
DODOMA: Serikali imesema haijauza wala kukabidhi rasilimali za misitu au maliasili za Tanzania kwa mataifa ya nje kupitia makubaliano ya biashara ya kaboni.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 26, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amekanusha madai yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani, akieleza kuwa taarifa zinazodai serikali imekabidhi maliasili kwa wawekezaji wa nje si za kweli na zinapotosha umma.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka msingi wa kisheria na kiutawala wa kusimamia biashara ya kaboni ili kuhakikisha Tanzania inanufaika na soko la kimataifa la biashara hiyo.
Kwa mujibu wa Masauni, bajeti ya mwaka wa fedha wa sasa imetenga fedha kwa ajili ya kuanzisha mifumo ya usajili, ukaguzi na ufuatiliaji wa biashara ya kaboni.
Alieleza kuwa mifumo hiyo itasaidia kudhibiti shughuli zote zinazohusiana na biashara hiyo na kuhakikisha mapato yanayostahili yanapatikana kwa mujibu wa sheria.
Aidha, alisema serikali imeunda kamati ya wataalamu kutoka wizara mbalimbali ili kupitia fursa zilizopo katika sekta ya biashara ya kaboni na kupendekeza namna bora ya kuongeza manufaa kwa taifa bila kuhatarisha uhifadhi wa mazingira na rasilimali za asili.
Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na mataifa mbalimbali, Masauni alisema makubaliano yaliyofikiwa na nchi kama Oman, Singapore, Japan na Korea yanahusu ushirikiano wa kiuchumi na kufungua masoko ya biashara, badala ya kuhamisha umiliki wa rasilimali za Tanzania.
