Katika mahojiano maalum na Leah Mushi pembezoni mwa mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Nassriya Nassir Ali amefunguka kuhusu safari yake ya uongozi, changamoto alizopitia kama mtu mwenye ulemavu wa kusikia, na ujumbe wake kwa jamii.

Akiwa anazungumza kupitia mkalimani wake wa lugha ya alama, Tusajigwa Ernest, Nassriya amesema safari yake ya uongozi ilianzia ngazi za chini kabisa za kijamii.

“Nimetokea kwenye Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu, na pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake na Watoto wenye Ulemavu SHIVYAWATA. Kabla ya kuwa mbunge, nilianza kujishughulisha na masuala ya kijamii na baadaye nikawa mjumbe wa serikali ya mtaa Kigamboni kwa takribani miaka minne.” 

UN News Mbunge Nassriya Nassir Ali kutoka Tanzania ambaye ana ulemavu wa kutosikia.

Amesema safari hiyo haikuwa rahisi. Baada ya kushiriki nafasi ya uongozi wa mtaa, alijaribu kugombea nafasi ya udiwani wa viti maalum lakini hakufanikiwa. Hata hivyo, hakuruhusu kushindwa huko kuzima ndoto yake.

“Nilipoona kura hazikutosha sikukata tamaa. Niliamua kuendelea kutafuta fursa nyingine. Leo namshukuru Mungu ndoto yangu imetimia na nimekuwa mbunge kamili.”

Mtazamo potofu

Nassriya anasema mojawapo ya changamoto kubwa aliyokutana nayo ilikuwa ni mtazamo hasi wa baadhi ya watu waliokuwa hawaamini kuwa mtu kiziwi anaweza kuongoza.

“Nilipitia unyanyasaji wa kimtazamo kwa sababu watu walikuwa wanaamini kiziwi hawezi kuwa kiongozi. Walijiuliza anawezaje kuzungumza au kuelewa mambo ya uongozi.”

Licha ya hali hiyo, aliamua kujitokeza na kugombea. Baada ya wananchi kumpa nafasi, aliweza kuvunja hofu na dhana zao kwa utendaji wake.

Kwa mujibu wake, mawasiliano kati yake na wananchi hayajawahi kuwa kikwazo kikubwa kama watu wengi wanavyodhani.

“Tunatumia mbinu za kibinadamu kuwasiliana. Hata kama si kila mtu anajua lugha ya alama, bado tunatafuta njia mbadala za kuelewana. Nilifanikiwa kuwahudumia wananchi wangu kwa miaka minne mfululizo, na mpaka leo bado wananihitaji.”

Akizungumza na vijana, hususan vijana wenye ulemavu, Nassriya amewataka kujenga hali ya kujiamini na kutambua haki zao.

“Unatakiwa kujua haki zako. Una haki ya kugombea, kuchaguliwa na kuchagua. Ukishafahamu hivyo, usibaki nyumbani. Nenda kachukue fomu, jitokeze.”

Picha ya UN/Mark Garten Ulemavu wa viungo sio ulemavu wa akili. Watu wenye ulemavu wa viungo wakiwa katika mkutano wa kimataifa mjini New York Marekani. (Maktaba)

Wenye ulemavu wasikae nyuma

Mbunge Nassriya ametoa rai kwa watu wenye ulemavu wasijione kuwa hawawezi kushika nafasi za juu za uongozi.

“Hakuna jambo litakalokushinda kama ukiamua kuipigania nafasi yako. Mimi kama ningebaki nikisema siwezi kwa sababu ni kiziwi, nisingefika hapa.”

Kwa wananchi wanaowadharau au kuwabeza watu wenye ulemavu, Nassriya ana ujumbe wa wazi. “Waondoe imani potofu kwamba mtu mwenye ulemavu hawezi. Mtu mwenye ulemavu anaweza kila kitu kama mtu mwingine yeyote. Mimi ni mbunge leo, na nina uwezo mkubwa wa kutekeleza wajibu wangu.”

Katika ujumbe wake wa mwisho, ametoa wito mzito kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuhakikisha hawawafichi watoto wao majumbani, bali wanawapeleka shule.

Msifiche watoto wenye ulemavu. Wapelekeni shule wapate elimu na waweze kujisimamia wenyewe. Elimu ndiyo msingi wa maisha yao ya baadaye.”

Ametumia pia nafasi hiyo kumshukuru mama yake kwa mchango mkubwa alioutoa katika maisha yake.

“Namshukuru sana mama yangu kwa kuniamini na kupambana kuhakikisha napata elimu. Kwangu, mama amecheza nafasi kubwa sana kufika hapa nilipo.”

Kwa Nassriya, simulizi yake ni ushahidi kuwa ulemavu si mwisho wa ndoto, bali changamoto inayoweza kushindwa kwa kujiamini, elimu na msaada wa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *