
Kiungo wa zamani wa Ujerumani, Toni Kroos ameonyesha wasiwasi juu ya mwenendo wa timu hiyo katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, akisema sio kizuri.
Kroos ambaye alikuwemo katika kikosi cha Ujerumani kilichotwaa taji hilo mwaka 2014, amesema kuwa timu hiyo inatakiwa kubadilika vinginevyo haoni kama itaweza kutwaa ubingwa au kufika mbali.
“Inapaswa iwe vigumu kwa wapinzani kucheza dhidi yetu. Hiyo ina maana tunapaswa kuwa na uwezo wa kulinda vizuri na kupambana kwa nguvu. Hilo bado hatulifanyi. Pia tunahitaji Musiala (Jamal) na Wirtz (Florian) wawe katika kiwango chao bora, jambo ambalo halipo kwa sasa.
“Ikiwa mambo hayo mawili hayatabadilika, hatutafika mbali kwenye mashindano haya. Zamani tulikuwa na mechi ambazo tulicheza vibaya pia, kama dhidi ya Algeria. Lakini bado tuliweza kushinda hata tulipocheza vibaya. Sidhani kama timu hii ya sasa ina uwezo huo,” alisema Kroos.
Kroos ameongeza pia kuwa timu hiyo kupoteza mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Ecuador kwa mabao 2-1, kulitokana na dharau ambayo ilionyesha kwa wapinzani.
“Hii ni timu inayojitoa kwa kila hali. Hata hivyo, sikubaliani na kocha aliposema kuwa hali ya kujiamini kupita kiasi haikuchangia kabisa. Unapokuwa tayari umefuzu, jambo hilo huwa linabaki akilini mwako.
“Huwezi kulipuuzia kabisa kwa sababu ni jambo la kawaida kwa binadamu. Ukweli ni kwamba sisi si timu yenye nguvu kubwa katika mapambano ya kimwili,” alisema Kroos.