Moshi. Mkoa wa Kilimanjaro umeweka mkakati wa kuhakikisha mashauri yote ya jinai yanamalizika ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu tangu yanapofunguliwa mahakamani, hatua inayolenga kuharakisha utoaji wa haki na kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani.

Mkakati huo umetangazwa leo wakati wa mafunzo ya pamoja yaliyozikutanisha taasisi za upelelezi, waendesha mashtaka na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kilimanjaro yaliyojikita katika kuimarisha uwezo wa taasisi hizo kukabiliana na uhalifu unaozidi kubadilika na kutumia mbinu za kisasa.

Akizungumza katika mafunzo hayo leo Jumamosi Juni 27, 2026, Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro, Ester Martine amesema ushirikiano kati ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Jeshi la Polisi na Takukuru ni msingi muhimu katika kuhakikisha uchunguzi na usikilizwaji wa mashauri unafanyika kwa haraka.

Amesema tayari mkoa umeanza kupunguza muda wa usikilizwaji wa mashauri ya jinai hadi chini ya miezi mitatu, hatua ambayo imechangia kupunguza msongamano wa mahabusu magerezani pamoja na kupunguza malalamiko ya wananchi kuhusu kuchelewa kwa haki.

“Tumeweka mkakati kwamba shauri linapofunguliwa lisikilizwe kwa haraka na ndani ya miezi mitatu liwe limeamuliwa. Hii itasaidia kupunguza msongamano wa mahabusu na malalamiko ya wananchi kuhusu haki jinai,” amesema Martine.

Aidha, amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza ufanisi kwa wachunguzi na waendesha mashtaka katika ukusanyaji wa ushahidi, uendeshaji wa kesi pamoja na matumizi ya mbinu za kisasa za uchunguzi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa maslahi ya umma.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa amesema mabadiliko ya teknolojia yamebadilisha pia namna uhalifu unavyotekelezwa, hivyo vyombo vya dola vinapaswa kuongeza ujuzi na ushirikiano ili kukabiliana na changamoto hizo.

Amesema sehemu kubwa ya uhalifu wa sasa hupangwa na kutekelezwa kupitia mitandao ya mawasiliano, jambo linalohitaji wataalamu wenye uelewa wa mbinu za kisasa za uchunguzi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amewataka watendaji wa vyombo vya dola kuimarisha uwezo wa uchunguzi wa kifedha na ufuatiliaji wa mali zinazotokana na uhalifu, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kupambana na uhalifu wa kiuchumi, rushwa na utakatishaji wa fedha.

Aidha, amesisitiza kasi ya uchunguzi wa mashauri iongezwe zaidi, akisema pamoja na kuweka ukomo wa miezi mitatu bado inawezekana mashauri kukamilika kwa muda mfupi zaidi iwapo mipango itaboreshwa.

“Hata kama tumejiwekea miezi mitatu, naamini mkiamua na mkajipanga vizuri mnaweza kufanya kazi kwa haraka zaidi bila kuathiri ubora wa uchunguzi,” amesema RC Babu.

Pia, ameagiza hatua kali za kisheria ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wahusika wa makosa makubwa yakiwemo ulawiti wa watoto, biashara ya dawa za kulevya na mauaji.

Kwa upande wake, Wakili wa Takukuru mkoani humo, Furahini Kibanga amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kuongeza ujuzi wa kukusanya, kuhifadhi na kuwasilisha ushahidi kwa viwango vinavyokubalika mahakamani, jambo litakalosaidia kuboresha uendeshaji wa mashauri ya jinai.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *