Tarime. Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mjini mkoani Mara imeanzisha mfumo maalumu wa kufuatilia wanafunzi watoro na wanaoacha masomo kabla ya kuhitimu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wanafunzi wote wanaoandikishwa katika shule za umma za msingi na sekondari wanamaliza masomo yao kwa wakati.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia hoja iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika ukaguzi wa hesabu za halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Akiwasilisha taarifa katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Tarime Mjini kilichofanyika leo Juni 23, 2026, Kaimu Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Helga Mosi amesema mfumo huo umeanza kuonyesha mafanikio kwa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaotoroka au kuacha shule kabla ya kuhitimu.

Amesema kwa shule za sekondari za umma, kiwango cha wanafunzi wanaoacha shule kimepungua kutoka asilimia 28 mwaka 2021 hadi asilimia 17 mwaka 2025.

“Kwa shule za msingi pia kiwango hicho kimepungua kutoka asilimia 25 mwaka 2021 hadi asilimia 22 mwaka 2025. Jitihada bado zinaendelea kuhakikisha changamoto hii inatokomezwa na kila mwanafunzi anayesajiliwa anahitimu masomo yake kwa mujibu wa kalenda ya elimu,” amesema Mosi.

Amefafanua kuwa mfumo huo unasaidia kubaini mapema wanafunzi watoro na wanaoacha shule, hivyo kuwezesha mamlaka husika kuchukua hatua za haraka ikiwemo kuwatafuta na kuwarejesha shuleni.

Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya mji wa Tarime wakati wa kujadili taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha 2024/25. Picha na Beldina Nyakeke.

Kuhusu ufaulu katika shule za sekondari za umma, Mosi amesema taarifa ya CAG iliibua hoja ya ufaulu hafifu ukilinganishwa na shule binafsi, jambo lililosababisha halmashauri kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha matokeo ya wanafunzi.

Hatua hizo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuongeza vifaa vya kufundishia, kuanzisha programu za chakula shuleni, kuajiri walimu wa sayansi na kuimarisha masomo ya ziada kwa wanafunzi wenye uwezo mdogo darasani.

“Hatua hizi zimechangia kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 82 mwaka 2024 hadi asilimia 86 mwaka 2025,” amesema.

Aidha, amesema halmashauri imeajiri walimu 45 wa masomo ya sayansi kwa shule za sekondari na walimu 30 kwa shule za msingi ili kuimarisha ufundishaji wa masomo hayo ambayo yamekuwa yakifanya chini ya matarajio.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, amesema taarifa ya CAG imeonyesha kuwepo kwa hoja tatu za ukaguzi zilizojirudia, hali inayoashiria udhaifu katika mifumo ya ndani ya usimamizi na udhibiti.

“Taarifa ya CAG ina jumla ya hoja 56 za miaka ya nyuma. Kati ya hizo, hoja 33 zimefungwa, 20 zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, lakini hoja tatu zimerudiwa. Kurudiwa kwa hoja za ukaguzi ni kiashiria cha udhaifu wa mifumo ya ndani ya usimamizi, jambo ambalo si zuri,” amesema Kanali Mtambi.

Amesema Baraza la Madiwani linapaswa kuisimamia kikamilifu menejimenti ya halmashauri katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan miradi ya maendeleo, ili kuhakikisha halmashauri inaendelea kupata hati safi za ukaguzi.

Pia, ameitaka halmashauri kuweka mikakati madhubuti ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika taasisi za umma na kwa wananchi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Kanali Mtambi, mikakati hiyo inapaswa kujumuisha utafutaji wa rasilimali na ushirikiano na wadau mbalimbali ili kufanikisha azma ya Serikali ya kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa asilimia 80 katika taasisi za umma zenye watu zaidi ya 100 ifikapo mwaka 2034.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *