Kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema, “Iwapo adui atafanya kosa na kuanzisha vita vipya, vita hivyo havitakuwa tena kama vita vya tatu vya kulazimishwa, bali vitasababisha hasara na maafa makubwa ya kibinadamu.

Mohsen Rezaei, aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati wa Vita vya Miaka Minane vya Kujihami vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran amesema hayo katika mahojiano na mtandao wa NewsNation wa Marekani:

“Mojawapo ya matatizo makubwa ambayo Iran imekuwa nayo na serikali za Marekani katika kipindi cha miaka 47 iliyopita ni kwamba, hazijawahi kujitahidi kusikiliza kwa makini, kuelewa na kuamini misimamo halisi ya Iran. Badala yake, mara nyingi zimekuwa zikiongozwa na taarifa na ushawishi wa mashirika ya ujasusi ya Israel au watu wasiouridhia mfumo wa Kiislamu wa Iran. Hilo ndilo tatizo kubwa zaidi la Marekani.”

Kamanda Mkuu wa zamani wa SEPAH ameongeza kuuwa, “Serikali ya Marekani inapaswa kutambua haki za taifa la Iran na kukubali kwamba wananchi wa Iran wana haki zao zinazotambuliwa, na kwamba Iran inatekeleza shughuli zake ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, huku mahusiano yake ya kimataifa pia yakifuata misingi ya sheria hizo.

Jambo la pili ni kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi na kuachiliwa kwa mali za Iran zilizozuiliwa. Suala la tatu ni mamlaka ya Iran juu ya Mlango wa Bahari wa Hormuz, ambao ni sehemu inayomilikiwa na Iran.

Mohsen Rezaei amesema akiwahutubu wananchi na familia za Marekani:

“Sisi tunawatenganisha wananchi wa Marekani na serikali ya Marekani. Hatuna kabisa nia ya kuona wananchi wa Marekani wakipata mateso au madhara yoyote. Kwa hiyo, wananchi wa Marekani wanapaswa kufahamu kwamba hakuna tishio wala hatari yoyote kutoka kwa taifa au serikali ya Iran dhidi yao. Hata hivyo, tutasimama imara dhidi ya jeshi la Marekani na vitendo vyovyote vya uchokozi vinavyofanywa na serikali ya Washington na tutajilinda kwa nguvu zote.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *