Kundi la wanazuoni wanawake wa Iran, wasomi wa taaluma mbalimbali na wataalamu wa masuala ya utamaduni, limesambaza barua ya wazi likirekodi ukiukaji wa kimfumo uliofanywa na Marekani na Israel wakati wa vita vya hivi karibuni dhidi ya Iran, na limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za dharura za uwajibikaji.

Katika barua hiyo iliyotumwa kwa taasisi za kimataifa za sheria, mashirika ya haki za binadamu na taasisi za elimu duniani, wanazuoni hao wametoa ufafanuzi kuhusu mashambulizi ya tawala hizo mbili dhidi ya Iran yaliyolenga miundombinu ya kiraia, shule, vyuo vikuu na vituo vya tiba, wakitaka kufanyike uchunguzi huru na hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Sehemu ya barua hiyo inasema: “Tunaandika barua hii kama wanazuoni, wasomi, na wataalamu wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tukitimiza wajibu wetu wa kusema ukweli, kutetea uadilifu na kudai uwajibikaji kwa kuuawa shahidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na wanasayansi, wanazuoni, makamanda wa jeshi, walimu, wahudumu wa uokoaji na wanawake na watoto wasio na hatia waliouawa na majeshi vamizi ya Marekani na Israel katika vita hivi.”

Watiwa-saini wameorodhesha mauaji ya watu 3,519 katika mashambulizi hayo, huku wakieleza kwa uzito shambulio dhidi ya Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyebeh huko Minab, kusini mwa Iran, ambako kwa uchache raia 168 waliuawa, wakiwemo watoto 120.

Kwa mujibu wa barua hiyo, tukio hilo “limekuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi dhidi ya watoto katika kipindi chote cha vita.”

Barua hiyo pia imeeleza uharibifu mkubwa uliofanyika dhidi ya vyuo vikuu, vituo vya utafiti, hospitali, magari ya wagonjwa, miundombinu ya nishati na vyanzo vya maji, ikitaja mashambulizi hazo kuwa ni ukiukaji wa dhahiri wa sheria za kimataifa za kibinadamu na Mikataba ya Geneva.

Waliotia saini wamesema kuwa: “Lengo letu haliko tu katika kutaka kufanyike uchunguzi, uwajibikaji na haki. Bali pia tunataka kulinda kumbukumbu ya kihistoria na kuzuia kuzoeleka jinai ambazo hurudiwa mara kimya kinapopewa nafasi, kama tulivyoshuhudia katika miaka miwili iliyopita huko Palestina na sasa Kusini mwa Lebanon.”

Barua hiyo imeutaka Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa “kuilaani bila kusita” Marekani na utawala wa Kizayuni wa israel kwa kufanya uchokozi wa kijeshi, huku umoja huo ukitakiwa kuunga mkono mifumo huru ya uchunguzi wa kimataifa.

Aidha, watiwa-saini wametoa wito kwa jamii ya kimataifa kupitisha hatua za kususia, kuondoa uwekezaji na kuidhinisha vikwazo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na taasisi zinazounga mkono jinai zinazoelekezwa kwa Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *