Matetemeko hayo mawili yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Richter yalitokea ndani ya muda wa chini ya dakika moja, yakiharibu nyumba, hospitali, barabara na miundombinu mingine muhimu. Serikali ya Venezuela imetangaza hali ya dharura huku vikosi vya uokoaji vikiendelea kutafuta manusura katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Maafisa wamesema kuwa hadi sasa watu 164 wamethibitishwa kufariki dunia, ingawa idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka kutokana na ugumu wa kufikia baadhi ya maeneo yaliyoathirika vibaya.

Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, amesema kuwa Umoja wa Mataifa umejizatiti kikamilifu kusaidia juhudi za kukabiliana na janga hilo.

“Umoja wa Mataifa umejizatiti kikamilifu kuisaidia Venezuela baada ya matetemeko haya mabaya,” amesema Bwana Fletcher kupitia ukurasa wa mtandao wa X na akaongeza kuwa yuko katika mawasiliano ya karibu na timu ya Umoja wa Mataifa mjini Caracas inayoongozwa na Mratibu wa Kibinadamu, Gianluca Rampolla.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inaratibu upelekaji wa haraka wa timu za kimataifa za utafutaji na uokoaji mijini pamoja na kutuma wafanyakazi wa ziada kuimarisha operesheni za msaada nchini humo.

Janga juu ya janga

Bwana Fletcher amekaribisha mshikamano mkubwa wa kikanda na kimataifa, lakini ametahadharisha kuwa janga hilo linaweza kuzidisha mahitaji ya kibinadamu yaliyokuwepo tayari nchini Venezuela, ambako karibu watu milioni nane walikuwa wanahitaji msaada kabla ya matetemeko hayo.

“Mahitaji ya dharura yanayotokana na janga hili yanaonesha umuhimu wa kuendelea kwa msaada wa kimataifa,” amesema.

UNOPS

Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Miradi na Huduma (UNOPS), Jorge Moreira da Silva, ametoa pole kwa waathirika na familia zao, akisema shirika hilo liko tayari kusaidia juhudi za dharura.

“Tunasimama pamoja na watu wa Venezuela na tuko tayari kusaidia juhudi za haraka za kukabiliana na athari za janga hili pale itakapohitajika,” amesema, akitaja uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu muhimu mjini Caracas na maeneo mengine yaliyoathirika.

UNHCR na WFP

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) pia limesema liko tayari kusaidia juhudi za misaada kwa kushirikiana na mamlaka za kitaifa na wadau wa kibinadamu.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limeahidi kutoa msaada wake huku mashirika ya kibinadamu yakiendelea kutathmini mahitaji ya chakula, malazi na huduma za usafirishaji katika jamii zilizoathirika.

Kwa upande wake, Tume Huru ya Kimataifa ya Kuchunguza Ukweli kuhusu Jamhuri ya Bolivaria ya Venezuela imeeleza mshikamano wake na waathirika wa janga hilo na kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia watu wote wanaohitaji.

Operesheni za utafutaji na uokoaji zimeendelea Alhamisi huku wahudumu wa dharura wakikimbizana na muda kufikia maeneo yaliyotengwa na kutathmini ukubwa halisi wa uharibifu.

Mashirika ya kibinadamu yameonya kuwa janga hilo linaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya kibinadamu nchini Venezuela na kuongeza mzigo kwa jamii ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi na kijamii.

Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaendelea kufanya kazi kwa karibu na mamlaka za Venezuela kubaini mahitaji ya kipaumbele na kuratibu msaada wa kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *