Arusha. Wafanyabiashara wadogo na wa kati nchini sasa wataweza kupata mtaji wa muda mfupi kwa urahisi zaidi baada ya Benki ya NMB, kwa kushirikiana na Mastercard, kuzindua NMB SME’s World Business Credit Card, bidhaa inayolenga kurahisisha upatikanaji wa fedha bila kupitia taratibu ndefu za mikopo na hitaji la dhamana kubwa.
Uzinduzi wa kadi hiyo umefanyika jana, Ijumaa, Juni 26, 2026, jijini Arusha, ukilenga kuziba pengo la upatikanaji wa fedha za haraka ambazo mara nyingi zimekuwa zikikwamisha ukuaji wa biashara ndogo na za kati.
Kadi hiyo inamwezesha mfanyabiashara kupata mkopo wa hadi Sh50 milioni kulingana na sifa zake za kifedha, huku ikimruhusu kufanya ununuzi wa bidhaa na huduma na kulipa baadaye bila riba ndani ya siku 53.
Ofisa Mkuu wa Biashara w a Benki ya NMB, Filbert Mponzi akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kadi Maalum SME Mastercard jijini Arusha.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ofisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, amesema bidhaa hiyo imebuniwa mahsusi kutatua changamoto ya ukosefu wa mtaji wa haraka licha ya kuwepo kwa biashara zenye uwezo wa kukua.
“Huu si uzinduzi wa kadi tu, bali ni nyenzo mpya ya kuwawezesha wafanyabiashara kuendelea kusonga mbele hata pale biashara inapohitaji unafuu wa muda mfupi wa kifedha,” amesema.
Amesema kupitia kadi hiyo, wafanyabiashara wataweza kununua bidhaa kutoka kwa wasambazaji au kulipia huduma mbalimbali kwa mkopo bila kupitia mchakato mrefu wa kuomba mkopo benki.
Kwa mujibu wake, badala ya kujaza fomu na kuwasilisha dhamana, mfanyabiashara atatumia kiwango cha fedha alichoidhinishwa nacho moja kwa moja kufanya malipo.
“Ukiwa unatumia mkopo huu ndani ya siku 53, hautatozwa riba yoyote. Ukivuka muda huo, utaanza kutozwa riba. Hizi ni fedha ambazo kwa taratibu za kawaida za kibenki zingehitaji mchakato mrefu wa maombi na dhamana,” amesema.
Mponzi amesema huduma hiyo itawawezesha wafanyabiashara kuongeza bidhaa dukani, kulipa wasambazaji kwa wakati na kutumia fursa za biashara zinapojitokeza bila kuchelewa kutokana na mchakato wa mikopo.
Aidha, amesema watumiaji wa kadi hiyo watanufaika na bima ya matibabu ya hadi dola 100,000 za Marekani wanaposafiri nje ya nchi, bima ya mizigo pamoja na huduma za VIP Lounge katika zaidi ya viwanja vya ndege 400 duniani.
Amesema kadi hiyo pia inakubalika katika mtandao wa Mastercard duniani kote, hivyo kurahisisha malipo ya kimataifa kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara za kuvuka mipaka.
“Kupitia kadi hii, wafanyabiashara wataweza kufanya miamala ya kimataifa kwa urahisi na usalama zaidi, jambo litakalowasaidia kupanua biashara zao nje ya Tanzania,” amesema.
Ofisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (katikati), Mkurugenzi wa Mastercard anayesimamia biashara za SME Afrika Mashariki, Imelda Ngunzu, na Meneja wa NMB Kanda ya Kaskazini, Baraka Ladislaus, wakizindua rasmi kadi ya biashara ya NMB SME World Business Credit Card iliyotolewa na Benki ya NMB kwa ushirikiano na Mastercard jijini Arusha.
Mponzi amesema huduma hiyo ni sehemu ya mkakati wa NMB wa kuboresha mazingira ya biashara kupitia mtandao mpana wa matawi zaidi ya 250, mawakala zaidi ya 80,000 na ATM zaidi ya 700, pamoja na bidhaa nyingine kama Business Accountna Mshiko Fasta.
Mkurugenzi wa Biashara wa Mastercard Afrika Mashariki, Imelda Ngunzu, amesema changamoto kubwa ya biashara nyingi si ukosefu wa wateja bali ni upatikanaji wa mtaji wa haraka unaokidhi mahitaji ya soko.
Amesema biashara nyingi hukwama kuongeza bidhaa, kununua kutoka kwa wasambazaji au kufanya biashara za kimataifa kutokana na mzunguko mdogo wa fedha.
“Biashara nyingi hukutana na vikwazo wakati wa kununua bidhaa kutoka kwa wasambazaji, kusimamia mzunguko wa fedha na kupanua biashara zao. Upatikanaji wa mtaji kwa wakati sahihi unaweza kuwa tofauti kati ya kupoteza fursa na kukua kwa biashara,” amesema.
Mkurugenzi wa Mastercard anayesimamia SME Commercialization Afrika Mashariki, Imelda Ngunzu, akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kadi maalumu iliyofanywa na Benki ya NMB kwa ushirikiano na Mastercard.
Amesema ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali nchini, ambapo miamala ya simu ilifikia takribani bilioni 6.4 mwaka 2024 yenye thamani ya karibu Sh trilioni 200, linaonyesha umuhimu wa suluhisho za kifedha za haraka na salama.
Kwa mujibu wake, biashara ndogo na za kati zinachangia zaidi ya asilimia 90 ya biashara zote nchini, asilimia 27 hadi 35 ya Pato la Taifa na kuajiri zaidi ya Watanzania milioni tano, hivyo kuboreshwa kwa upatikanaji wa mitaji kutachochea ukuaji wa uchumi.
“Lengo letu si kuwezesha malipo pekee, bali ni kuwawezesha wafanyabiashara kupata fursa, kukua na kuhimili mazingira ya biashara yanayobadilika kwa kasi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Biashara wa NMB, Deogratius Shirima, amesema upatikanaji wa mtaji pekee hautoshi bila mifumo bora ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.
Amesema NMB imeendelea kuwekeza katika huduma za kidijitali kama QR, PayByLink na mashine za POS ili kurahisisha malipo, kuboresha mzunguko wa fedha na kusaidia wafanyabiashara kulipa wasambazaji kwa wakati.
“Huduma hizi zimebuniwa kuwasaidia wateja wetu kukusanya mapato kwa haraka, kuboresha mzunguko wa fedha na kukuza biashara zao,” amesema.
Amesema ni muhimu kwa wafanyabiashara kuachana na utegemezi wa fedha taslimu pekee ili kunufaika kikamilifu na fursa za uchumi wa kidijitali.