Moshi. Benki ya NMB imewaasa wafanyabiashara mkoani Kilimanjaro kuendeleza utamaduni wa kuweka akiba ili kukuza biashara zao.

Mbali na kuwahamasisha benki hiyo imewapa elimu ya fedha nankuwaeleza fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya benki hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa NMB Business Club uliowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali mkoani humo, Meneja Mwandamizi wa Idara ya Biashara wa NMB Makao Makuu, Leonard Tony, amesema benki hiyo imewakutanisha wateja, wadau na wateja watarajiwa ili kuwafahamisha huduma, bidhaa na maboresho mbalimbali yanayoendelea kutolewa.

Alisema miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele ni umuhimu wa wafanyabiashara kuweka akiba kwenye akaunti zao, hatua inayoiwezesha benki kutathmini mwenendo wa biashara zao na kurahisisha upatikanaji wa mikopo pamoja na usimamizi wa marejesho.

“Akiba huwasaidia wafanyabiashara kujenga historia nzuri ya kifedha ambayo hutuwezesha kutambua uwezo wa biashara zao na kurahisisha utoaji wa mikopo pamoja na marejesho kwa wakati,” alisema Tony.

Aliongeza kuwa NMB inaendelea kutoa elimu kuhusu namna bora ya kuendesha biashara, kutunza kumbukumbu za kifedha na kuzingatia sheria na taratibu za nchi ili kuhakikisha biashara zinakuwa endelevu.

Kwa upande wake, msambazaji wa Taifa Gas Mkoa wa Kilimanjaro, Maria Olomi, alisema ushirikiano wake na NMB umechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa biashara yake tangu alipoianzisha.

“Nimekuwa mteja wa NMB tangu nilipoanza biashara. Benki hii imenikuza na kunifikisha hapa nilipo. Tumekuwa tukipata mikopo yenye riba nafuu ambayo imetusaidia kupanua biashara zetu. Kwetu sisi, NMB ni benki rafiki,” alisema.

Naye mfanyabiashara wa Moshi, Gidan Parma, alisema NMB imeendelea kuwa mshirika muhimu wa wafanyabiashara wa makundi mbalimbali kwa kuwawezesha kupata mitaji kupitia huduma zake za mikopo.

“Benki ya NMB ina mchango mkubwa kwa wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa. Kupitia huduma zake za mikopo imewawezesha wajasiriamali wengi kukuza biashara zao na kuongeza kipato,” alisema.

Alisema huduma zinazotolewa na benki hiyo zimeendelea kuwanufaisha wananchi wengi na kuchochea ukuaji wa biashara katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *