Taarifa hizo zimetolewa na James Swan, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, aliyoitoa mbele ya Baraza hilo lililokutana Ijumaa mchana kwenye mjadala wa wazi kujadili hali inayoendelea kwenye taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika kwa kuzingatia ripoti ya Katibu Mkuu iliyosambazwa kwa wajumbe tarehe 19 mwezi huu wa Juni.

“Wananchi wa mashariki mwa nchi wanaendelea kukabiliwa na moja ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu barani Afrika, huku mapigano kati ya makundi yenye silaha yakiongezeka, maelfu wakilazimika kuyahama makazi yao, na mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola ukitishia matumaini ya kufikiwa kwa amani ya kudumu,” amesema Swan ambaye pia ni Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO.

Ikiwa ni hotuba yake ya kwanza tangu achajuliwe na Katibu Mkuu kushika wadhifa huo, Bwana Swan ameweka bayana kuwa hali ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo bado ni “ngumu, tete na yenye madhara makubwa kwa wananchi,” licha ya hatua muhimu zilizopigwa katika juhudi za kidiplomasia ndani ya mwaka mmoja uliopita.

Hotuba yake imekuja takribani mwaka mmoja tangu kusainiwa kwa Mkataba wa Amani wa Washington kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, pamoja na Mchakato wa Doha wa Makubaliano ya Kina ya Amani, unaolenga kumaliza mzozo wa muda mrefu mashariki mwa DRC.

“Ni muhimu sasa kuhakikisha kasi ya juhudi hizi inaendelea, na kwamba ahadi zote zilizotolewa na waliotia saini zinatekelezwa kikamilifu,” Swan ameliambia Baraza la Usalama.

Raia wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa vita

Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea, mapigano bado ni makali katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako waasi wa AFC/M23, wanaodaiwa kuungwa mkono na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), wanaendelea kupambana na Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (FARDC) pamoja na makundi washirika wake.

Mapigano ya hivi karibuni yamejikita katika eneo la Rubaya, ambalo ni kitovu muhimu cha uchimbaji madini pamoja na Rutshuru jimboni Kivu Kaskazini, pamoja na nyanda za juu za Minembwe huko Kivu Kusini.

Vifo vya raia na matumizi ya droni za kivita

Matumizi ya ndege zisizo na rubani za kivita, mizinga na silaha nzito yameongeza kwa kiasi kikubwa hatari kwa raia na kusababisha uharibifu wa miundombinu muhimu.

Tangu mwezi Machi, MONUSCO imerekodi vifo vya raia 632 vilivyotokana na mapigano jimboni Kivu Kaskazini na Ituri. Wakati huo huo, mashambulizi ya kundi la Allied Democratic Forces (ADF) yameongezeka na kuua raia 287 jimboni Ituri, wakiwemo wanawake 44, huku raia wengine 66, wakiwemo wanawake na watoto, wakipoteza maisha katika eneo la Beni, Kivu Kaskazini.

Mbali na vifo hivyo, makundi yenye silaha yamehusishwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyohusiana na migogoro, kuwahamisha watu kwa nguvu kutoka makazi yao na kuzuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, hali inayozifanya jamii zilizoathirika kuwa katika mazingira magumu zaidi.

Benki Goma bado zimefungwa halikadhalika uwanja wa ndege Goma

Mapigano ya muda mrefu yamewaacha mamilioni ya watu wakihangaika kupata mahitaji yao ya msingi.

Swan ameonya kuwa kufungwa kwa benki pamoja na viwanja vya ndege vya Goma na Kavumu kunaendelea kuongeza mateso kwa wananchi na kuchelewesha usambazaji wa misaada ya kuokoa maisha.

Ebola yaongeza changamoto kwa juhudi za amani

Mbali na vita vinavyoendelea, DRC sasa inakabiliwa na mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola uliotangazwa rasmi na Serikali tarehe 15 Mei.

“Eneo ambalo mlipuko mkuu umetokea ni eneo lenye mapigano makali na mazingira ya mijini yenye huduma za afya zilizokwishaelemewa, jambo linaloongeza hatari kubwa ya kuenea zaidi kwa ugonjwa huu,” amesema.

Mlipuko wa Ebola unaonesha jinsi ukosefu wa usalama unavyoweza kudhoofisha juhudi za kudhibiti magonjwa, huku dharura za afya zikielekeza rasilimali ambazo zingetumika katika kujenga amani na kurejesha maendeleo.

Nuru ya matumaini inaonekana

Licha ya changamoto hizo, Swan ameeleza kuwa kuna maendeleo muhimu katika juhudi za kidiplomasia.

Serikali ya DRC na AFC/M23 tayari zimesaini makubaliano yanayowezesha utekelezaji wa mfumo wa kufuatilia usitishaji wa mapigano chini ya mchakato wa Doha. MONUSCO pia imeendelea kusaidia maandalizi ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Pamoja wa Uhakiki na Ufuatiliaji (EJVM+), ambao utasimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Wakati huo huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa umeendelea kulinda raia kupitia doria za pamoja na FARDC, kusaidia mipango ya amani katika ngazi za jamii, kuimarisha mageuzi ya sekta ya usalama, pamoja na kusaidia shughuli za kuwavua silaha, kuwavunja vikundi vya wapiganaji na kuwarejesha katika maisha ya kiraia.

Wito wa Kufikia Amani ya Kudumu

Swan amezitaka pande zote zinazohusika kuheshimu kikamilifu makubaliano ya Washington na Doha na kuendelea na juhudi za kumaliza mzozo kwa njia ya mazungumzo.

“Ninazihimiza pande zote zinazotekeleza makubaliano ya Washington na Doha kuendeleza mafanikio ya kidiplomasia yaliyopatikana hadi sasa na kuendelea na safari ya kuelekea amani ya kudumu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *