
Kamanda wa Jeshi la Iran amesema Jamhuri ya Kislamu imepata mafanikio endelevu katika teknolojia ya ulinzi wa ndege zisizo na rubani na anga licha ya madai ya uhasama ya vyombo vya habari.
Naibu Kamanda wa Jeshi la Ulinzi wa Anga la Iran Brigedia Jenerali Mohammad Yousefi Khoshqalb ametoa matamshi hayo katika mahojiano na Defapress yaliyochapishwa Jumatatu, ambapo alikanuusha vikali madai yaliyotolewa hivi karibuni ya vyombo vya habari vya kigeni kwamba mifumo ya ulinzi wa angani ya Iran imedhoofika.
“Programu mbalimbali zinazofanyika mara kwa mara kote nchini, pamoja na usalama kamili wa mipaka ya nchi kavu na majini na kutokuwepo vyombo vya uadui katika anga ya Iran, kunaonyesha nguvu, uhodari na utayari kamili wa mtandao jumuishi wa ulinzi wa anga katika mfumo tata na madhubuti,” amesema Brigedia Jenerali Khoshqalb.
Ameongeza kuwa Vikosi vya Jeshi la Iran vimefanikiwa kupenya mfumo wa kupambana na makombora wa utawala wa Israel, unaojulikana kama “Iron Dome”, na kutimiza malengo yaliyokusudiwa, akisisitiza kwamba mafanikio hayo ni ushuhuda wa nchi kuwa na “droni zenye nguvu sana na za kisasa zenye uwezo wa kipekee”.
“Uundaji na utumaji wa ndege zisizo na rubani zenye teknolojia ya kisasa kwenye uwanja wa vita sasa umekuwa jambo la kawaida katika Jeshi letu, na tunamshukuru Mungu, mchakato huu unaendelea kwa kasi na nguvu,” amesisitiza kamanda huyo wa Jeshi la Iran.
Akizungumzia uboreshaji wa mara kwa mara wa mifumo ya ulinzi wa anga, amesema matumizi ya vifaa vya “kisasa, bora na vyenye ufanisi” katika uwanja wa vita na usimamizi wa vita vya anga ni “mchakato wa kila siku na wa kudumu” ndani ya Jeshi la Ulinzi la Anga.
“Kwa kutegemea uwezo wa kisayansi, viwanda, na maarifa wa Jeshi la Ulinzi la Anga, Wizara ya Ulinzi, na Vikosi vya Jeshi, leo tunashuhudia mabadiliko na maendeleo endelevu katika mifumo ya ulinzi,” Khoshqalb amesema.
Awali, Msemaji wa Jeshi la Iran, Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia, alikuwa amesema kwamba nchi imeweza kutengeneza vifaa vya kijeshi vya kisasa zaidi wakati wa vita vya hivi karibuni vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kislamu.