Marta Hurtado ambaye ni Msemaji wa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amewaeleza waandishi wa habari leo jijini Geneva, Uswisi kwamba, Türk amesema inatia wasiwasi kwamba, kwa mujibu wa takwimu rasmi za Serikali ya Marekani, watu 18 walifariki katika vituo vya kizuizini vya ICE katika miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu. Kifo kingine pia kimeripotiwa mwezi huu. Kwa mwaka 2025, jumla ya vifo 33 vilirekodiwa, ikilinganishwa na vifo 11 mwaka 2024.

Katika taarifa ambayo ofisi ya Kamishna imeisambaza kwa vyombo vya habari, Türk  anasema ukosefu wa uwazi kuhusu mazingira ya vifo hivyo unadhoofisha uwajibikaji.

“Ninatoa wito wa kufanyika haraka kwa uchunguzi huru, usio na upendeleo na wenye ufanisi kuhusu vifo vyote vinavyotokea chini ya ulinzi wa ICE. Wale wanaobainika kukiuka sheria wanapaswa kuwajibishwa, na haki za familia za waathirika kupata ukweli, haki, fidia na dhamana ya kutorudiwa kwa matukio hayo zinapaswa kuheshimiwa,” amesema Türk.

Vifo hivyo vimetokea wakati mfumo wa Marekani wa kuwashikilia wahamiaji umeendelea kupanuka. Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa ICE kwa sasa inawashikilia zaidi ya watu 60,000, ikilinganishwa na takriban watu 40,000 mwanzoni mwa mwaka 2025. Pia kuna mipango ya kuongeza uwezo wa vituo hivyo hadi kuwahifadhi watu 90,000 ifikapo mwisho wa mwaka huu 2026.

Huduma hafifu

Taarifa imeeleza kwamba watu wanaozuiliwa, wakiwemo familia nzima zenye watoto na watu wenye matatizo ya kiafya, mara nyingi huripotiwa kukabiliwa na mazingira yasiyo ya kibinadamu, yakiwemo ukosefu wa huduma za afya na chakula cha kutosha pamoja na hatari ya magonjwa kutokana na msongamano mkubwa katika vituo hivyo. Pia kumekuwa na madai yanayotia wasiwasi kuhusu matumizi ya nguvu.

Aidha, vifo vitano kati ya vilivyoripotiwa rasmi mwaka 2026 vimeainishwa kuwa ni kwa kujiua.

Ripoti pia zimeeleza kuwa kuna ukosefu wa taarifa kuhusu mahali walipo wanaozuiliwa wanapohamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine, jambo linalosababisha huzuni na wasiwasi mkubwa kwa familia zao. Kutokuwa na uhakika kuhusu hali zao za kisheria na taratibu za uhamiaji pia kunachangia msongo wa mawazo kwa wanaozuiliwa.

Türk pia ameonesha wasiwasi kuhusu matumizi ya kifungo cha upweke, akisema kuwa hatua hiyo inapaswa kutumiwa kwa nadra sana, na inapodumu kwa muda mrefu au bila ukomo inaweza kufikia kiwango cha matendo ya kikatili, yasiyo ya kibinadamu au yanayodhalilisha utu.

“Mambo haya yote yanaongeza mazingira ya hatari na kuibua wasiwasi mkubwa kuhusu iwapo baadhi ya vifo hivi vilivyotokea chini ya ulinzi wa ICE vingeweza kuzuilika,” amesema Kamishna Mkuu huyo.

Zitumike njia mbadala

Amesisitiza kuwa njia mbadala za kuwazuilia wahamiaji zinapaswa kupewa kipaumbele. Amesema kuwa kuwazuia wahamiaji kunapaswa kuwa hatua ya mwisho na ya kipekee, na kwa ujumla kunapaswa kuepukwa kwa watu wenye matatizo makubwa ya afya ya mwili au akili pamoja na wanawake wajawazito.

Pia amesisitiza kuwa watoto hawapaswi kuwekwa kwenye vituo vya kizuizini vya wahamiaji bila kujali hadhi yao ya uhamiaji au ya wazazi wao.

Türk amesema mamlaka za uhamiaji za Marekani zinapaswa kuhakikisha kuwa vituo vyao vya vizuizi vinafuata viwango na kanuni za kimataifa za haki za binadamu. Hii ni pamoja na kuheshimu utu wa watu, kuepuka msongamano, kutoa huduma za afya kwa wakati ikiwemo huduma za afya ya akili, kuwajulisha familia, kuruhusu msaada wa kibalozi, uwakilishi wa kisheria na huduma za ukalimani kwa watu wote walioko kizuizini.

Kamishna Mkuu pia ametoa wito wa kurejeshwa na kuimarishwa kwa mifumo huru ya uangalizi wa vituo vya kuwashikilia wahamiaji, akisema kuwa mifumo hiyo ni kinga muhimu dhidi ya vitendo vya unyanyasaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa vyombo vya Bunge la Marekani katika kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji na matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha utekelezaji bora wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Türk amelaani vikali kuendelea kwa tabia ya kuwavua utu na kuwahalalisha wahamiaji na wakimbizi kama wahalifu. Ameeleza kuunga mkono watu na taasisi zote zinazoendelea kutetea utu, usawa na ulinzi wa haki za binadamu, wakiwemo wanasheria, wanahabari, mashirika ya kidini na makundi ya kiraia.

Amesisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kurejeshwa mahali ambapo anaweza kukabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu au madhara mengine yasiyoweza kurekebishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *