
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Baqer Qalibaf, ametoa wito kwa mataifa ya Asia Magharibi na ulimwengu wa Kiislamu kuanzisha mpangilio mpya wa kikanda unaotegemea uwezo, rasilimali na watu wa mataifa hayo, akisisitiza kwamba “chanzo cha misiba yote ni utawala wa Kizayuni.”
Akizungumza pembeni mwa kikao cha 20 cha Muungano wa Mabunge ya Nchi za Kiislamu (PUIC) kilichofanyika Baku siku ya Jumatano, Qalibaf alikutana na Spika wa Bunge la Uturuki, Numan Kurtulmuş, pamoja na Spika wa Bunge la Azerbaijan, Sahiba Gafarova, akitoa wito wa kuimarishwa kwa mshikamano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu.
Katika mazungumzo yake na Kurtulmuş, Qalibaf alirejea matokeo ya vita vya Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Iran, vya siku 12 vya Juni 2025 na Vita vya Ramadhani vya siku 40 vilivyoanza Februari 28, ambapo amesisitiza mafunzo muhimu ambayo mataifa ya eneo hilo na ulimwengu wa Kiislamu yanapaswa kuyazingatia.
Qalibaf amefafanua ukubwa wa mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, akieleza mashambulizi ya mabomu hayo kuwa “yasiyowazika” na “makubwa hata kuliko baadhi ya vita vikuu vya enzi ya kisasa.”
Amesema Iran ilijibu “kwa ukali na kwa usahihi,” huku akiwapongeza wananchi wa Iran kwa uimara wao na kwa kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya miji na vijiji kwa zaidi ya siku 110.
Aidha ametoa shukrani kwa Uturuki kwa kuiunga mkono Iran na kulaani “uchokozi wa kinyama” wa Marekani na Israel.
Qalibaf amesema mshikamano kati ya nchi za Kiislamu ni “wa lazima na hauepukiki.”
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na mwenzake wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan, wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu kujadili matukio ya kikanda, huku mataifa ya Kiarabu ya Ghuba ya Uajemi yakipanga upya mkakati wao kujikurubisha na Iran baada ya vita vilivyofichua mipaka ya uwezo wa Marekani.
Araghchi alimweleza waziri wa Saudi siku ya Jumatano kuhusu hatua za karibuni katika utekelezaji wa makubaliano ya pande mbili na mazungumzo yanayoendelea kufuatia hati ya makubaliano ya awali (MoU) kati ya Marekani na Iran iliyosainiwa tarehe 18 Juni.
Wanadiplomasia hao wawili wakuu walisisitiza umuhimu wa kudumisha njia za mawasiliano ya kidiplomasia, kuimarisha ushirikiano wa pamoja kwa ajili ya kuunga mkono utulivu wa kikanda, na kufikia matokeo chanya na endelevu.
Mazungumzo hayo yamefanyika wakati duru za habari zinadokeza kuwa Saudi Arabia inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo yanayolenga kurekebisha uhusiano kati ya Iran na nchi za Ghuba ya Uajemi kufuatia vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Shirika la habari la AFP lilinukuu mwanadiplomasia anayefahamu mipango hiyo akisema siku ya Jumatano kwamba mkutano wa kikanda unapangwa kufanyika Riyadh na unaweza pia kujumuisha nchi nyingine jirani, ingawa tarehe rasmi bado haijawekwa.
Kwingineko, Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, alisafiri kwenda Muscat siku ya Jumatano kwa lengo la kuanzisha mchakato wa mazungumzo kati ya Iran, nchi za Ghuba ya Uajemi na Iraq kuhusu mustakabali wa uendeshaji wa Mlango Bahari wa Hormuz.