
MKUU wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ), Kanali Said Juma Shamhuna, amesema kutwaa ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) ni juhudi za uwekezaji wa miaka 22.
Kanali Shamhuna alisema ubingwa huo ni matokeo ya juhudi zilizofanywa na wachezaji, viongozi na benchi la ufundi kuhakikisha timu hiyo inakuwa miongoni mwa timu bora ligi hiyo.
Kiongozi huyo alisema, mafanikio hayo yamekuja baada ya timu kupitia misimu kadhaa ya ushindani mkubwa ambapo ilikosa taji hilo kwa tofauti ndogo ya pointi na wakati mwingine idadi ya mabao.
“Kwa misimu iliyopita tumekuwa tukikaribia kutwaa ubingwa, lakini tulikosa kwa tofauti ndogo sana, tulijifunza kutokana na changamoto hizo na kuamua kuongeza juhudi ili kufikia ndoto yetu ya kuwa mabingwa,” alisema.
Alisema, hali hiyo haikuwakatisha tamaa, badala yake iliwapa nguvu ya kuongeza juhudi, nidhamu na mshikamano uliowezesha kufikia lengo la kutwaa ubingwa msimu huu.
Kanali Shamhuna aliwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa KVZ kwa kujituma kwao na kuwataka kuendelea kudumisha nidhamu, mshikamano na ari ya ushindani ili kuendeleza mafanikio hayo katika misimu ijayo.
Aidha, aliwataka wachezaji kutambua kuwa ubingwa huo ni heshima na wana wajibu wa kuendelea kuutangaza vyema mchezo wa soka Zanzibar kupitia matokeo mazuri.
Ubingwa huo unaifanya KVZ kuingia katika historia kama moja ya timu zilizofanikiwa kutwaa taji la Ligi Kuu ya Zanzibar baada ya juhudi za muda mrefu za kulitafuta taji hilo.
Timu hiyo baada ya kutwaa ubingwa huo msimu huu 2025-2026, imefanikiwa kuondoka na kombe na Sh50 milioni, ikiiacha JKU nafasi ya pili ikiambulia Sh20 milioni, wakati Zimamoto ikiondoka na Sh10 milioni kwa kushika nafasi ya tatu na ya nne imekamatwa na Mlandege