Hali ya usalama bado ni mbaya, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikiwa ni mwaka mmoja kamili tangu kutiwa saini kwa mkataba wa amani kati ya serikali ya Kinshasa na Kigali jijini Washington nchini Marekani.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Tangu kutiwa saini kwa mkataba huo kati ya rais Felix Tshisekedi na Paul Kagame wa Rwanda, mapigano bado yanashuhudiwa kati ya wanajeshi wa serikali FARDC na waasi wa AFC/M23.
Mkataba huo wa Washington, ulisainiwa Juni tarehe 27 mwaka 2025, kwa lengo la kumaliza vita kati ya vikosi vya DRC na waasi wa AFC/M23 wanaoungwa mkono na Rwanda.
Miongoni mwa mambo yaliyokuwa yafanyike ni kuondoka kwa wanajeshi wa Rwanda Mashariki mwa DRC, ndani ya siku 90 baada ya kusaini kwa mkataba huo.
Aidha, serikali ya DRC ilikuwa iache kuwaunga mkono waasi wa FDLR ambao walikimbilia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya mauaji ya kimbari mwaka 1994.
Mwaka mmoja baadaye, hakuna kilichotekelezwa kwenye mkataba huo kati ya DRC na Rwanda huku Marekani ikisema Juni 25 mwaka huu kuwa, inataka mkataba huo utekelezwe mara moja.
Hata hivyo, katika kipindi hiki, Marekani imetangaza vikwazo dhidi ya wakuu wa kijeshi wa Rwanda, huku wiki hii Wasington ikitangaza vikwazo dhidi ya mtandao wa madini wa Rwanda unaohusishwa na kundi la waasi la AFC/M23.