
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikitarajia kuadhimisha siku ya familia pamoja na siku ya mtoto wa Afrika leo Jumanne, Juni 30, 2026 wataalamu wa masuala ya malezi na saikolojia wameeleza familia ndiyo nguzo kuu ya kujenga kizazi chenye maadili na uwajibikaji.
Kwa kawaida siku ya familia duniani huadhimishwa kila ifikapo Mei 15 na mtoto wa Afrika huadhimishwa kila ifikapo Juni 16 ya kila mwaka.
Hata hivyo, kwa mwaka huu Tanzania, kupitia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dk Dorothy Gwajima ilitangaza kuadhimisha siku hizo kwa pamoja leo Jumanne, Juni 30, 2026 ikiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Mtoto ni malezi, msingi wa familia bora kwa Taifa imara.’
Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa malezi, Irene Mwakalinga amesema familia ndiyo taasisi ya kwanza ya malezi na ndiyo inayobeba jukumu la kumwandaa mtoto kuwa raia mwema.
Amesema mtoto huanza kujifunza maisha ndani ya familia kabla ya kuingia shuleni au kukutana na jamii pana, hivyo mazingira anayokulia yana mchango mkubwa katika kumjengea tabia, maadili na mtazamo wake kuhusu maisha.
“Jamii bora inaanza na familia inayofundisha uadilifu, heshima, uwajibikaji na kuthamini utu wa wengine. Mtoto anayekulia katika mazingira yenye upendo na maadili huwa na uwezekano mkubwa wa kuwa mtu anayeheshimu sheria na kuchangia maendeleo ya jamii,” amesema.
Irene amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa watoto wao kwa vitendo badala ya maneno pekee.
“Asilimia 70 mtoto huelewa na kujifunza kwa haraka kile anachokiona kwa vitendo na asilimia 30 tu ndiyo kwa kusikiliza kile anachoambiwa au kufundishwa,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dk Zena Mabeyo amesema mtoto anapozaliwa anakuwa hana uelewa juu ya jambo lolote linaloendelea duniani lakini mwalimu wake wa kwanza ambaye anakutana naye na kujifunza familia anayoishi.
“Matendo ambayo familia hiyo inayafanya kwa siku nzima pamoja na malezi ikijumlisha maamrisho na makatazo inayompatia mtoto nafasi kubwa ya kuamua mtoto huyo atakuwa ni wa namna gani,” amesema.
Amesema mtoto naye kama binadamu mzazi anaweza kujitahidi kumtengeneza mtoto wake katika maadili katika kila nyanja na baadaye mtoto akakengeuka.
“Anapotoka nje ya wazazi kuna mambo mengine ambayo huweza kuwa ni kichocheo kwa mtoto kukengeuka malezi aliopatiwa na wazazi, mambo kama masuala ya utandawazi, makundirika ambayo yanaweza kusababisha mabadiliko ya kimaadili kwa mtoto husika.”
Naye mwanasaikolojia, Charles Kalungu amesema changamoto nyingi zinazowaathiri vijana, ikiwamo matumizi ya dawa za kulevya, ukatili na kujiingiza katika makundi hatarishi, zinaweza kupunguzwa ikiwa familia zitajenga mawasiliano ya karibu na watoto.
Amesema katika ulimwengu wa sasa wenye maendeleo makubwa ya teknolojia, wazazi hawapaswi kuishia kuwapatia watoto mahitaji ya msingi pekee, bali wanapaswa kujua marafiki zao, matumizi yao ya mitandao ya kijamii na changamoto wanazopitia kila siku.
“Wazazi wanatakiwa kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao. Mazungumzo ya kila siku huwapa watoto nafasi ya kueleza hisia zao na kuwafanya wajisikie salama wanapokabiliwa na changamoto,” amesema.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Daniel Sendoro amesema ili kukiokoa kizazi cha sasa na kijacho juu ya tatizo la mmomonyoko wa maadili kuna haja ya wazazi kusimama katika nafasi yao katika malezi.
Ameongeza wazazi wanatakiwa kujikita katika kulea watoto na kuwatunza na kuacha tabia ya kutunza watoto pekee.
“Kuna tofauti kati ya kutunza na kulea mtoto, kulea ni kuelimisha, kuonya pamoja na kufuatilia na kutunza ni kuhakikisha amepata mahitaji yake muhimu kama chakula, malazi na makazi,” ameeleza.
Naye Sheik Ndembo amesisitiza familia kuweka muda wa pamoja wa mazungumzo, kula pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali ili kuimarisha mahusiano ndani ya nyumba.
Pia, wazazi wanatakiwa kuwalea watoto kwa usawa, kuwapa muda wa kuwasikiliza bila ubaguzi ili kujenga kujiamini na upendo kwa watoto wote.