UONGOZI wa Azam FC, umeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya winga wake Idd Seleman ‘Nado’ wakati huu wa sasa kufikia ukomo mwishoni mwa msimu, huku akihusishwa kutakiwa Yanga na Simba.

Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti Nado bado ni mchezaji anayehitajika  kwa ajili ya msimu ujao, ambapo taratibu za mazungumzo ya kusaini mkataba mpya zimeanza na ziko hatua nzuri zaidi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu Msaidizi wa Azam, Rashid Seif alisema suala lolote linalohusu usajili au kuboresha mkataba wa mchezaji wowote wa klabu hiyo watatoa taarifa rasmi, hivyo kwa sasa ni mapema pia kuzungumzia hilo.

Mwanaspoti linatambua Nado ni miongoni mwa wachezaji wanaopigiwa hesabu za kusajiliwa na miamba wa soka nchini Yanga na Simba, ambapo hata hivyo, bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa na sasa Azam FC inataka kumuongeza mkataba mpya.

Nado aliyejiunga na Azam FC tangu Julai 1, 2019, akitokea Mbeya City, amekuwa muhimili mkubwa wa kikosi hicho cha Azam FC, ambapo hadi sasa msimu huu amechangia mabao 14 ya Ligi Kuu kati ya 42, baada ya kufunga nane na kuasisti sita.

Idadi hiyo ya mabao ya msimu huu ni mengi zaidi tofauti na aliyochangia msimu uliopita wa 2024-2025, ambapo nyota huyo aliyeichezea pia Ashanti United, alichangia mabao 11 ya Azam katika Ligi Kuu, baada ya kufunga sita na kuasisti matano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *