
Dar es Salaam. Mazungumzo mapya ya kidiplomasia kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kufanyika Jumanne mjini Doha, Qatar, katika jaribio jipya la kurejesha mwafaka wa kusitisha mapigano uliokuwa umeanza kuyumba baada ya kuibuka tena mashambulizi ya kijeshi.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Axous nchini Marekani, pande hizo mbili zimekubaliana kusitisha mashambulizi katika Ghuba ya Uajemi na kuanza mazungumzo mapya kuhusu usalama wa Mlango Bahari wa Hormuz, hatua inayotazamwa kama inaweza kumaliza kabisa vita hivyo.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya mashambulizi mapya kuripotiwa na kuhofiwa kurejea kwa vita katika ukanda huo ambapo viongozi wa pande zote wamekuwa na kauli tata zikionesha kuzorota kwa makubaliano ya awali.
Mazungumzo hayo yaliyopangwa kufanyika Uswisi, sasa yanatarajiwa kufanyika Qatar kufuatia mapigano na kauli za kutunishiana misuli kwa viongozi wa Iran na Marekani. Moja ya kauli tata ni ile iliyochapishwa na Rais wa Marekani Donald Trump katika ukurasa wake wa ‘Truth Social’, akitishia kuwa Iran itashambuliwa na kufutwa duniani ikiwa Marekani itaamua kuachana na mazungumzo.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itashambuliwa na kuondolewa kabisa duniani ikifika hatua Marekani ikakosa tena uvumilivu na Tehran,” aliandika Trump Jumapili Juni 28, 2026 akijibu mashambulizi ya Iran hatua iliyoongeza kuzika ndoto za amani zilizofikiwa awali.
Mwafaka wa awali uliotiwa saini Juni 17 ulijumuisha kusitishwa kwa mashambulizi ya moja kwa moja, kufunguliwa kwa njia za mawasiliano za dharura na kuanza majadiliano kuhusu kuachiliwa kwa fedha za Iran zilizozuiwa nje ya nchi.
Hata hivyo, makubaliano hayo yalianza kuvunjika baada ya mashambulizi ya Israel na baadaye Marekani ambayo yalijibiwa na Iran na kuzorotesha makubaliano hayo.
Mvutano ulianzia katika usimamizi wa Mlango bahari wa Hormuz ambapo huduma zilirejea kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa (UN) na baadaye kukumbwa na mashambulizi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, akiwa Baghdad, Iraq, wiki iliyopita, alinukuliwa na DW akisema: “Jaribio lolote la kuingilia usimamizi wa Iran katika Mlango Bahari wa Hormuz litachukuliwa kama hatua ya uchokozi na litaongeza mvutano katika eneo lote.” Kauli hiyo ilitolewa wakati Tehran ikisisitiza kuwa Hormuz ni sehemu ya masilahi yake ya usalama wa taifa.
Siku chache baadaye Iran ilihusishwa na shambulizi la meli ya mizigo katika njia hiyo hatua iliyofanya UN kusitisha huduma zake za uokoaji na baadaye majibizano ya mashambulizi na Marekani yakarejesha mapigano mapya ambayo yameripotiwa hadi Jumapili Juni 28, 2026.
Mvutano huo umekuwa ukichochewa zaidi na udhibiti wa Mlango Bahari wa Hormuz, ambapo Iran inasisitiza kuwa usimamizi wake ni haki ya Tehran, wakati Marekani na washirika wake wakitaka uhuru wa usafiri wa kimataifa. Hii ndiyo inayotajwa kuwa hoja kuu inayosukuma mazungumzo ya Jumanne huko Doha.
Mzozo huo umeendelea kuiweka dunia katika mjadala wa kupanda kwa gharama za nishati tangu ulipopelekea bei ya mafuta kupanda hadi takriban Sh205,000 kwa pipa katikati ya vita kabla ya kushuka hadi takriban Sh190,000 baada ya kurejea kwa mwafaka wa amani.
Kufuatia mashambulizi mapya, soko la mafuta sasa liko katika hali ya tahadhari kali, likisubiri matokeo ya mazungumzo ya Jumanne, ambapo kushindwa kufikia makubaliano kunaweza kusababisha kupanda tena kwa bei na kuathiri uchumi wa dunia.
Kwa sasa, soko la mafuta linasubiri mazungumzo ya Doha kama hatua muhimu ya kidiplomasia kati ya vita na amani, ambapo kila kauli kutoka Washington, Tehran na Doha inaweza kubadilisha mwelekeo wa mgogoro na gharama za maisha ya dunia.