Korea Kaskazini imekosoa vikali mazoezi ya kijeshi yanayoendelea kati ya Marekani na Japan, ikiituhumu Tokyo kutumia hali ya sasa ya dunia iliyojaa misukosuko kama kisingizio cha “kujihalalishia mabadiliko yake kuwa taifa la vita.”

Katika tahariri iliyochapishwa jana Jumatatu na Shirika Rasmi la Habari la Korea Kaskazini (KCNA), Pyongyang imelaani ushiriki wa Jeshi la Japan katika mazoezi ya kijeshi yanayojulikana kama Resolute Dragon, yanayofanywa kwa pamoja na wanamaji wa Marekani.

Mazoezi hayo yalianza Juni 20 katika visiwa vya Okinawa na Kyushu, kusini-magharibi mwa Japan, na yanatarajiwa kukamilika leo Jumanne.

Pyongyang imeonya kuwa hatua kama hizo zinachochea hali ya wasiwasi wa kiusalama na kuyumbisha utulivu wa eneo hilo.

Korea Kaskazini imeionya Japan kuhusu mazoezi hayo ya kijeshi na Marekani, ikikumbusha “mwisho wa kusikitisha” ulioyapata baadhi ya mataifa yaliyofuata kibubusa njia ya kujizatiti kijeshi.

Wakati huo huo, China imetangaza hatua mpya za udhibiti wa mauzo ya nje zinazolenga makampuni kadhaa ya Japan, huku Beijing ikizidisha mashinikizo kwa Tokyo kutokana na kuongezeka shughuli zake za kijeshi na mvutano unaohusiana na Taiwan.

Jana Jumatatu, Wizara ya Biashara ya China iliweka taasisi 20 za Japan kwenye orodha ya udhibiti wa mauzo ya nje, hatua inayozuia taasisi hizo kupata bidhaa za matumizi ya aina mbili (dual-use) zinazozalishwa nchini China.

Hatua hizo mpya zinakuja wakati mvutano kati ya Beijing na Tokyo ukiendelea kuongezeka kuhusu masuala ya usalama wa kikanda na sera ya Japan ya kupanua uwezo wake wa kijeshi.

Mahusiano kati ya nchi hizo yalianza kuzorota zaidi baada ya Waziri Mkuu wa Japan, Sanae Takaichi, kupendekeza mwaka uliopita kuwa Japan inaweza kuingilia kati iwapo China itatumia nguvu za kijeshi dhidi ya eneo la Taiwan ambayo limejitenga na China. Serikali ya China inasisitiza kuwa Taiwan ni sehemu ya nchi hiyo kwa mujibu wa sera ya ‘China Moja.”

Kwa upande wake, Tokyo imeendelea kupanua uwepo wake wa kijeshi kwa kusambaza makombora ya masafa marefu zaidi na kulegeza baadhi ya vizuizi vya usafirishaji wa silaha nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *