Mji mkuu wa Ireland, Dublin, umeshuhudia kufanyika kwa wakati mmoja shughuli mbalimbali za wananchi na matukio ya michezo yaliyolenga kuunga mkono Palestina na kupinga kuanzishwa uhusiano wa kimichezo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Quds (Qudsna), kwenye moja ya madaraja makuu ya mji wa Dublin, wafuasi wa vilabu 9 vya michezo vya Ireland walikusanyika katika kampeni iliyopewa kaulimbiu ya “Sitisheni Mchezo” (Stop the Game).

Washiriki hao walibeba mabango yenye jumbe mbalimbali wakitaka kupingwa aina yoyote ya  uhusiano wa kimichezo na utawala wa Kizayuni wa Israel, na pia walitoa wito wa kususiwa  timu za michezo za Israel au timu zinazoshiriki katika mashindano ya kimataifa zikiwa zinaiwakilisha Israel.

Washiriki wa kampeni hiyo walisisitiza kuwa, hatua hiyo ni sehemu ya shinikizo la wananchi na wanamichezo la kushinikiza kusitishwa ushiriki wa timu za Israel katika mashindano ya kimataifa. Walisema kuwa, kuendelea ushiriki wa timu hizo huku vita dhidi ya Ukanda wa Gaza vikiendelea ni aina ya kuhalalisha kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa kivamizi, jambo ambalo wanapinga.

Wakati huohuo, katika eneo jingine la mji wa Dublin, CodePink iliandaa mkusanyiko wa maandamano ya kupinga na kuonesha mshikamano, ikitaka kuachiwa huru wafungwa wa Palestina wanaoshikiliwa katika magereza ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Washiriki wa mkusanyiko huo pia walipaza sauti na kutoa nara na kaulimbiu zilizolaani sera za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Shughuli hizi zinafanyika katika mwendelezo wa wimbi linalozidi kuongezeka la harakati za wananchi katika miji mbalimbali ya Ulaya. Harakati hizo zinataka kuwekwa vikwazo vya kimichezo na kisiasa dhidi ya Israel na kupanuliwa kampeni za mshikamano na wananchi wa Palestina, hasa katika kipindi ambacho vita dhidi ya Ukanda wa Gaza vinaendelea na kuacha madhara makubwa ya kibinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *