Leo ni Jumapili 13 Mfunguuo Nne Muharram 1448 Hijria mwafaka na 28 Juni 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita, yaani sawa na tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Bin Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa waziwazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na wafuasi wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wacha-Mungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abdullah bin Afif usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkatakata kwa mapanga.   

***

Miaka 153 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Dakta Alexis Carrel, mwanabiolojia na mwanafalsafa wa Kifaransa. Msomi huyo alizaliwa katika mji wa Lyon. Mwaka 1912 Dakta Carrel alitunukiwa tuzo ya heshima ya Nobel kutokana na mchango wake mkubwa katika uwanja wa tiba. Alitumia kipindi fulani katika maisha yake kutalii na kuzitembelea nchi mbalimbali zikiwemo za Kiislamu na kushuhudia kwa karibu mila na tamaduni za nchi hizo. Kwa sababu hiyo Dakta Alexis Carrel amesisitiza mno katika maandishi na vitabu vyake juu ya umuhimu na nafasi ya dini na masuala ya kiroho katika maisha ya mwanadamu. Nadharia nyingi za msomi huyo zimo katika kitabu mashuhuri alichokipa jina la “Mwanadamu, Kiumbe Asiyefahamika” ambamo ndani yake anapinga demokrasia ya Kimagharibi.

***

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Juni 1914 aliuawa Franz Ferdinand, mrithi wa kiti cha ufalme wa Austria akiwa pamoja na mkewe, wakati alipokuwa safarini Sarayevo, mji mkuu wa Bosnia Herzegovina ya leo, baada ya kufyatuliwa risasi na mwanachuo mmoja wa Kiserbia. Mara baada ya kutokea shambulio hilo, serikali ya Austria ilitaka ipewe nafasi ya kuingilia kati uchunguzi wa faili la kesi hiyo, jambo lililopingwa na serikali ya Serbia. Baada ya kupita mwezi mmoja tu, Austria ilianza kuishambulia Serbia kwa kisingizio hichohicho, na kuanzia mwezi Agosti mwaka huohuo, vikaanza rasmi Vita vya Kwanza vya Dunia baada ya Ujerumani kuamua kuiunga mkono Austria na ikaishambulia ardhi ya Ubelgiji. 

***

Siku kama ya leo miaka 69 iliyopita, yaani tarehe 28 Juni mwaka 1957, Kituo cha Kiislamu mjini Washington, Marekani kilianzisha rasmi shughuli zake. Ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1949 kwa ushirikiano wa Waislamu wa nchi hiyo na baada ya kuanza kazi hapo mwaka 1957 kiligeuka na kuwa alama yao ya kidini. Kituo cha Kiislamu cha Washington, mji mkuu wa Marekani kinajumuisha msikiti, shule, maktaba na kadhalika. Ratiba na shughuli mbalimbali za kidini zilizokuwa zikifanyika katika kituo hicho ni miongoni mwa mambo yaliyowafutia sana Waislamu na wasiokuwa Waislamu katika eneo hilo muhimu. Shughuli za kituo hicho zilipelekea viongozi wa serikali ya nchi hiyo, kutafuta vijisababu vya kubana kazi zake au kukifunga kabisa. 

***

Katika siku kama ya leo miaka 45 iliyopita mwafaka na tarehe 7 mwezi wa Tir mwaka 1360 Hijria Shamsiya, Ayatullah Dakta Muhammad Beheshti aliuawa shahidi akiwa pamoja na watu wengine 72 waliokuwa miongoni mwa shakhsiya bora wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya kuripuliwa kwa bomu ofisi kuu ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu. Ayatullah Beheshti pia alikuwa miongoni mwa shakhsiya wa awali waliotoa mchango mkubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu. Dakta Beheshti pia alikuwa mmoja kati ya wasaidizi wakuu wa Imam Khomeini. Mlipuko huo wa bomu uliwaua shahidi Dakta Beheshti na wasaidizi 72 wa Imam Khomeini wakiwemo mawaziri na wabunge kadhaa.

***

Miaka 39 iliyopita katika siku kama ya leo mji wa Sardasht huko magharibi mwa Iran ulishambuliwa kwa mabomu ya kemikali na ndege za kivita za utawala wa zamani wa Iraq. Raia wasio na ulinzi 110 wa Iran wakazi wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 530 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya utawala wa zamani wa Saddam Hussein. Utawala wa Saddam ambao ulikuwa umekata tamaa ya kupata ushindi katika medani za vita dhidi ya Iran ulikuwa ukidhani kwamba kwa kufanya mashambulizi hayo ya kemikali dhidi ya raia wa mji wa Sardasht ungeweza kulitwisha taifa la Iran matakwa yake. Taasisi muhimu za kimataifa na madola makubwa duniani hata hivyo hazikuchukua hatua yoyote ya jadi ya kuuzuia utawala wa Saddam kutumia silaha za kemikali wala hata kulaani jinai hizo ulizozifanya dhidi ya raia wasio na hatia wa Iran.

***

Siku kama ya leo miaka 20 iliyopita sawa na tarehe 28 mwezi Juni mwaka 2006 jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Utawala wa Kizayuni uliendesha mashambulio hayo ya kinyama kwa kisingizio cha kuuawa wanajeshi wake wawili siku tatu kabla ya mashambulio hayo. Israel ilidai kuwa wanamapambano wa Palestina walifanya oparesheni katika kituo kimoja cha upekuzi na kuua wanajeshi wake wawili na kumkamata mateka mwingine mmoja. Idadi kadhaa ya mawaziri, wabunge na wawakilishi wa baraza la mji la serikali halali ya Palestina iiliyokuwa ikiongozwa na Hamas walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel katika siku za kwanza za mashambulizi hayo makubwa ya jeshi yaliyopewa jina la “Mvua za Kiangazi”.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *