakini baada ya mchezo kurejea walipoteza mwelekeo na kufungwa mabao 7-1.

Jamhuri ya Czech nayo ilitawala dhidi ya Korea Kusini kabla ya mapumziko hayo, lakini ilipoteza kasi na hatimaye ikafungwa 2-1.

Kwa upande mwingine, Uholanzi ilikuwa mbele kwa mabao 2-1 dhidi ya Japan kabla ya mapumziko ya maji ya kipindi cha pili mjini Arlington, Texas. Hata hivyo, ilishindwa kulinda uongozi huo na mchezo ukaisha kwa sare ya 2-2.

Bila shaka, si kila mabadiliko ya matokeo yanaweza kuhusishwa moja kwa moja na mapumziko ya maji. Hata hivyo, kadiri mashindano yanavyoendelea, itakuwa rahisi kutathmini iwapo kusimamishwa kwa mchezo kunachangia kwa kiasi kikubwa kubadilika kwa mwenendo wa mechi.

Nani wanaonufaika?

Brazil ilisawazisha baada ya mapumziko ya maji dhidi ya Morocco.

Canada pia ilisawazisha muda mfupi baada ya mapumziko kama ilivyokuwa Scotland na Australia ambazo zilifunga mabao muhimu mara tu baada ya mchezo kurejea.

Mshindi wa Kombe la Dunia akiwa na Hispania mwaka 2010, Juan Mata, amesema asingefurahia mfumo huo akiwa mchezaji.

“Mapumziko hayo yanakatiza kasi ya mchezo. Ukiwa nyuma unataka kushambulia haraka, ukiwa mbele unataka kuendelea kutawala mpira,” alisema.

Afya ya wachezaji au biashara?

Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal na England, Ian Wright, ameonyesha wazi kutoridhishwa kwake na utaratibu huo.

“Nadhani ni njia nyingine tu ya kuingiza matangazo zaidi kwa mtazamo wa biashara wa Marekani,” alisema.

Katika mechi ya ufunguzi kati ya Mexico na Afrika Kusini, kituo cha televisheni cha Fox nchini Marekani kiliongeza muda wa matangazo yake wakati wa mapumziko ya maji.

“Wametumia hoja ya ustawi wa wachezaji, lakini binafsi sioni ndiyo sababu kuu,” aliongeza Wright.

Hata hivyo, wapo wanaounga mkono hatua hiyo. Kocha wa Hispania, Luis de la Fuente, amesema afya za wachezaji ndiyo kipaumbele kikuu.

“Ninaweka mbele ustawi wa wachezaji wangu. Nafikiri ni hatua sahihi kusimamisha mchezo kwa muda mfupi, kurejesha nguvu na kuendelea,” alisema kabla ya mechi dhidi ya Cape Verde Jumatatu.

Aliongeza kuwa hata kama halijoto ya uwanjani si ya juu sana, wachezaji wanahitaji muda wa kunywa maji, kupumzika kwa sekunde chache na kupokea maelekezo mafupi kabla ya mchezo kuendelea.

“Kesho, kuna baridi kali katika uwanja,” aliongeza De la Fuente siku ya Jumapili.

“Kwa wiki nzima, tumeona halijoto kubwa. Ni vigumu sana kukabili halijoto hizi kwa muda mrefu unapofanya kazi.

“Kwa maoni yangu, jambo bora ni kunywa maji mengi, pumzika, waache wapumue kwa sekunde chache.

“Haitakuwa joto hivyo [Jumatatu] lakini tunahitaji kuwaacha wapumue na kisha dakika moja au mbili kuwapa maelekezo kadhaa.”

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *