Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeruhusu mshtakiwa Gilbert Nyamitah (33) na Fabian Kulwa(40) kuanza kikao cha kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini( DPP) kwa ajili ya kuimaliza kesi yao.
Kikao hicho cha kwanza kitafanyika Julai 2, 2026 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao na wenzao wanne ambao hawajaandika barua ya kufanya majadiliano, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuongeza genge la uhalifu na kutumia laini za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine kujipatia fedha.
Pia, wanadaiwa kutumia vitambulisho vya Nida vya watu mbalimbali kusajili laini za simu za watu tofauti kinyume cha sheria pamoja na kutakatisha Sh355 milioni.
Uamuzi huo wa kuruhusu Jamhuri kufanya majadiliano na washtakiwa hao wawili, umetolewa leo Jumatatu Juni 29, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki.
Hakimu Nyaki ametoa uamuzi huo, baada ya upande wa Jamhuri kuieleza Mahakama hiyo kuwa wameshapitia barua za maombi za washtakiwa hao kukubaliana kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi.
Awali, wakili wa Serikali Titus Aron aliieleza Mahakama kuwa wamepokea maombi ya mshtakiwa Nyamitah na Kulwa ya kufanya majadiliano na DPP ya kuimaliza kesi yao.
Mshtakiwa Gilbert Nyamitah anayekabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo kutumia laini za simu zenye usajili wa watu wengine, akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
“Mheshimiwa hakimu, maombi hayo tumeyapitia na kukubaliana nayo, hivyo tunaomba kufanya kikao cha kwanza Julai 2, 2026,” amesema wakili Aron.
Hakimu Nyaki baada ya kusikiliza hoja hiyo, amekubaliana na ombi la upande wa Jamhuri na kisha kuahirisha kesi hadi Julai 6, 2026 kwa ajili ya kutajwa.
“Mahakama itatoka hati ya kuwaleta washtakiwa hao hapa Mahakamani wakitokea mahabusu Julai 2, 2026 ili waweze kufanya kikao cha kwanza cha majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka,” amesema Hakimu Nyaki na kisha kuahirisha kesi hiyo.
Katika kesi hiyo mshtakiwa Nyamitah na Kulwa wapo rumande kutokana na kuwa na shtaka la kutakatisha fedha ambalo halina dhamana, huku washtakiwa wengine wakiwa nje kwa dhamana.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 4, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 9426 ya mwaka 2026
Katika mashtaka mashitaka 28 yanayowakabili 16 ni ya kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, 10 ni ya kutumia kitambulisho cha Taifa (Nida) cha mtu mwingine kusajilia laini za simu, moja ni kuongoza genge na jingine ni kutakatisha Sh355 milioni.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, katika shitaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili wote, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Mei Mosi 2025 na Aprili 2026, eneo lisilojulikana ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, waliongoza genge la uhalifu kwa kutumia taarifa za wateja na kutumia laini za simu zenye usajili wa watu wengine na kadi za Nida za watu tofautitofauti bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.