Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameahirisha Baraza la Wawakilishi akifunga mjadala kuhusu hoja tatu zilizoibuka barazani na kuibua hisia tofauti mitandaoni juu ya Muungano, ajira kuchukuliwa na wageni na matibabu ya bima Zanzibar.
Hoja hizo ziliibuka kwa nyakati tofauti baada ya Kaimu Waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya kunukuliwa akihoji mwenendo wa watu wasiokuwa Wazanzibari kwenda kutibiwa visiwani humo kupitia matibabu kadi, ambayo ni maalumu kwa Wazanzibari.
Amesisitiza kuwa bajeti ya Zanzibar ni Sh8 trilioni pekee, hivyo haiwezi kubeba gharama za matibabu kwa watu milioni 60 kauli iliyoibua mjadala hasa kwa wananchi wa Tanzania bara waliopokea kama ya kibaguzi.
Vilevile Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Khamis Hafidh maarufu (Diaspora) wakati akichangia hotuba ya bajeti ya wizara yake amesema Zanzibar ina hoteli 1,184 zilizosajiliwa, lakini wafanyakzi wengi katika hoteli hizo si Wazanzibari akisema wanatakiwa kufanya mapinduzi.
Hoja hizo ziliendelea kujadiliwa wakati wa michango mbalimbali ya wajumbe wa baraza hilo wengine wakifika mbali wakasema iwapo kuwatetewa Wazanzibari itaonekana ni ubaguzi, hivyo ni vyema Muungano uvunjike.
Wengine walisema Muungano hauwezi kuvunjika na Waznzibari ndio wanaonufaika zaidi ispokuwa vijana wa Kizanzibari ndio wanabagua kazi za kufanya.
Akizungumza leo Juni 23, 2026 wakati akiahirisha mkutano wa tatu wa Baraza la 11 la Wawakilishi, Hemed alieleza kwa kina mambo hayo akisema yanachagizwa na watu wanaotaka kujiletea sifa na umaarufu kwenye mambo ya msingi yanayogusa maisha ya watu akionya hawatafanikiwa.
“Sote tunakubaliana kwamba Muungano wetu sio tu wa kihistoria bali umejengeka kwa undani zaidi. Hatujachanganya udongo pekee, bali tumechanganya damu kupitia ndoa,” amesema Hemed.
“Wananchi wa pande zote mbili wana fursa ya kushiriki katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tazania bila ubaguzi, wowote.”
Katika kuthibitisha hilo, amesema katika kikao cha kushughulikia masuala ya Muungano kilichofanyika Aprili 26, 2026 Zanzibar, kimefanikiwa kuondoa hoja ya sukari kutoka Zanzibar kuingia soko la Tanzania Bara.
Amesema licha ya hoja za hivi karibuni kutawala mitandaoni, lakini hakuna ubaguzi wowote utakaoruhusiwa kwa pande zote.
“Leo hii wananchi wa Zanzibar ukienda katika mikoa yote ya Tanzania Bara tayari wana familia wana mali na wana vitu vingine vingi, hivyo hivyo kwa wananchi wa Tanzania Bara huku Zanzibar,” amesema.
Akizungumza kuhusu Bima ya Afya kwa Wote, Hemed amesema ni mageuzi ya kimkakati katika sekta ya afya yanayolenga upatikanaji wa huduma bora, za haki na endelevu bila vikwazo vya kifedha, huku yakijenga mfumo wa mshikamano wa kijamii na uwajibikaji wa pamoja.
Amesema Zanzibar imeweka msingi wa utekelezaji wa mfumo huo kupitia sheria ya kuanzisha mfuko wa huduma za afya Zanzibar (ZHSF), sheria namba 1 ya mwaka 2023, ambapo kila mkaazi wa Zanzibar anatakiwa kujisajili kama wajibu wa kisheria, bila ya kujali hali ya ajira, kipato au eneo analoishi.
Amesema kwa upande wa Tanzania Bara, sheria namba 13 ya mwaka 2023 ya bima ya afya kwa wote, imeweka misingi imara ya kitaifa ya kuhakikisha wananchi wote wa Tanzania Bara wanashiriki katika mfumo rasmi wa Bima ya Afya.
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakimsikiliza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman wakati akihutubia baraza hilo na kutoa hoja ya kuliahirisha baada ya kumaliza mkutano wa Bajeti Chukwani Unguja, Zanzibar
“Hivyo, nawataka wananchi wote wa Tanzania kujiunga na mifumo rasmi ya Bima ya Afya inayotambulika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza changamoto za kifedha wakati wa matibabu na kuimarisha ufanisi wa huduma za afya,” amesema.
“Hivi karibuni Waziri Mkuu (Mwigulu Nchemba) amelitolea ufafanuzi pia, nadhani kuna watu walikuwa wanapotosha kwa kuleta mizozo kwa misingi yao ya kisiasa, lakini kwa lugha nyepesi ukiwa na kadi ya Zanzibar utatibiwa Tanzania Bara, lakini ukiwa na NHIF ya Tanzania Bara utapata matibabu Zanzibar kikubwa ni kujisajili na ni bure,” amesema.
Amesema wataweka mazingira mazuri zaidi kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka.
Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imeweka sera na mazingira mazuri kwa wananchi kujiajiri na kuajiriwa katika taasisi za umma na binafsi pamoja na utoaji wa huduma za umma ikiwamo huduma za afya.
“Hivyo, tunapenda kuwafahamasisha wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla suala la fursa za ajira na huduma zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kwa watu wote waliomo ndani ya visiwa vya Zanzibar bila ya kuangalia rangi, kabila, dini wala siasa,” amesema.
Kiongozi huyo amesema watu wote wataendelea kupata ajira kulingana na fursa husika.
“Hatutaangalia huyu anatoka Tanzania Bara wala anatoka Zanzibar, kama fursa hiyo anasifa, ataendelea kufanya kazi bila kuangalia anapotoka,” amesema Hemed.