PATI la ubingwa wa tano mfululizo wa Yanga wa Ligi Kuu Bara linazidi kunoga baada ya nyota wa timu hiyo, Allan Okello, kufunga mabao matatu (hat -trick) katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Okello ameanza kuipa Yanga furaha baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 27, likiwa ni lake la 12 katika Ligi Kuu Bar, tangu ajiunge na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026 akitokea Vipers SC ya kwao Uganda.
Mchezaji huyo amefunga bao hilo baada ya kutumia vyema pasi ya mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Prince Dube na kuuzamisha mpira wavuni uliomshinda kipa wa TRA United, Jean-Noel Amonome, huku mabeki wa kikosi hicho wakidhani tayari alikuwa katika eneo la kuotea.
Katika mechi hiyo ilishuhudiwa Yanga ikitengeneza mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la TRA United, tofauti na wapinzani wao ambao muda mwingi walionekana kucheza kwa tahadhari kubwa ya kujilinda huku wakishambulia kwa kushtukiza zaidi.
Kipindi cha pili kikaendelea kwa Yanga kulishambulia lango la wapinzani wao ambapo dakika ya 51, Allan Okello alifunga bao la pili na la 13, kwake kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa TRA United, Christopher Tebandeke kuunawa mpira katika eneo la hatari na mwamuzi, Saad Mrope wa Dodoma kuipa Yanga faida hiyo.
Wakati TRA United ikijipanga kwa ajili ya kusawazisha mabao hayo, Allan Okello akazidi kupeleka kilio kwa timu hiyo baada ya kufunga bao la tatu la dakika ya 60, ikiwa ni Hat-Trick yake ya kwanza katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Hat-Trick hiyo ya Okello inakuwa ni ya kwanza kwa Yanga msimu huu lakini ni ya nne kufungwa katika Ligi Kuu Bara, baada ya Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars, Mathew Momanyi wa Pamba Jiji na Fabrice Ngoy wa Namungo FC kutangulia kufunga pia.
Mabao hayo matatu yanamfanya Okello kufikisha jumla ya mabao 14, ya Ligi Kuu Bara na kukoleza vita mpya ya ufungaji bora akiwa sawa wa Mrundi wa Singida Black Stars, Mossi Ndumumwe wenye 14, wakizidiwa na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga 15.
Huu unakuwa ni ushindi wa kwanza kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara msimu huu dhidi ya TRA United, baada ya mechi ya kwanza kati ya miamba hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha Machi 18, 2026, kutoka suluhu ya (0-0).
Ushindi huo ni muhimu zaidi kwa Yanga inayosaka taji la tano mfululizo la Ligi Kuu Bara, kutokana na upinzani mkali unaoendelea kati yao na watani zao wa jadi Simba ambayo ndio mshindani aliyebakia kwa kikosi hicho cha mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini, Dar es Salaam.
Hata hivyo, mechi za mwisho wa msimu wa 2025-2026, zitakazopigwa Jumanne ya Juni 30, 2026, ndizo pia zitakazoamua bingwa wa Ligi Kuu Bara, japo ushindi huu kwa Yanga kwa sasa unaiweka katika mazingira mazuri zaidi tofauti na wapinzani wao.
Yanga itahitimisha msimu ugenini dhidi ya maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, ambapo ikiwa itashinda itatwaa rasmi ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara, japo hata ikitoa sare huenda ikatwaa pia, kutokana na wingi wa mabao ya kufunga na kufungwa iliyonayo sasa.
DIARRA ATWAA TUZO YA KIPA BORA
Wakati Yanga ikikaribia kusherehekea pati la ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara, Djigui Diarra ametwaa tuzo ya kipa bora wa msimu huu wa 2025-2026 baada ya kufikisha clean sheet 17 ambazo haziwezi kufikiwa na makipa wengine kwa mechi moja iliyobakia.
Clean Sheets 17 za Diarra ni sawa na alizokuwa nazo pia msimu uliopita wa 2024-2025, japo alizidiwa mbili na kipa wa Simba, Moussa Camara aliyeibuka kidedea baada ya kufikisha 19, ikiwa ni msimu wake wa kwanza tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea Horoya AC ya kwao Guinea.
Kipa aliyekuwa katika nafasi nzuri ya kushindana na Diarra ni Mahamadou Tanja Kassali wa Simba, ambaye hata hivyo, kikosi hicho kisiporuhusu bao lolote ataishia na 16, ambazo haziwezi kumfia Diarra anayehitaji Clean Sheets moja ili kuivunja rekodi yake aliyoweka kwa msimu uliopita wa 2024-2025.