Iran na Oman zimefanya mkutano wa kwanza wa kamati mpya ya pamoja ya Hormuz, unaojadili usimamizi wa baadaye wa Lango-Bahari la Hormuz.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na Sheria na Masuala ya Kimataifa, Kazem Gharibabadi, ametoa tangazo hilo katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X leo Jumatatu.

Gharibabadi amesema mkutano huo ulifanyika wakati wa ziara yake huko Muscat na ulihudhuriwa na Abdulaziz al-Hinai, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman.

Amesema, pande hizo mbili zilijadili masuala ya Lango-Bahari la Hormuz na usimamizi wake wa baadaye.

Iran ilifunga njia hiyo muhimu ya majini kwa maadui na washirika wao baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Tehran Ilidhibiti kikamilifu lango hilo baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza mzingiro haramu wa majini dhidi ya meli na bandari za Iran kinyume cha masharti ya kusitisha mapigano yaliyotangazwa Aprili 7.

Baadaye mkataba wa maelewano ulioandaliwa na Pakistan ulisainiwa kati ya Tehran na Washington kwa lengo la kukomesha hali hiyo iliyosababishwa na uchokozi wa Marekani.

Kifungu cha tano cha mkataba huo (MoU) kinasisitiza utambuzi wa mamlaka ya Iran juu ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa Gharibabadi: “Wakati wa mkutano huo, sambamba na kupitia masuala ya sasa kuhusu Lango Bahari la Hormuz, tulibadilishana maoni kuhusu usimamizi wake wa baadaye ndani ya mfumo wa kifungu cha tano cha Mkataba wa Maelewano wa Islamabad na haki za mamlaka za nchi za pwani wa lango hilo.”

Mkutano huo unafuatia taarifa ya pamoja iliyotolewa na pande hizo mbili tarehe 22 Juni baada ya ziara ya Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araqchi mjini Muscat.

Katika taarifa hiyo, Oman na Jamhuri ya Kiislamu zilisisitiza kwamba mipango yote kuhusu Lango-Bahari la Hormuz lazima iheshimu kikamilifu mamlaka na haki za kujitawala mataifa mawili ya pwani wa Hormuz.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *