Chanzo cha picha, Getty Images
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kushambulia na kuharibu madaraja na vituo vya kuzalisha umeme nchini Iran wiki ijayo ikiwa nchi hiyo haitarejea kwenye meza ya mazungumzo.
Kauli hizo zilitolewa katika mahojiano na shirika la habari la Fox News, huku Marekani na Iran zikiendelea kushambuliana kwa siku ya nne mfululizo.
Awali, Trump alibatilisha tishio la kutoza ada ya asilimia 20 kwa shehena zote zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, lakini baadaye akaendelea na hatua za kuzuia usafirishaji wa mizigo kupitia bandari za Iran.
“Nchi hiyo itakumbana na hali mbaya sana wiki ijayo,” Trump alisema. “Tutaharibu vituo vyao vyote vya kuzalisha umeme.”
Chanzo cha picha, Reuters
Mwezi Aprili, Trump alitishia kushambulia miundombinu ya kiraia nchini Iran, ikiwemo madaraja na vituo vya kuzalisha umeme.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, alijibu wakati huo kwa kusema,”Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kushambulia kwa makusudi raia na miundombinu ya kiraia ni uhalifu wa kivita.”
Mikataba ya Geneva ya mwaka 1949 kuhusu sheria za kibinadamu wakati wa vita inapiga marufuku mashambulizi dhidi ya maeneo yanayochukuliwa kuwa muhimu kwa maisha na ustawi wa raia.
Trump amesema kuwa wapatanishi wa Marekani waliwaambia wenzao wa Iran Jumanne jioni kwamba, “Ni heri mkubali kufanya makubaliano, la sivyo hamtabaki na chochote.”
Kuongezeka kwa kauli hizi kali na zenye vitisho kunakuja baada ya Trump kusema kwamba ushuru wa asilimia 20 aliokuwa ametishia kutoza kwa usafirishaji wa bidhaa kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz ungeondolewa na badala yake kuwepo makubaliano ya biashara na uwekezaji na mataifa ya Ghuba.
Tangazo la Trump lilitolewa saa chache kabla ya jeshi la Marekani kufanya mashambulizi yaliyodumu kwa saa saba dhidi ya Iran na huku wakiendelea kuzuia bandari zake.
Kulingana na jeshi la Iran, wanajeshi takriban saba waliuawa katika mashambulizi ya Marekani yaliyolenga kambi ya kijeshi katika mji wa Bampur, kusini mashariki mwa Iran, siku ya Jumatano.
Wakati huo huo, televisheni ya taifa ya Iran, IRIB, iliripoti kuwa Tehran ilirusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea maeneo yaliyoko kambi za Marekani nchini Jordan, Kuwait na Bahrain.
Mapema Jumatano, jeshi la Kuwait lilisema lilidungua ndege zisizo na rubani za Iran, huku jeshi la Bahrain likisema lilifanikiwa kuzuia mashambulizi ya angani.
Marekani pia ilidai kuwa Iran iliwalenga kwa makusudi raia katika eneo hilo kwa kushambulia meli saba za kibiashara, jambo ambalo, kwa mujibu wa Centcom, limesababisha karibu watu 12 kuuawa, kutoweka au kujeruhiwa.
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) imesema Jumatatu usiku kuwa makombora ya masafa marefu ya Iran yalilenga meli mbili za mafuta za taifa hilo, na kusababisha mfanyakazi mmoja kuuawa huku wengine wanane wakijeruhiwa.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilithibitisha mashambulizi hayo kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye Telegram. Katika taarifa hiyo, ilidai kuwa meli hizo mbili zilipuuza onyo walizopewa, zilizima mifumo yao ya urambazaji na kujaribu kupita katika njia iliyokuwa imewekwa mabomu ya baharini.
Hayo yakijiri, baharia mmoja wa Kihindi aliyekuwa ametoweka baada ya meli yake kushambuliwa karibu na pwani ya Oman wiki iliyopita alipatikana amefariki dunia, familia yake ilithibitisha siku ya Jumatano.
Wafanyakazi wengine 23 waliokuwa ndani ya meli ya GFS Galaxy, iliyosajiliwa nchini Cyprus, waliokolewa baada ya meli hiyo kushindwa kuendelea na safari yake siku ya Jumapili. Centcom iliishutumu IRGC kwa kuhusika na shambulio hilo, lakini Tehran ilikuwa bado haijatoa tamko lolote
Mapigano mapya kati ya Marekani na Iran yamesababisha bei ya mafuta duniani kupanda kwa kasi, huku usafirishaji wa meli za kubeba mafuta kupitia Mlango Bahari wa Hormuz ukusimama kabisa.
Iran imeishutumu Marekani kwa kuingilia usimamizi wake wa Mlango bahari wa Hormuz, huku udhibiti wa njia hiyo ukiipa Tehran uwezo wa kutishia uchumi wa dunia.
Siku ya Jumatatu, Trump alitangaza kuwa Marekani sasa ndiyo “mlinzi” wa Mlango Bahari wa Hormuz, na akaahidi kutoza ada ya asilimia 20 kwa mizigo yote inayosafirishwa kupitia njia hiyo ya bahari ili kugharamia ulinzi wake.
Trump pia alitangaza kurejesha kizuizi cha kijeshi dhidi ya bandari za Iran.
Katika ujumbe wake wa hivi karibuni kwenye Truth Social, Trump aliandika,”Nimeamua kubatilisha ada ya asilimia 20 ya Marekani dhidi ya usafirishaji wa bidhaa kupitia Mlango wa Hormuz badala yake mataifa mbali mbali ya Ghuba yatawekeza nchini marekani kugharamia hilo”
Rais huyo wa Marekani hakutoa maelezo zaidi kuhusu mpango huo.
Pia alisema kuwa mlango huo wa bahari “uko wazi kwa meli zote isipokuwa za Iran,” na kwamba “mafuta yanapita kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali, kutokana na nguvu kubwa ya Jeshi la Marekani.”
Kujibu tangazo la Trump, Iran imesema itaendelea kudhibiti Mlango Bahari wa Hormuz.
Naibu Waziri wa Mambo ya kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, alisema uamuzi wa Trump wa kurejesha Kizuizi cha kijeshi “kwa namna fulani umevunja” makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano”
Gharibabadi pia alinukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa,
“Ikiwa Marekani inadhani kuwa kwa kuongeza mashambulizi yake ya kijeshi na kutuzuia kiuchumi tutarejea kwenye meza ya mazungumzo, basi inakosea.”