Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, ametangaza kuwa kiasi cha dola bilioni 6 mali ya nchi hii zinazozuiliwa Qatar kufuatia mashinikizo ya Marekani, zitaachiliwa.

Amesema hatua hiyo inafuatia kutiliwa saini Hati ya Maelewano (MoU) ya Islamabad kati ya Iran na Marekani, kwa upatanishi wa Pakistan.

Akizungumza jana Jumatatu wakati wa mikutano yake na Marjaa mwandamizi wa Kiislamu, Ayatullah Shobeiri Zanjani mjini Qum, Rais Pezeshkian alisema: “Kwa mujibu wa mipango iliyoandaliwa, dola bilioni 6 kati ya jumla ya dola bilioni 12 za Iran zilizoko Qatar zitaachiliwa na kukabidhiwa kwa Tehran.

Ameongeza kuwa “juhudi na ufuatiliaji wa karibu zinaendelea” ili kuhakikisha urejeshwaji wa fedha hizo.

Pezeshkian ameutaja mkataba huo kati ya Iran na Marekani kama “ushindi mkubwa na adhimu kwa taifa la Iran,” akisisitiza kuwa vikwazo dhidi ya mafuta na sekta ya petrokemikali vimeondolewa kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Rais Pezeshkian amefafanua kuwa: “Mwishowe, Marekani imelazimika kuulazimisha utawala wa Kizayuni (Israel) na kuufanya ukubali mwongozo huo wa maelewano, ingawa utawala huo pamoja na baadhi ya makundi ya waungaji mkono utawala wa kifalme (uliotimuliwa Iran) wangali wanapinga vikali utekelezwaji wake.”

Mnamo Julai 18, marais wa Iran na Marekani walitia saini hati ya maelewano yenye vipengele 14 chini ya upatanishi wa Pakistan, inayotaka kukomeshwa kabisa uhasama katika medani zote, ikiwemo Lebanon, sambamba na kuondolewa vikwazo vya baharini dhidi ya Iran ndani ya siku 30, na kurejeshwa safari za kawaida za meli za kibiashara kupitia Lango Bahari la Hormuz.

Chini ya hati hiyo, Tehran na Washington zimeingia katika kipindi cha siku 60 cha mazungumzo ya kidiplomasia kwa lengo la kufikia mwafaka kamili na wa mwisho.

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Rais Pezeshkian amepongeza ustahimilivu na subira ya wananchi wa Iran dhidi ya mashinikizo na vitisho vya maadui wakati wa vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na muungano wa Marekani na Israel mnamo Februari 28.

Amesema kuwa, licha ya maadui kumuuwa shahidi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, mawaziri kadhaa, makamanda wa jeshi, wasomi na hata wanafunzi, taifa la Iran na Vikosi vyake vya Ulinzi vilisimama imara bega kwa bega kulinda heshima ya nchi na kuzuia maadui kufikia malengo yao khabithi.

Ameongeza kuwa Marekani na Israel zilitumia mbinu na uwezo wao wote kuvuruga utulivu wa ndani ya Iran, kupitia mashinikizo makali ya kiuchumi na kuchochea fitna za ndani ili kuidhoofisha Jamhuri ya Kiislamu.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa njama za maadui za kukwamisha gurudumu la maendeleo la Iran kwa kushambulia viwanda vya nchi, miundombinu ya gesi, viwanda vya chuma na vile vya petrokemikali zimegonga mwamba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *