
Akihutubia wajumbe kwenye ukumbi wa Baraza Kuu wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya Tume hiyo pamoja na Mfuko wa Ujenzi wa Amani (PBF), Guterres amesema taasisi hizo zimekuwa zikiisaidia jamii nyingi kurejea katika hali ya utulivu baada ya vita kwa kipindi cha miongo miwili.
Ametolea mfano Colombia, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Liberia, huku Mfuko wa Ujenzi wa Amani ukiwekeza zaidi ya dola bilioni mbili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006 na kusaidia zaidi ya nchi 75 duniani.
“Chonde chonde nchi wanachama endeleeni kuunga mkono juhudi za ujenzi wa amani kupitia michango ya hiari, kwani ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kujenga dunia isiyo na vurugu,” amesema Guterres.
Balozi Hilale azungumzia PBC: Colombia nayo yapaza sauti
Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Ujenzi wa Amani ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Morocco katika Umoja wa Mataifa, Balozi Omar Hilale, amesema ni heshima kubwa kuadhimisha miaka 20 ya Tume hiyo katika ukumbi uleule ambako ilianzishwa mwaka 2006.
“Kwa kipindi hicho Tume imefanikiwa kutekeleza dhamira yake ya kuzipatia nchi zinazotoka kwenye migogoro msaada wa muda mrefu kwa kushirikisha serikali, taasisi za kifedha za kimataifa, mashirika ya kikanda, asasi za kiraia na sekta binafsi,” amesema.
Colombia imetajwa moja ya nchi nufaika mbapo Mwakilishi wake wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa Balozi Leonor Zalabata Torres, akizungumza kwa kofia ya Urais wa Baraza la Usalama kwa mwezi Juni, amesema juhudi za kitaifa za kujenga na kudumisha amani ni msingi muhimu wa kulinda amani na usalama wa kimataifa.
“Baraza la Usalama linaendelea kuitambua Tume ya Ujenzi wa Amani kama jukwaa muhimu la kuratibu ushirikiano na kuwaleta pamoja wadau mbalimbali ili kuunga mkono mikakati ya nchi katika kujenga amani endelevu,” amefafanua.
Nina ushuhuda wa dhati wa manufaa ya PBF – Balozi Macharia Kamau
Amesema ushahidi wa miaka 20 ya utekelezaji wa mfuko huo unaonesha wazi kuwa uwekezaji katika kuzuia migogoro na kujenga amani huleta matokeo chanya, akisema mafanikio ya mfuko huo yamewezekana kutokana na uungwaji mkono wa nchi wanachama pamoja na Tume ya Ujenzi wa Amani.
“Nilipokuwa Mjumbe Maalum wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ajili ya eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, nilijionea jinsi amani ilivyo dhaifu na jinsi hatua za mapema zilivyo muhimu. Baada ya kuchunguza ushahidi wa miaka 20 ya ujenzi wa amani, hitimisho ni moja tu: ujenzi wa amani na kuzuia migogoro hufanya kazi. Mfuko huu huchukua hatua kwa haraka, huwezesha viongozi wa kitaifa na wa ngazi za jamii kutekeleza mipango yao ya amani, na huwaleta pamoja Umoja wa Mataifa na washirika wengine katika kuunga mkono juhudi hizo,” amesema Balozi Kamau.
Tukio la leo likiambatana na video maalum ya kuonesha shughuli za Mfuko wa Ujenzi wa Amani, ni sehemu ya maadhimisho hayo ni sehemu ya Wiki ya Ujenzi wa Amani ya Umoja wa Mataifa yaliyoanza tarehe 22 mwezi huu na yanatamatishwa Ijumaa tarehe 26 Juni.