ILIPOISHIA

Wakwetu alimrudishia simu Sharifa bila kumuuliza chochote zaidi. Akaingia chumbani akiwa amekunja uso.

Sharifa alipobaki peke yake aliketi na kuanza kuwaza. Alijua kuwa mume wake alikuwa ameudhika na alikuwa ameanza kupata wasiwasi kati yake na Majaliwa.

Alijiambia ilikuwa ni juu yake kuhakikisha kuwa amani inarudi hapo nyumbani na mwanawe Majaliwa pia anarudi na kupokelewa na Wakwetu kwa mikono miwili.

Wakati wa kulala ulipowadia Sharifa alijichangamsha na kuanza kumpa maneno matamu Wakwetu ili kumsahaulisha maudhi na mawazo aliyokuwa nayo.

Usiku huo Wakwetu alioneshwa mapenzi ya hali ya juu ambayo hakuwahi kuyaona kwa Sharifa tangu amuoe. Mzee aliudisha moyo.

SASA ENDELEA…

ILE ilikuwa kama huduma ya kwanza ya kumtuliza Wakwetu. Sharifa alipoona amefanikiwa kumlegeza Wakwetu alijiambia kimoyomoyo.

“Hiyo ni trela, bado picha iko nyuma”

Asubuhi ya siku iliyofuata Wakwetu alipoondoka kwenda kazini, Sharifa alimpigia simu Majaliwa.

“Uko wapi?” akamuuliza.

“Niko hapa gesti ninapolala. Halafu mama pesa zimeniishia naomba unitumie nyingine”

“Mimi nakuja hapo hapo gesti. Nataka twende kwa mganga tukamtengeze huyu mzee”

“Kama unakuja huku , basi nakusubiri”

“Nikukute hapo nje, twende mara moja”

“Usisahau kuniletea pesa”

Sharifa hakumjibu, alikata simu. Alifuta ile namba ya Majaliwa kwenye simu yake. Akamuachia majukumu mtumishi wao wa ndani. Alimdanganya kuwa anakwenda Super Market.

Alipotoka alikwenda kituo cha teksi akakodi teksi iliyompeleka kwenye mtaa uliokuwa na gesti ambayo Majaliwa alikuwa anaishi tangu alipotoroka kwao.

Alimkuta Majaliwa amesimama mbele ya gesti hiyo. Sharifa alitoa kichwa kwenye dirisha akamuita. Majaliwa alikwenda akafungua mlango wa upande wa pili wa teksi akajipakia.

Teksi ikaondoka.

“Tunakwenda Machui” Sharifa alimwambia Majaliwa.

“Machui kwa nani?”

“Kwani nilkwambia nini kwenye simu?’

Majaliwa alijaribu kukumbuka, akasema.

“Ahaa…sasa ndio tunakwenda kwa teksi?”

“Acha twende kwa teksi tuwahi kurudi”

“Kwani baba amesemaje?”

“Ameona namba zako kwenye simu yangu. Ameanza kupata mashaka. Amejua kuwa tunawasiliana”

“Hajakubali nirudi nyumbani?”

“Atakubali tu, nitamuweka sawa”

Walifika Maccchui na kuteremshwa mbele ya nyumba  moja ambayo ujenzi wake ulikuwa haujakamilika lakini watu walikuwa wanaishi ndani.

“Tusubiri” Sharifa alimwambia dereva wa teksi wakati akishuka na Majaliwa.

Ile nyumba ilikuwa ya mganga wa kienyeji. Alikuwa mganga aliyepata sifa kwa kutengeza ndere za kupagawisha wanaume.

Kwa vile Sharifa alikuwa akimfahamu mganga huyo alipiga hodi na kuingia ndani. Upande wa kulia wa nyumba hiyo kulikuwa na sebule iliyokuwa imetandikwa busati. Hicho ndicho kilikuwa chumba cha mganga na shughuli za uganga zilifanyika humo.

Mganga mwenyewe alikuwa ameketi kwenye kigoda huku chetezo kilichokuwa kikifuka moshi kikiwa mbele yake.

Alikuwa mtu mzima aliyekwishapituka umri wa miaka sitini. Alikuwa amevaa shuka nyeupe na shati la rangi ya samawati.

“Karibuni” alimwambia Sharifa na mwanawe. Akaongeza.

“Nimeambiwa kuna wageni wanakuja mwanamke na mwanaume, bila shaka mtakuwa ni nyinyi”

“Tutakuwa ni sisi, kwa maana tulipanga tangu jana kuja kwako. Shikamoo”

“Marahaba. Karibuni sana” Mganga aliwakaribisha.

Sharifa alivua viatu kabla ya kulikanyaga busati. Alimwambia Majaliwa naye avue viatu.

“Wewe si mgeni machoni mwangu” Mganga alimwambia Sharifa wakati anaketi kwenye busati hilo.

“Niliwahi kufika kwako siku za nyuma”

“Ndyo, nakukumbuka. Sura yako inanijia akilini mwangu”

“Tuna matatizo kidogo”

“Nielezeni, ni matatizo gani?”

“Huyu niliyenaye hapa ni mwanangu. Ana matatizo na baba yake. Nataka waelewane”

“Wana matatizo gani?’

“Aliwahi kuchukua gari la baba yake bila ruhusa akaenda kugonga mtu ksha akakimbia na kuliacha gari. Baba yake amekasirika mpaka leo na mwanangu hafiki nyumbani” Sharifa alimueleza nusu nusu akiogopa kumueleza ukweli wote.

“Hiyo ni kazi ndogo tu”

“Na mimi mwenyewe pia nataka nimuweke sawa. Tangu jana nimegundua ameanza kuwa na mashaka na mimi”

Mganga akacheka kwa kujilazimisha.

“Hizo zote ni kazi ndogo kwangu. Unataka mumeo aweje kwa mwanao?”

“Amuite arudi nyumbani na ampende kama zamani na asahau yaliyopita”

“Na wewe mwenyewe unataka mumeo aweje kwako?”

“Nataka anipende, ninachomwambia anisikilize. Aondoe shutuma na chuki kwangu. Hata kama kuna kitu amegundua kwangu, adharau. Asikitilie maanani”

“Hapa mmefika. Jina langu mimi naitwa Mkuru Mandonga. Natoka Sumbawaga. Najulikana nchi nzima kwa huduma zangu. Mnazo shilingi laki mbili?” Mganga aliwambia.

“Punguza kidogo”

“Unazo ngapi?’

“Nusu yake”

“Nusu yake ni ndogo sana. Ongeza iwe Laaaki na nusu.”

“Laki na nusu sina na siwezi kurudi nyumbani kuchukua pesa nyingine. Muda haotoshi. Nimefanya kutoroka nyumbani. Mume wangu hajui kama nimeondoka. Nataka niwahi kurudi kabla hajafika nyumbani”

“Sasa tufanye kitu kimoja. Nikudai hizo zilizobaki, kesho uniletee”

“Sawa. Nitampa mwanangu akuletee”

Mganga akajiweka sawa.

“Tuanze na kazi ipi?” alimuuliza Sharifa.

“Tuanze na kazi ya mwanangu”

“Mume wako anaitwa nani?’

“Anaitwa Wakwetu. Unataka na la baba yake?”

“Hilo moja linatosha”

Mganga akaliandika jina hilo kwenye kipande cha karatasi kisha akakitia kikaratasi hicho ndani ya tunguri.

“Na mwano anaitwa nani?”

“Anaitwa Majaliwa”

Mganga akaandika jina la Majaliwa kwenye kipande kingine cha karatasi ambacho pia alikitia kwenye ile tunguri.

“Sogea hapa karibu yangu” Mganga alimwambia Majaliwa.

Majaliwa alisogea mbele ya mganga huyo.

“Kaa hapa hapa”

Mganga huyo alisema na kuchukua ile tunguri akaipuliza kwenye mdomo wake hadi ikatoa mlio kama wa vuvuzela. Baada ya hapo aliiweka tunguri hiyo kwenye kichwa cha Majaliwa na kuanza kuitabania maneno ya kiganga.

Kila alipotabana alitaja jina la Waketu na Majaliwa.

Alifanya hivyo kwa karibu nusu saa. Alipomaliza aliiondoa tunguri hiyo kichwani kwa Majaliwa na kuiweka mbele ya mdomo wa kijana huyo.

“Sasa nuia hapa unavyotaka” Mganga akamwambia Majaliwa.

“Ninuie vipi?” Majaliwa akamuuliza.

“Isemee hii tunguri vile unavyotaka kwa baba yako”

“Niisemee kwa sauti au kimya kimya?”

“Unavyotaka wewe”

Majaliwa akaisemea kimya kimya. Alinuia maneno mengi mpaka mganga akamwambia. “Imetosha”

Baada ya hapo mganga aliitabania tunguri hiyo maneno yake kisha akamwambia Majaliwa.

“Sasa nataka kukuchanja kidogo kwenye uso wako na kwenye ulimi wako”

“Ulimi pia unachanjwa?” Majaliwa akauliza.

“Ndiyo. Unachanjwa ili kila neno utakalosema limfurahishe baba yako. Na pia akiona uso wako afurahi hata kama alikukasirikia”

Mganga alichukua kiwembe kipya akakitoa kwenye karatasi na kumchanja chale tatu kwenye paji la uso wake.

“Sasa toa ulimi wako”

Majaliwa alitoa nje ulimi wake, mganga akauchanja chale moja. Baada ya kumchanja alichukua ile tunguri akamimina ujiuji uliokuwemo ndani kwenye kiganja chake. Kisha akauchovya ujiuji huo kwa kidole cha mkono mwingine na kumpaka Majaliwa kwenye zile sehemu alizomchanja.

Majaliwa alikunja uso, ulimi wake ulipopakwa ujiuji huo.

“Unaona ladha gani?” Mganga alimuuliza.

“Tamu tamu kama asali”

“Hukukosea ni asali kweli. Sasa nenda kapumzike nje”

Majaliwa akainuka na kutoka nje.

“Sasa wewe mama mtu itabidi uvue nguo” Mganga akamwambia Sharifa.

Sharifa akagutuka.

“Nibaki uchi kabisa?”

“Ndio uganga wenyewe mama”

“Mh!” Sharifa akaguna.

“Umesema unataka uwahi kurudi, mbona unasita sita au tuache?’

“Tusiache, nilikuwa nawaza tu”

“Unawaza nini?”

“Kitu chenyewe umeniambia kwa ghafla, sikuwa nimejiandaa”

“Wenzako wengi wamefanikiwa, ukienda kwa daktari kuwa tayari na utakachoambiwa”

“Sawa, ngoja nivue kwa sababu nina shida”

Sharifa alivua gauni akabaki na nguo za ndani.

“Endelea kuvua,” Mganga akamwambia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *