
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), hadi watu milioni 6.8 wanaweza kuathiriwa na janga hilo lililotokea wiki hii Jumatano Juni 24, kulingana na makadirio ya hivi karibuni ya idadi ya watu na kiwango cha uharibifu.
Kupitia mfumo wa mtandaoni uliowekwa kwa ajili ya kuripoti waliopotea, zaidi ya watu 41,000 pia wameripotiwa kutoweka.
Wanachimba kwa mikono
Wakati huohuo, taarifa zinaeleza kuwa baadhi ya waokoaji katika maeneo yaliyoathirika wanachimba vifusi kwa mikono yao wenyewe, huku watu wengi wakiendelea kuwa na hofu ya kurejea katika nyumba zao au majengo mengine yaliyoharibiwa.
“Watu bado wana hofu ya kurejea katika nyumba zao za zamani au miundombinu mingine, na wanahitaji msaada,” limesema Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC), shirika ambalo ni mshirika wa Umoja wa Mataifa.
Matetemeko hayo yenye ukubwa wa kipimo cha 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Richter yaliathiri zaidi wilaya ya mji mkuu Caracas pamoja na majimbo ya Miranda, Carabobo, Yaracuy na La Guaira.
Mkurugenzi wa Kanda ya Amerika wa IFRC, Loyce Pace, amesema kuwa wakazi wengi walikimbia bila kuchukua chochote.
“Watu wameacha kila kitu na hakuna kinachofanya kazi kama ilivyokuwa katika maeneo haya. Kipaumbele chetu sasa ni kuhakikisha watu wanapata mahitaji ya msingi ili waweze kuendelea kuishi,” alisema Pace akiwa Panama kupitia mkutano wa video na waandishi wa habari mjini Geneva.
Mahitaji ya huduma za afya pia yameelezwa kuwa ni ya dharura
Mkurugenzi wa Dharura za Afya wa Shirika la Afya la nchi za America (PAHO), Dkt. Ciro Ugarte, amesema kipaumbele kikubwa ni kutoa huduma za kuokoa maisha na kuwaokoa watu wengi iwezekanavyo.
“Saa za kwanza baada ya janga ni muhimu sana katika kuokoa maisha,” amesema.
Dkt. Ugarte ameeleza kuwa timu za matibabu zinakabiliwa na changamoto ya kuhudumia idadi kubwa ya majeruhi, wakiwemo waliovunjika mifupa, walioungua na waliojeruhiwa kutokana na kuporomoka kwa majengo.
Pia amebainisha kuwa upatikanaji wa maeneo yaliyoathirika bado ni mgumu sana kwa timu za misaada, hasa katika sekta ya afya.
“Tumekuwa tukihangaika kufikia vituo vyote vya afya,” amesema.
Mbali na huduma za afya za dharura, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limesema watu waliopoteza kila kitu wanahitaji makazi ya muda, maji salama, huduma za usafi wa mazingira, huduma za afya, ulinzi na vifaa muhimu vya msaada.
Afisa wa IOM, Zoe Brennan, amesema juhudi za kurejesha maisha ya kawaida zitahitaji kuendelea kwa muda mrefu ili kusaidia familia kujenga upya makazi yao, kurejesha vyanzo vyao vya kipato na kupona kwa heshima.
Mashirika ya misaada pia yameeleza kuwa matetemeko hayo yameikumba Venezuela wakati nchi hiyo tayari ilikuwa katika mazingira magumu kutokana na changamoto za kiuchumi na ukiukwaji wa haki za binadamu uliodumu kwa miaka mingi, hali ambayo imesababisha mamilioni ya raia kuondoka nchini.
Shida ya intaneti
Wakati huo huo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) imethibitisha kuwepo kwa hitilafu kubwa ya huduma za intaneti nchini Venezuela baada ya matetemeko hayo.
Msemaji wa ofisi hiyo, Marta Hurtado, amesema vikwazo vilivyokuwapo kabla ya janga hilo bado vinaendelea.
“Tunatoa wito, kama tulivyofanya hapo awali, kuchukuliwa hatua za kulinda mazingira ya kidijitali na kuhakikisha haki ya kupata taarifa, uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa vyombo vya habari vya kidijitali nchini Venezuela,” amesema Hurtado.
UNHCR
Nalo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kupitia Mkuu wa Kitengoc ha Afya ya Jamii cha shirika hilo Dkt. Allen Maina limesema linaendelea kuhamasisha wafanyakazi na rasilimali zake ili kukabiliana na athari za matetemeko hayo na kwamba kwa sasa, juhudi za Serikali ya Venezuela zimeelekezwa katika shughuli za utafutaji na uokoaji, utoaji wa huduma za matibabu ya dharura na tathmini ya kiwango cha uharibifu na kwamba UNHCR iko tayari kuunga mkono juhudi za mwitikio huo kwa kushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, huku ikiendelea kuhamasisha msaada na kupanga upya vifaa vya dharura vilivyopo ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kujitokeza.